Tafuta

Vatican: Dhuluma, nyanyaso na vita kwa misingi ya kidini ni shambulio dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu! Vatican: Dhuluma, nyanyaso na vita kwa misingi ya kidini ni shambulio dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Dhuluma na vita kwa misingi ya kidini ni shambulio la utu wa binadamu!

Dhuluma na nyanyaso zozote zile ni shambulio dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vitendo hivi, kimaadili na kiutu, haviwezi kukubalika! Kuna haja ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ili kukuza na kudumisha udugu; majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ikumbukwe kwamb: Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini ni Wakristo; kwani kuna watu ambao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Jumuiya ya Kimataifa, haiwezi kuendelea kukaa kimya na kufumbia macho mauaji ya kinyama, mateso na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna idadi kubwa ya mashuhuda wanaouwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Karne hii, pengine kuliko ilivyowahi kutokea kwenye Karne zilizopita.

Damu ya Wakristo wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia. Watu wanapotea katika mazingira ya kutatanisha na hatimaye kuuwawa kinyama, Makanisa yanalipuliwa; maeneo ya kumbu kumbu za kale yanaharibiwa na watu wanauwawa kutokana na chuki za kidini. Hapa, inaonekana kana kwamba, Wakristo ndio walengwa wakuu wa mauaji, nyanyaso na dhuluma mbali mbali, ingawa hata waamini wa makundi madogo madogo ya kidini nao pia wanadhulumiwa kama inavyojionesha huko Iraq. Mshikamano na majadiliano ya kiekumene utawawezesha Wakristo kushirikishana tunu msingi za maisha na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa. Mashuhuda wa imani wanapoteseka na kunyanyasika, waamini wengine pia wanateseka na kunyanyasika pamoja nao! Kifo dini ni sehemu ya vinasaba, maisha na utume wa Kanisa tangu mwanzo kabisa, na daima mashuhuda wa imani wataendelea kuibuka ndani ya Kanisa kila kukicha.

Waamini watambue kwamba, Yesu Kristo Mwana wa Mungu ameonesha huruma na upendo wake kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, pale Kristo Yesu alipoyamimina maisha yake ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ushuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, kwa njia hii Wakristo kwa namna ya pekee wanafanana na Kristo.  Kifodini ni zawadi ya imani ambayo inawaambata waamini wote, lakini ni wachache tu wanaoweza kuipokea zawadi hii kwa imani na matumaini kwa kuonesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, mbele ya watesi wao pasi na mashaka wala woga wowote! Njia ya Msalaba ni sehemu ya Kanisa, lakini Wakristo pia wanayo haki ya kuheshimiwa na kuhakikishiwa uhuru wa kuabudu ambao ni nguzo ya haki msingi za binadamu. 

Ukosefu wa haki msingi za binadamu ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Umefika wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu pamoja na kupinga misimamo mikali ya kidini na kiimani inayosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini ni haki ya kila mwananchi na wala haupaswi kuwa ni upendeleo kwa watu wachache tu ndani ya jamii. Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu Msaidizi wa mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, hivi karibuni amezindua Jarida jipya kuhusu madhulumu ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia linalojulikana kama “Persecution of Christians Review”.

Katika hotuba yake elekezi, amesema kwamba, dhuluma na nyanyaso zozote zile ni shambulio dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vitendo hivi, kimaadili na kiutu, haviwezi kukubalika hata kidogo. Kuna haja ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kukuza na kuendeleza udugu wa kibinadamu; majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, lakini waamini wakumbuke daima kwamba, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Uzinduzi wa Jarida Jipya la “Persecution of Christians Review” umefanyikia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Bartolemeo, Mtume na shuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa hili liko Jimbo kuu la Roma. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya kigaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani; jambo ambalo kwa kiasi kikubwa halijapewa uzito unaostahili kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Lakini kwa Vatican, dhuluma, nyanyaso na misimo mikali ya kidini na kiimani pamoja na madhara yake katika maisha ya watu ni jambo linalopewa kipaumbele cha pekee kabisa kwa sababu linagusa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni haki ya kimataifa kwamba, Serikali mbali mbali ziwe mstari wa kwanza katika kuwalinda na kuwatetea raia pamoja na mali zao. Viongozi wa kidini wao wanayo dhamana ya kuchochea na kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha: haki, amani, umoja na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali. Hati ya Udugu wa Kibinadamu na Amani Duniani, iliyotiwa mkwaju mwezi Februari 2019 ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Hati inawataka waamini kujikita katika kutenda mema; kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi.

Waamini wawe na ujasiri wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Washirikiane katika mambo ya kiuchumi kwa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo nchini Miari wameonesha dira na mwongozo wa hija ya: haki, amani na upatanisho miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. Hii ni dhamana inayowafumbata na kuwaunganisha watu wote wenye mapenzi mema, daima wakijitahidi kuongozwa na dhamiri nyoofu pamoja na kuwa na tafsiri sahihi ya Vitabu vitakatifu vya dini zao. Huu ni mwaliko wa kutenganisha dini na serikali, ili kuwahudumia wananchi kwa ukamilifu zaidi Monsinyo Antoine Camilleri anaendelea kufafanua kwamba, lengo msingi ni kujenga mazingira yatakayowawezesha watu kuishi katika ulimwengu unaosimikwa katika haki, upendo na mshikamano.

Huu ni mwaliko wa kuondokana na kufuru ya kutumia jina la Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao binafsi, sababu za kuanzisha vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuimarisha madaraja ya amani kati ya watu wa Mataifa; kizazi cha sasa na kile kijacho! Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayokita mizizi yake katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kidini unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu.

Lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka hata katika nchi zile ambazo zinadai kwamba, zinafuata demokrasia, hali inayoonesha kinzani katika uelewa na ufahamu wa demokrasia ya kweli! Kinzani za uhuru wa kidini zinajionesha hata maisha ya kawaida, kwenye ndoa za mseto na familia katika ujumla wake. Changamoto zote hizi anasema Monsinyo Antoine Camilleri ziendelezwe katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; kwa kuzingatia: ukweli, haki, ustawi na mafao ya wengi. Dhana ya raia inakita mizizi yake katika misingi ya haki, usawa, wajibu na dhamana. Katika uelewa huu, hakuna raia wa daraja la kwanza au raia wa daraja la pili, wote ni sawa mbele ya Katiba na sheria za nchi. Misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko ni chanzo cha kinzani, ubaguzi, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kidini. Sera za kibaguzi katika baadhi ya historia zimesababisha mauaji ya kimbari.

Dhuluma Wakristo
17 July 2019, 14:43