Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za familia ya binadamu! Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za familia ya binadamu!  (ANSA)

Simameni kidete kulinda na kutetea haki ya familia ya binadamu!

Askofu mkuu Paglia amegusia haki msingi za familia ya binadamu; umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Lakini, kimsingi familia inapaswa kupendwa, kulindwa, kutajirishwa, kudumishwa, kuendelezwa na kusindikizwa, ili iweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake katika jamii. Mwelekeo huu ni mintarafu utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia inayokita mizizi yake katika Injili uhai anafafanua kwa kusema kwamba,  familia ni hospitali iliyoko karibu nawe na ni huduma ya kwanza yenye mvuto na mashiko. Familia ni kiini cha upendo, umoja na ukarimu. Familia ni shule ya kwanza ya imani, matumaini na mapendo kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, familia ni makazi maalum ya wazee na wagonjwa. Familia bado inaendelea kuwa ni kitovu na chemchemi ya Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Ni wajibu wa wanafamilia kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Hii ni Familia mintarafu mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji na kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, Mafundisho tanzu ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema. Familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia! Familia ina tunu na changamoto zake, kwani kuna wakati wanandoa wanarushiana sahani utadhani kana kwamba, ni mbayuwayu wanaruka kutafuta chakula, lakini pia ni shule ya msamaha, upendo, haki, amani na utulivu wa ndani!

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha na Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II, hivi karibuni akiwa mjini Brescia, Italia, amechangia kwa kina na mapana kuhusu haki msingi za familia ya binadamu kwa kujikita katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii. Askofu mkuu Paglia amegusia haki msingi za familia ya binadamu; umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Lakini, kimsingi familia inapaswa kupendwa, kulindwa, kutajirishwa, kudumishwa, kuendelezwa na kusindikizwa, ili iweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake katika jamii. Mwelekeo huu pia ndio unaopaswa kutolewa mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia kunatishia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya ndoa ambazo zimevunjika au zimedhohofu kiasi cha kushindwa kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya. Watu wengi wanapenda kufurahia tu maisha ya ndoa na familia, bila kujizatiti kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na kwa jamii katika ujumla wake.

Matokeo yake ni upendo kwa Mungu na jirani unaendelea kupungua kila kukicha! Umefika wakati wa kuanza kuzungumzia na kujadili kuhusu haki msingi za familia ya binadamu, kwa sasa na kwa siku za usoni. Huu ni mwaliko wa kung’amua, kukuza na kudumisha upendo ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Upendo huu unapaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika medani mbali mbali za maisha. Dhana ya upendo inayofundishwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa inaweza kuwasaidia walimwengu kukuza na kudumisha mshikamano na mafungamano ya kijamii. Huu ndio ule upendo uliotangazwa na kushuhidiwa na Kristo Yesu; upendo usiotafuta mambo yake yenyewe.

Huu ni upendo unaokamilishana kwa kutakiana mema katika maisha. Upendo kwa Mungu na jirani anasema Askofu mkuu Vincenzo Paglia ni ule unaomsukuma mtu kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zake. Upendo wa kweli uwawezeshe waamini na watu wenye mapenzi mema kuumwilisha kwa njia ya huduma kwa watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali katika maisha; watu wanaopaswa, kuhudumiwa, kusaidiwa na kupendwa kwa dhati!

Askofu Mkuu Paglia
13 July 2019, 15:18