Tafuta

Vatican News
Hotuba za Baba Mtakatifu Francisko nchini Romania, tarehe 31 Mei 2019 zimeonesha dira na mwongozo wa kufuata kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Barani Ulaya! Hotuba za Baba Mtakatifu Francisko nchini Romania, tarehe 31 Mei 2019 zimeonesha dira na mwongozo wa kufuata kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Barani Ulaya!  (AFP or licensors) Tahariri

TAHARIRI: Dira na Mwongozo wa Jumuiya ya Ulaya na watu wake!

Si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko kunyooshea kidole “madonda” yanayoutesa ulimwengu mamboleo; mfumo wa uchumi unaotoa kipaumbele kwa faida kubwa yaani “fedha” kiasi cha kuabudiwa kama miungu wadogo, badala ya kutoa umuhimu wa pekee kwa: utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi wanaoendelea kuchakarika katika uzalishaji na huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hotuba zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa siku yake ya kwanza, katika hija yake nchini Romania, inayoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ametoa dira na mwongozo wa Bara la Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake, kwa siku za usoni. Katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia, Baba Mtakatifu amesema, Romania inapaswa kujielekeza katika ujenzi wa jamii shirikishi kwa kutoa fursa kwa kila mwananchi kutumia vyema karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani ni kwa njia ya kazi inayofanywa kwa uhuru, kwa ubunifu, kwa kushirikiana na kwa kusaidiana na wengine, ndivyo mwanadamu hudhihirisha na kuendeleza heshima na utu wao.

Hii ni Jamii ambamo maskini wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama ndugu, kwa kushirikishwa katika ujenzi wa nchi yao, kielelezo makini cha jamii inayoendelea, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maendeleo ya kweli yanafumbatwa katika mshikamano na upendo unaounganisha nguvu, sera na mikakati kwa ajili ya mafao ya wengi kwa kutumia vyema rasilimali iliyopo! Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika tahariri yake anakaza kusema, si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko kunyooshea kidole “madonda” yanayoutesa ulimwengu mamboleo; mfumo wa uchumi unaotoa kipaumbele kwa faida kubwa yaani “fedha” kiasi cha kuabudiwa kama miungu wadogo, badala ya kutoa umuhimu wa pekee kwa: utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi wanaoendelea kuchakarika katika uzalishaji na huduma.

Haya ni maneno machungu yanayohitaji ujasiri na utashi wa kisiasa kuweza kukubalika na watu wenye nguvu kiuchumi. Hili ni onyo kwa Bara la Ulaya ambalo kwa sasa: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaendelea kusiginwa kila kukicha! Huu ni wakati kwa Bara la Ulaya kuwa karibu zaidi na wananchi wake. Huu ndio mwelekeo ambao pia umeoneshwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa la kiorthodox nchini Romania, kwa kuwataka kumsikiliza Mwenyezi Mungu kwa pamoja kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo zinazojitokeza katika masuala ya kijamii na kitamaduni; katika maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na ustawi wa kiuchumi, mambo ambayo yameleta faida kubwa kwa watu, lakini wengi wao wametengwa na mafanikio haya.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, utandawazi umepelekea kung’oa tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili na kwamba, maisha ya pamoja yanaonekana kukosa mashiko na kwamba, kumekuwepo na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Matokeo yake ni watu kushikwa na woga, chuki, uhasama na hali ya kutaka kujitafuta binafsi. Kuna haja ya kuondokana na kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza watu kwenye utamaduni wa chuki na uhasama; ubinafsi na uchoyo, kama ilivyokuwa wakati wa madhulumu na ukanimungu.

Baba Mtakatifu kama muhtasari wa Sala ya Bwana, Sala ya Baba Yetu, amemwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia waamini mkate wa kumbu kumbu, neema itakayosaidia kuimarisha mizizi ya utambulisho wao kama Wakristo, ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuthamini asili na utambulisho wao. Kuna umuhimu wa kugundua tena mizizi, tunu msingi na ndoto ya waasisi wa Jumuiya ya Ulaya ili kuondokana na kishawishi cha ujenzi wa kuta za utengano. Tunu hizi ziwe nyenzo ya kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano mapya ya kijamii, ili kuimarisha ukarimu na ushirikishwaji mkamilifu!

Tahariri: Tornielli
01 June 2019, 12:02