Vatican News
Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen asema, watu wana kiu ya kusikiliza Neno la Mungu, kumbe kipaumbele cha kwanza ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen asema, watu wana kiu ya kusikiliza Neno la Mungu, kumbe kipaumbele cha kwanza ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. 

Askofu mkuu Hurbetus Van Megen: Kipaumbele cha kwanza ni uinjilishaji Kenya

Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini, hivi karibuni ameyataka Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa nchini Kenya kutambua kwamba, mwanadamu ana kiu ya kutaka kusikia Neno la Mungu kwani mchakato wa Uinjilishaji ni kati ya vipaumbele vya Kanisa hadi wakati huu. Uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2017 na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu likaanza utekelezaji wa maadhimisho yake yanayoongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linataka kuendeleza utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda muafaka wa kuzama zaidi katika maisha ya sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji! Kila Mkristo anawajibika barabara kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, wito ambao unabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kumbe, kwa njia ya neema ya Sakramenti ya Ubatizo, wabatizwa wanageuzwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa maisha na utume wa Kanisa, na hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 93 ya Kimisionari Ulimwenguni anakazia umuhimu wa Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa kutambua kwamba, asili ya Kanisa ni utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kila mwamini anao mchango wake makini kwani haya ni matunda ya upendo wa Mungu. Kama vile Kristo Yesu alivyotumwa na Baba yake wa Mbinguni, ndiyo dhamana aliyolikabidhi Kanisa kuendeleza utume huu kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayokita mizizi yake kwa toba na wongofu wa ndani.

Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anaendelea kuhimiza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kuamsha uzuri na utakatifu wa Injili ya Kristo kwa watu wanaosinzia kiimani na kimaadili bila kuwasahau watu waliotopea katika dhambi. Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini, hivi karibuni ameyataka Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa nchini Kenya kutambua kwamba, mwanadamu ana kiu ya kutaka kusikia Neno la Mungu kwani mchakato wa Uinjilishaji ni kati ya vipaumbele vya Kanisa hadi wakati huu. Hizi ni juhudi ambazo zinapaswa kujikita katika furaha, ukarimu, ukweli, upendo na ushuhuda wenye mashiko. Uinjilishaji ni chachu ya mageuzi katika maisha, utume pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa sanjari na mchakato wa maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili.

Miundo mbinu ya uinjilishaji ni muhimu, lakini kipaumbele cha kwanza ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Ari na moyo wa kimisionari ndani ya Kanisa vinapaswa kukuzwa na kudumishwa zaidi. Inasikitisha kuona kwamba, ndani ya Kanisa kuna baadhi ya waamini wenye mawazo na mwono potofu kuhusu ari na mwamko wa kimisionari kwa kudhani kwamba, huu ni utume unaopaswa kutekelezwa na Mashirika ya kitawa na kazi za kitume peke yake, kumbe, huu ni utume wa wakristo wote katika ujumla wao. Mapadre wa majimbo na Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume wanapaswa kushirikiana na kusaidiana ili kusongesha mbele umisionari wa Kanisa. Dhanama hii iwashirikishe pia waamini walei, ili wasaidie mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni kwa njia ya ushuhuda wa Injili, toba na wongofu wa ndani, utaweza kusaidia watu kuheshimiana na kushikamana kama ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi za kiimani, kitamaduni na kikabila! Hakuna utamaduni wenye hadhi ya juu kuliko tamaduni nyingine zote!

Kenya: Uinjilishaji.

 

 

31 July 2019, 14:37