Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Jimbo Katoliki la Albano, Italia, tarehe 21 Septemba 2019 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Jimbo Katoliki la Albano, Italia, tarehe 21 Septemba 2019 

Papa Francisko kutembelea Jimbo la Albano 21 Septemba 2019

ilikuwa ni tarehe 21 Septemba 1953, Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, Mwinjili, Baba Mtakatifu Francisko, wakati huo akiwa na umri wa miaka 17, wakati wa maungamo, kwa mara ya kwanza kutoka katika undani wa moyo wake, akasikia wito wa kuwa Padre! Mang’amuzi haya yakamsaidia kugundua ndani mwake kwamba: Yesu alikuwa anamsubiri, ili kumwonesha dira na mwelekeo wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma”, anasema kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Huruma na upendo huu, akaumwilisha katika maisha na utume wake wakati wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu; alipokuwa anawaondolea watu dhambi, kuwaponya magonjwa yao pamoja na kuwalisha wakati wa njaa na taabu! Kilele cha huruma na upendo wa Mungu kinajionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili kuweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hatimaye, kuanza hija inayoelekea nyumbani kwa Baba wa milele.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, msamaha ni chombo ambacho kimewekwa kwenye mikono dhaifu! Lakini Kristo Yesu ameifanya huruma kuwa ni kielelezo cha maisha na kipimo cha thamani ya imani ya waja wake. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu na anataka kuwaona waja wake wakiwa wamesheheni furaha! Waamini wakiguswa na huruma yake, wanaweza kuwa pia mashuhuda na vyombo vya huruma kwa jirani zao. Baba Mtakatifu anasema, Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya maisha mapya yanayosimikwa katika toba na wongofu wa ndani.

Hii ni Sakramenti inayomfanya mwamini aguse kwa mikono yake ukubwa wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake na hivyo inakuwa kwa hakika ni chimbuko la amani ya ndani na utulivu moyoni! Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho anasema Askofu Marcello Semeraro wa Jimbo Katoliki la Albano, nchini Italia ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Makardinali Washauri, kwamba ilikuwa ni tarehe 21 Septemba 1953, Siku kuu ya Mtakatifu Mathayo, Mwinjili, Baba Mtakatifu Francisko, wakati huo akiwa na umri wa miaka 17, wakati wa maungamo, kwa mara ya kwanza kutoka katika undani wa moyo wake, akasikia wito wa kuwa Padre!

Mang’amuzi haya ya imani, akayavalia njuga, kwa sababu aligundua ndani mwake kwamba, kwa hakika Kristo Yesu alikuwa anamsubiri, ili kumwonesha dira na mweleo mpya wa maisha! Huu ni ushuhuda alioutoa wakati wa Kesha la Sherehe ya Pentekoste, tarehe 18 Mei 2013. Kama sehemu ya kumbu kumbu angavu na endelevu ya huruma na upendo wa Mungu unaojifunua kwa waja wake, Askofu Marcello Semeraro anasema, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Septemba 2019, atafanya hija ya kichungaji, Jimbo Katoliki la Albano, ili kuwatia shime waamini ili waweze kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo thabiti katika maisha yao, licha ya changamoto kadhaa zinazoendelea kujitokeza kila kukicha!

Hija hii ya kichungaji ni sehemu pia ya kumbu kumbu endelevu, kwani ilikuwa ni tarehe 21 Septemba 2008, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Jimbo Katoliki la Albano, ili kutabaruku Altare na Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Albano. Haya ni matukio ambayo yanakumbukwa na Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuwaunga mkono, kwa kuwatembelea, changamoto na mwaliko kuanzia sasa ni kuanza kujiandaa kikamilifu hasa katika maisha ya kiroho, ili kweli hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko iweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha! Askofu Marcello Semeraro anapenda kuchukua fursa hii tangu wakati huu kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali wito na mwaliko wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Albano, kuweza kuitembelea, ili kwa pamoja hapo tarehe 21 Septemba 2019, waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu anayowakirimia waja wake katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Hii itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kwanza kabisa kukutana na kusali na Mapadre kwenye Kanisa kuu kama sehemu ya maadhimisho haya! Baada ya hapo, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Kwa sala, maombezi, tunza na ulinzi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Albano inataka kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kukumbatia utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Papa: Albano
13 July 2019, 15:42