Vatican News
Askofu Mkuu Protase Rugambwa: Jimbo kuu la Mbeya ni Jibu la kiu ya huduma za shughuli za kichungaji kwa watu wa Mungu katika eneo hili! Umoja na ushirikiano ni muhimu sana! Askofu Mkuu Protase Rugambwa: Jimbo kuu la Mbeya ni Jibu la kiu ya huduma za shughuli za kichungaji kwa watu wa Mungu katika eneo hili! Umoja na ushirikiano ni muhimu sana!  (ANSA)

Askofu mkuu Protase Rugambwa; Jimbo kuu la Mbeya! Jibu la kiu ya kichungaji!

Uamuzi wa Baba Mtakatifu kuunda Jimbo jipya na hatimaye, kumteua Askofu mkuu Gervas Nyaisonga ni kwa kusoma alama za nyakati na kutaka kujibu kiu ya watu wa Mungu kwa ajili ya mahitaji ya huduma ya shughuli za kichungaji. Askofu mkuu Protase Rugambwa, anaombea jitihada hizi, ili ziendelee kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani; ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume amekazia mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Maaskofu wakuu wapya 31 kati yao, walikuwepo pia Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza pamoja na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anasema, kuundwa kwa Jimbo kuu la Mbeya ni dalili za kukua na kukomaa kwa Kanisa la Tanzania. Changamoto ni kuhakikisha kwamba, kila mwamini anachangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania, kwa kutoa ushirikiano na mshikamano kwa Maaskofu wakuu wapya! Kabla ya Baba Mtakatifu Francisko kuunda Jimbo kuu la Mbeya; Tanzania ilikuwa na Majimbo makuu sita yaani: Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Jimbo kuu la Dodoma, Jimbo kuu la Arusha, Jimbo kuu la Tabora, Jimbo kuu la Mwanza na hatimaye, Jimbo kuu la Songea.

Uamuzi wa Baba Mtakatifu kuunda Jimbo jipya na hatimaye, kumteua Askofu mkuu Gervas Nyaisonga ni kwa kusoma alama za nyakati na kutaka kujibu kiu ya watu wa Mungu kwa ajili ya mahitaji ya huduma ya shughuli za kichungaji. Askofu mkuu Protase Rugambwa, anaombea jitihada hizi, ili ziendelee kuzaa matunda ya katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ndani na nje ya Tanzania. Askofu mkuu Rugambwa, ameyasema haya, Jumamosi, tarehe 29 Juni 2019 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, wakati wa hafla ya kuwapongeza Maaskofu wakuu wapya kutoka Tanzania, kama kielelezo cha umoja na mshikamano kutoka kwenye Umoja wa wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma na wale wanaoishi mjini Roma.

Askofu mkuu Protase Rugambwa amewaombea Maaskofu wakuu wapya ili waweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao kwa kuzingatia: sheria za Kanisa, kanuni na taratibu zinazoongoza na kuratibu shughuli na utume wa Maaskofu wakuu. Mafanikio katika utume wa Maaskofu wakuu ni matunda ya ushirikiano, umoja na mshikamano wa familia nzima ya watu wa Mungu katika majimbo husika. Askofu mkuu Protase Rugambwa, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania. Amewashukuru watanzania wanaoishi na kusoma Roma kwa kujisadaka ili kufanikisha hafla hii kwa heshima ya Maaskofu wakuu wapya.

Watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma, wamewaomba pia Maaskofu wakuu wapya kuwasindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wao mjini Roma na Italia katika ujumla wake, ili kwamba, kwa njia ya mikono ya watanzania, utukufu wa Mungu uweze kuonekana na waendelee kuwa ni mabalozi na wawakilishi wema! Askofu mkuu Protase Rugambwa amekiri kwamba, kwa hakika nyumbani kumenoga! Watanzania wengi kwa sasa wanafunga funga vilago kurudi nyumbani baada ya masomo na wengine kwa ajili ya likizo ya kipindi cha kiangazi.

Askofu mkuu Rugambwa
02 July 2019, 15:54