Tafuta

Vatican News
Kongamano la Kimataifa la Siku za Machapisho ya Kikatoliki, changamoto ni kukuza na kudumisha umoja katika utofauti wa njia za mawasiliano ya kijamii, ili kuifikia hadhira kubwa zaidi. Kongamano la Kimataifa la Siku za Machapisho ya Kikatoliki, changamoto ni kukuza na kudumisha umoja katika utofauti wa njia za mawasiliano ya kijamii, ili kuifikia hadhira kubwa zaidi. 

Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki 2019: Umoja!

Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki zinazoongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali”. Huu ni muda muafaka wa kushirikishana uzoefu, mang’amuzi pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kadiri ya maeneo ya kijiografia mintarafu teknolojia ya kidigitali. Waandaaji: Baraza la Mawasiliano na CEI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 26 Juni hadi 29 Juni 2019, Kanisa linaadhimisha Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki zinazoongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali”. Huu ni muda muafaka wa kushirikishana uzoefu, mang’amuzi pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kadiri ya maeneo ya kijiografia mintarafu teknolojia ya kidigitali. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Kongamano hili linahudhuria na wadau kutoka katika viwanda 50 vya uchapaji vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Kati ya wawezeshaji wakuu ni pamoja na: Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Fra Giulio Cesareo, O.F.M. Conv. Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, LEV. Dr. Paolo Ruffini katika hotuba yake elekezi amesema, huu ni mwanzo mpya wa viwanda vya uchapaji vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kuanza mchakato wa kutembea kwa pamoja. Umoja na mshikamano katika uzalishaji na utoaji wa huduma ni muhimu sana ili kukabiliana na changamoto mamboleo za kiekolojia na kiutu, zinazoendelea kumwandama mwanadamu wa nyakati hizi, kiasi hata cha kugusa machapisho ya Kanisa.

Hapa kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja katika utofauti unaojidhihirisha katika vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii, ili hatimaye, kujenga mtandao wenye nguvu zaidi, utakaoweza kukabiliana uso kwa uso na changamoto mamboleo. Machapisho ya Kanisa ni daraja la mawasiliano kati ya Kanisa na Ulimwengu, mwaliko kwa wahariri wakuu kuanza kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Maandiko Matakatifu na tunu msingi za Kiinjili, kwa kuwalenga watu maalum watakaoweza kusikiliza, kuona na kusoma machapisho haya. Hadhira inayokusudiwa na Kanisa la Kiulimwenu, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na waandishi mahiri na manabii wenye uwezo wa kusoma alama za nyakati, tayari kujisadaka kwa kuandika vitabu vinavyoweza kusambazwa kwa mifumo mbali mbali kiasi hata cha kuingia katika ulimwengu wa kidigitali hali ambayo itasaidia kufikia hadhira kubwa kwa wakati mmoja!

Machapisho ya Kanisa Katoliki yanalenga kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kuwajengea watu tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kiutu na kijamii. Kumbe, wahariri wa vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa wanapaswa kuhakikisha kwamba, vyombo vyao vinatumiza pia kueneza, kulinda na kutetea imani ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Kwa upande wake Padre Marko Ivan Rupnik, amewataka wahariri wakuu kuhakikisha kwamba, machapisho yao, yanasaidia kulisha na kuboresha imani, ili kuondokana na tabia ya uchoyo, ubinafsi mambo ambayo yanawatumbukizwa watu wengi kwenye utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ni wajibu wa wahariri kuhakikisha kwamba, wanasaidia kueneza: Imani ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na unyoofu wa moyo unaobubujika kutoka katika Amri za Mungu pamoja na maisha ya sala, kama kielelezo cha majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake.

Machapisho Kanisa
27 June 2019, 15:53