Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameteuwa Dr. Matteo Bruni kuwa Msemaji Mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 22 Julai 2019. Papa Francisko ameteuwa Dr. Matteo Bruni kuwa Msemaji Mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 22 Julai 2019.  (ANSA)

Dr. Matteo Bruni ateuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Vatican!

Dr. Matteo Bruni ateuliwa kuwa Msemaji mkuu wa Vatican na uteuzi huu unaanza rasmi tarehe 22 Julai 2019. Alizaliwa tarehe 23 Novemba 1976 huko Winchester. Dr. Bruni ana shahada ya uzamivu katika lugha na fasihi, shahada ambayo alijipatia kutoka Chuo Kikuu cha Sapienza kilichoko mjini Roma. Dr. Bruni alianza kazi kwenye Ofisi ya Msemaji mkuu wa Vatican kunako mwezi Julai 2009.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Dr.  Matteo Bruni, kuwa Msemaji mkuu wa Vatican na uteuzi huu unaanza rasmi tarehe 22 Julai 2019. Alizaliwa tarehe 23 Novemba 1976 huko Winchester, Uingereza. Dr. Bruni ana shahada ya uzamivu katika lugha na fasihi, shahada ambayo alijipatia kutoka Chuo Kikuu cha Sapienza kilichoko mjini Roma. Dr. Bruni alianza kazi kwenye Ofisi ya Msemaji mkuu wa Vatican kunako mwezi Julai 2009. Huko alikuwa ni mratibu wa usajili wa waandishi wa habari ndani ya Vatican pamoja na kuendelea kuratibu shughuli za mawasiliano ya Ofisi ya Msemaji mkuu wa Vatican. Mwezi Desemba 2013, akateuliwa kuratibu shughuli za waandishi wa habari kwenye msafara wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, nje ya Italia. Mwanzoni mwa mwaka 2016 akateuliwa kuwa Mratibu wa Operesheni maalum za vyombo vya habari na  waandishi wa habari waliosajiliwa Vatican.

Dr. Bruni alifanya kazi kubwa ya kuratibu shughuli za mawasiliano ya jamii wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kwa miaka mingi ni mwamini mlei ambaye amekuwa akijishughulisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hususan kwenye mradi ya ushirikiano na maendeleo kwa ajili ya huduma kwa wazee. Dr. Matteo Bruni, ameoa na amebahatika kupata zawadi ya mtoto mmoja! Dr. Matteo Bruni katika mahojiano maalum na Vatican News anasema anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwona na kumteua kuwa Msemaji wake mkuu. Huu ni uzoefu ambao amejitwalia kutoka kwa wasemaji wakuu waliotangulia pamoja na ushirikiano wa dhati na wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wakati wa hija mbali mbali za Baba Mtakatifu nje ya Italia.

Ofisi ya Msemaji mkuu wa Vatican ni kitengo nyeti cha mawasiliano katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Baba Mtakatifu Francisko ameliona na kulitambua hili, ndiyo maana ameamua kumteua kiongozi anayefahamu walau kile kinachoendelea katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Vatican. Dr. Matteo Bruni anakiri kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni amekuwa akifanya kazi bega kwa bega na wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Hata katika ukimya wake, daima amejitahidi kuhakikisha kwamba, walau mambo msingi yaliyokuwa yanapewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko yanapewa uzito unaostahili, kwa kutoa habari za ukweli na sahihi. Msemaji mkuu wa Vatican ni kiongozi anayepaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kutumikia amana, utajiri na karama alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ujuzi, weledi, kanuni, sheria na taratibu za kazi zikizingatiwa.

Dr. Matteo Bruni anatambua dhamana hii mpya inayopaswa kwenda sanjari na utume wake kama baba wa familia; huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, huduma yake kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa ajili ya wazee, umekuwa ni utajiri mkubwa katika maisha yake. Anatambua kwamba, sasa anayo dhamana ya kutekeleza kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Kanisa na huduma kwa maskini. Dr. Matteo Bruni kwa namna ya pekee kabisa anapenda kumshukuru Padre Federico Lombardi, gwiji la mawasiliano ya Vatican, kiongozi aliyejisadaka usiku na mchana kwa ajili ya Baba Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake! Kwake huyu ni mfano bora wa kuigwa. Anawakumbuka na kuwashukuru Dr. Grek Burke na Paloma Garcia Ovejero, wasemaji wakuu wa Vatican ambao walijuzulu nafasi zao za kazi miezi kadhaa iliyopita.

Amesafiri hatua kwa hatua na wadau wa mawasiliano ya jamii mjini Vatican. Ni matumaini yake kwamba, wataendeleza uhusiano mwema, umoja mshikamano katika huduma ya mawasiliano. Dr. Matteo Bruni anasema, ulimwengu mamboleo unahitaji taarifa rasmi zinazozingatia: misingi ya ukweli na uwazi; ufafanuzi na maelezo ya kina ili kuwapatia walengwa habari kamili pamoja na kusoma alama za nyakati. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, wanapaswa kuwasaidia wasikilizaji, watazamaji na wasomaji kuelewa kile kinachotendeka. Maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko yanajikita katika matendo yake ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anaweza kueleweka vyema kwa maneno, vipaumbele katika maisha na utume wake pamoja na muktadha wa yale yanayotendeka. Dr. Bruni anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Dr. Alessandro Gisoti ambaye amekuwa Mseamji mkuu wa Vatican kwa muda wa miezi kadhaa. Katika kipindi chote hiki amejisadaka kwa moyo wa upendo na ukarimu, akaonesha upole na ukarimu kwa wale wote waliomwendea. Hivi ndivyo anasema Dr. Matteo Bruni anataka kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Msemaji mkuu wa Vatican.

Dr. Mattei Bruni
18 July 2019, 15:37