Kardinali Pietro Parolin anasema, mkutano awamu ya tatu kati ya Papa na Mabalozi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia, umekuwa na mafanikio makubwa! Kardinali Pietro Parolin anasema, mkutano awamu ya tatu kati ya Papa na Mabalozi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia, umekuwa na mafanikio makubwa! 

Kardinali Parolin: Mshikamano na Papa Francisko katika utume!

Wanapaswa kuungana na kushikamana katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa! Kama Mabalozi na wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wako huru kuamua na kutenda katika mambo ambayo yanaonesha mashaka, lakini upendo hudumishwe katika yote! Walatini wakaweka maneno haya kwa ufupi wakisema “In necessariis unitas, in dubiis libertas, in omnibus caritas”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 12 Juni 2019 alifungua mkutano wa Mabalozi wa Vatican kutoka katika nchi 103; kati yao wamo Mabalozi 98 na wengine 5 ni Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa malengo ya Baba Mtakatifu Francisko anayetaka kuimarisha umoja na mafungamano miongoni mwa wawakilishi wa Vatican duniani! Kama wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, wanahamasishwa kuheshimu, kuzingatia na kutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na katika nchi wanamoiwakilisha Vatican.

Watambue kwamba, huduma yao ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; yanayotekelezwa na kumwilishwa katika diplomasia ya Vatican. Sheria inapaswa kupewa kipaumbele kama sehemu ya huduma muhimu kwa binadamu! Mabalozi wa Vatican pia wanashiriki utume wa Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu wa kweli, ili waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Mfufuka na Kanisa lake. Mabalozi hawa wawe ni mashuhuda wa imani, mapendo na matumaini ya watu. Mabalozi hawa katika maisha na utume wao, wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, kama kielelezo cha utume unaotekelezwa na Baba Mtakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili kama zinavyofafanuliwa kwenye Agano Jipya.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwakumbusha Kanuni 10 wanazopaswa kuzizingatia katika maisha na utume wao kama Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia! Mwongozo wa maisha na utume wa Mabalozi na wawakilishi wa Vatican unawakumbusha kwamba, wao: Ni watu wa Mungu na Kanisa wenye ari na mwamko wa kitume. Ni wapatanishi na wawakilishi wa Papa; ni watu wanaochakarika kwa ajili ya maendeleo ya watu; maisha yao yanasimikwa katika utii, sala, huduma ya upendo na unyenyekevu wa maisha, kama wafuasi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! Baba Mtakatifu, Jumamosi, tarehe 15 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Kalenga alifariki dunia, tarehe 12 Juni 2019. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu alisema, maisha yawafundishe waamini kusema buriani kama wachungaji, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo na kama ilivyokuwa kwa Yesu na wengine kama hata ilivyo kwa Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele. Viongozi wa Kanisa waanze kujiandaa kuagana na ndugu zao: wanapohamishwa kwenye maeneo ya kazi, lakini zaidi, wanapokwenda nyumbani kwa Baba katika makazi ya uzima wa milele! Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika mahojiano maalum na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican baada ya mkutano wa awamu ya tatu kati ya viongozi wakuu wa Vatican pamoja na Mabalozi na wawakilishi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia anasema, ameridhishwa sana na mkutano huu.

Kardinali Parolin anasema kwamba, Mabalozi na wawakilishi wote wanawajibika kuungana na kushikamana na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kukutana na kusalimiana na Mabalozi pamoja na wawakilishi wote wa Vatican waliohudhuria mkutano huu na hivyo kuweza kumegeana furaha ya Injili, changamoto na matatizo yanayoliandama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Ujumbe wa Baba Mtakatifu umepokelewa kwa mikono miwili, tayari kufanyiwa kazi katika maisha na utume wao kama wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu ni sehemu ya mwendelezo wa utamaduni wa Baba Mtakatifu wa kukutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi mbali mbali kila baada ya miaka mitatu.

Uzoefu huu unapata chimbuko lake mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa kunako mwaka 2013 na wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kunako mwaka 2016. Mwongozo wa maisha na utume wa Mabalozi na wawakilishi wa Vatican anasema Kardinali Pietro Parolin, kwamba, wanatambua udhaifu na mapungufu yao kama binadamu na walikuwa tayari kusikiliza ushauri na mwongozo kutoka kwa Baba Mtakatifu mwenyewe, ili kuboresha huduma ya Kanisa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, mwongozo huu umepokelewa kwa unyenyekevu na moyo mkuu kama sehemu ya maboresho ya utume wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa watu wa Mungu katika ujumla wao!

Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, kimsingi wao ni watu wa Mungu na Kanisa wenye ari na mwamko wa kitume. Ni wapatanishi na wawakilishi wa Papa; ni watu wanaochakarika kwa ajili ya maendeleo ya watu; maisha yao yanasimikwa katika utii, sala, huduma ya upendo na unyenyekevu wa maisha, kama wafuasi wa Kristo Yesu na Kanisa lake! Jambo kubwa hapa ni kukumbuka kwamba,  wanapaswa kuungana na kushikamana katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa! Kama Mabalozi na wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wako huru kuamua na kutenda katika mambo ambayo yanaonesha mashaka, lakini upendo hudumishwe katika yote! Walatini wakaweka maneno haya kwa ufupi wakisema “In necessariis unitas, in dubiis libertas, in omnibus caritas”.

Wanaweza kuzungumza kwa uhuru wote, kwani Baba Mtakatifu ni mkweli na muwazi, yuko tayari kupokea ushauri, angalisho na maoni ambayo mara nyingi anayafanyia kazi! Lakini wanapaswa kujenga na kudumisha umoja katika mambo msingi, kama sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa maisha na utume wao! Umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake; mambo yanayotafsiriwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu alipata fursa pia ya kuzungumza faragha na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Vatican. Huu ni mkutano uliojikita katika ukweli na uwazi; ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu katika huduma. Mabalozi wameuliza maswali na Baba Mtakatifu kama kawaida ameyajibu kwa ufasaha kiasi kwamba, wengi wao wameridhishwa na utamaduni wa kukutana kila baada ya miaka mitatu!

Kard. Parolin: Mabalozi
19 June 2019, 11:29