Tafuta

Baraza la Makardinali Mashauri: Katiba ya Kitume: "Predicate evangelium" yaani "Hubirini Injili" bado inaendelea kuboreshwa na muswada wake unatarajiwa kutolewa Septemba 2019. Baraza la Makardinali Mashauri: Katiba ya Kitume: "Predicate evangelium" yaani "Hubirini Injili" bado inaendelea kuboreshwa na muswada wake unatarajiwa kutolewa Septemba 2019. 

Baraza la Makardinali Washauri: Katiba ya Kitume: Hubirini Injil

Kumbe, mabadiliko ya Sekretarieti kuu ya Vatican yanapaswa kujielekeza zaidi katika kujibu changamoto mamboleo kwa kusoma alama za nyakati. Ni matumaini ya Baraza la Makardinali washauri kwamba, muswada wa Katiba mpya unaoendelea kuboreshwa kwa kuzingatia maoni na ushauri mbali mbali, utaweza kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ifikapo mwezi Septemba 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali Washauri tayari limekwisha wasilisha Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili”. Muswada huu unaendelea kupitiwa na Mabaraza ya Kipapa, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Sinodi za Makanisa ya Mashariki, kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Makardinali washauri, kuanzia tarehe 25 Juni hadi tarehe 27 Juni 2019 wamefanya mkutano wa XXX wa Baraza la Makardinali Washauri. Mkutano huu umehudhuriwa na Makardinali washauri: Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Oscar Andrès Rodrìgues Maradiaga, Kardinali Reinhard Marx, Kardinali Seàn Patrick O’Malley, Kardinali Giuseppe Bertello pamoja na Kardinali Oswald Gracias.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Marcello Semeraro, Katibu wa Baraza la Makardinali Washauri pamoja na Askofu Marco Mellino wamehudhuria pia kutokana na nyadhifa zao. Katika mkutano huu, Askofu Marco Mellino, Katibu mwambata wa Baraza la Makardinali Washauri amewasilisha mapendekezo yaliyotolewa kutoka sehemu mbali mbali za dunia; tathmini ya kina kuhusu muswada wa Katiba mpya ya Kitume pamoja na masuala msingi yanayopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina kabla ya kuchapishwa kwa Katiba hii ya Kitume. Mapendekezo yaliyokwisha kufika kwenye Baraza la Makardinali ni yale yaliyotolewa na Mabaraza ya Kipapa na Vyuo Vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma, bado Baraza linaendelea kupokea maoni kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia!

Haya ni Mabaraza ambayo hayakuzingatia muda uliokuwa umewekwa rasmi kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo yao. Katika mkutano huu, Monsinyo Pio Vito Pinto, Dekano wa “Rota Romana” yaani Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa amedadavua kuhusu dhamana, wajibu na utume wa Mabaraza ya Kipapa mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za maisha na utume wa Kanisa. Mkutano ujao wa thelathini na moja wa Baraza la Makardinali Washauri utafanyika kati ya tarehe 17 hadi 19 Septemba 2019. Askofu Marcello Semeraro amebainisha mambo msingi yaliyomo kwenye Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili”. Jambo la msingi zaidi ni ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza kwa makini, changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi tangu mwaka 2013, Baraza la Makardinali Washauri lilipoundwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Lengo ni kuendeleza dhana ya “Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”, jambo linalopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu anaendelea kukazia wongofu wa kichungaji unaobanishwa kwenye Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” kama dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, hiki ni kiini cha Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili”.

Dhana na utume wa kimisionari ndani ya Kanisa ni muhimu kwa kusoma pia alama za nyakati kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, mabadiliko ya Sekretarieti kuu ya Vatican yanapaswa kujielekeza zaidi katika kujibu changamoto mamboleo kwa kusoma alama za nyakati. Ni matumaini ya Baraza la Makardinali washauri kwamba, muswada wa Katiba mpya unaoendelea kuboreshwa kwa kuzingatia maoni na ushauri mbali mbali, utaweza kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ifikapo mwezi Septemba 2019.

Baraza la Makardinali Juni
01 July 2019, 15:19