Kardinali Pietro Parolin tarehe 12 Juni 2019 amefungua mkutano wa awamu ya tatu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Pietro Parolin tarehe 12 Juni 2019 amefungua mkutano wa awamu ya tatu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia. 

Mabalozi na wawakilishi wa Vatican wanakutana mjini Vatican!

Ibada ya Misa Takatifu kwa Mabalozi wa Vatican kutoka katika nchi 103; kati yao kuna Mabalozi 98 na wengine 5 ni Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa malengo ya Baba Mtakatifu Francisko anayetaka kuimarisha umoja na mafungamano miongoni mwa wawakilishi wa Vatican duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 12 Juni 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Mabalozi na wawakilishi wa Vatican kutoka katika nchi 103; kati yao kuna Mabalozi 98 na wengine 5 ni Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa malengo ya Baba Mtakatifu Francisko anayetaka kuimarisha umoja na mafungamano miongoni mwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, kama alivyofanya kunako mwaka 2013 na mwaka 2016. Mkutano huu, utahitimishwa hapo tarehe 15 Juni 2019.

Katika mkutano huu, Mabalozi 46 waliokwisha kung’atuka kutoka kwenye nyadhifa zao, wamekaribishwa kushiriki. Huu ni muda wa kutafakari, kupembua na kushirikishana hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa bila kusahau majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Mabalozi hawa wanaendelea kukutana na kuzungumza na Mabalozi mbali mbali wanaoziwakilisha nchi pamoja na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa. Viongozi wakuu wa Mabaraza ya Kipapa, watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza nao mubashara.

Tarehe 15 Juni 2019, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican akisaidiana na Mabalozi wake kutoka sehemu mbali mbali za dunia na baadaye, watapata chakula cha mchana ambacho Baba Mtakatifu amewaandalia Mabalozi wake, ili kuweza kupata tena nafasi ya kubadilishana mawazo katika hali ya utulivu! Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko mjini Vatican amekazia umuhimu wa upendo na utii katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Sheria kuu ni Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!

Kama wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, wanahamasishwa kuheshimu, kuzingatia na kutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na katika nchi wanamoiwakilisha Vatican. Watambue kwamba, huduma yao ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; yanayotekelezwa na kumwilishwa katika diplomasia ya Vatican. Sheria inapaswa kupewa kipaumbele kama sehemu ya huduma muhimu kwa binadamu! Kardinali Parolin anakaza kusema, msingi wa Sheria na upendo unaooneshwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa kwa watu wote, lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Paulo Mtume anasema, Yeye ameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Huu ni utume kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa nguvu zake mwenyewe anaweza kuutekeleza. Mabalozi wa Vatican nao pia wanashiriki utume wa Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu wa kweli na mashuhuda amini wa Kristo Mfufuka na Kanisa lake.

Mabalozi hawa wawe ni mashuhuda wa imani, mapendo na matumaini ya watu. Mabalozi hawa katika maisha na utume wao, wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, kama kielelezo cha utume unaotekelezwa na Baba Mtakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili kama zinavyofafanuliwa kwenye Agano Jipya. Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin, amewataka Mabalozi wa Vatican kukumbukana na kuombeana; kwani kwa njia ya utume wao, wamefungwa na mnyororo wa Injili ya Kristo, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili mintarafu sheria ya upendo!

Parolin: Misa
12 June 2019, 15:36