Maadhimisho ya Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki: Changamoto katika ulimwengu wa kidigitali! Maadhimisho ya Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki: Changamoto katika ulimwengu wa kidigitali!  Tahariri

Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki 2019: Digitali!

Fra Giulio Cesareo, anasema, wachapaji wa vitabu, majarida na magazeti ya Kanisa Katoliki, wanapaswa kusoma alama za nyakati, ili kweli waweze kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; daima: masuala ya imani, kanuni maadili na utu wema yakipewa kipaumbele cha kwanza. Wahariri na wachapaji wasiposoma alama za nyakati, wako hatarini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 26 Juni hadi 29 Juni 2019, Kanisa Katoliki limeadhimisha Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki zinazoongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali”. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Wadau kutoka katika viwanda 50 vya uchapaji vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia wanashiriki kikamilifu. Hadi wakati huu mkazo umekuwa ni mchakato wa ujenzi wa umoja katika tofauti, ili kuwezesha tunu msingi za kiinjili ziweze kuwafikia watu wengi zaidi kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali.

Wahariri na wachapaji wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia umuhimu na uzuri wa machapisho ya Kikatoliki kama sehemu ya mchakato wa maboresho na upyaisho wa maisha na imani, kanuni maadili na utu wema; ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Fra Giulio Cesareo, O.F.M. Conv. Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, LEV., ambaye ni kati ya wawezeshaji wakuu anasema, tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mama Kanisa ameendelea kupyaisha maisha na utume wake, ili kuwawezesha watoto wa Kanisa kuwa  ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia, ili kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati.

Hii ni sehemu ya uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kuna haja ya kuanzisha msingi wa umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya wahariri na wachapaji wa machapisho ya Kikatoliki, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi pamoja na matumizi ya teknolojia ya kidigitali. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa wahariri na wachapachaji kuwa na mwelekeo mpya zaidi utakaowawezesha kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara kwa kuendelea kusoma alama za nyakati! Fra Giulio Cesareo, anasema, wachapaji wa vitabu, majarida na magazeti ya Kanisa Katoliki, wanapaswa kusoma alama za nyakati, ili kweli waweze kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; daima: masuala ya imani, kanuni maadili na utu wema yakipewa kipaumbele cha kwanza.

Lengo ni kuwawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukutana na Kristo Mfufuka katika machapisho haya, ili waweze kuboresha na kupyaisha maisha na utume wao wa kuyatakatifuza malimwengu. Wakati umefika wa kuanza kufikiri namna ya kutumia mitandao mbali mbaliya kijamii. Vinginevyo, maduka ya vitabu na machapisho ya Kikatoliki yataendelea kufungwa kila kukicha kwa sababu tu, wafanyakazi wake hawakuweza kusoma alama za nyakati. Huu ni mwaliko kwa wadau wa machapisho ya Kanisa Katoliki kuhakikisha kwamba, wanatoa nafasi kwa Kanisa kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Soko la machapisho ya Kikatoliki linakabiliwa na changamoto nyingi zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki imekuwa ni nafasi kwa wadau mbali mbali kushiriki katika maonesho ya machapisho kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mambo ya kuzingatia ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sifa, utukufu wa Mwenyezi Mungu; Umoja, maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo pamoja na kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Wahariri na wachapishaji wawe ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na tunu msingi za kiinjili, kitamaduni, kiutu na kijamii.

Machapisho Katoliki

 

29 June 2019, 17:35