Mtandao wa Utume wa Saka Kimataifa unaadhimisha Jubilei ya Miaka 175 ya uhai na utume wake: Yaliyojiri katika kipindi cha miaka hii yote! Mshikamano katika utume wa sala! Mtandao wa Utume wa Saka Kimataifa unaadhimisha Jubilei ya Miaka 175 ya uhai na utume wake: Yaliyojiri katika kipindi cha miaka hii yote! Mshikamano katika utume wa sala! 

Miaka 175 ya Utume wa Sala Kimataifa: Upyaisho wa maisha!

Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa unaadhimisha Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwake pia unakijumuisha Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi Takatifu, EYM. Utume wa Sala Kimataifa ulianzishwa kunako tarehe 3 Desemba 1844 huko Paris, Ufaransa na Padre Francesco Saverio Gaufrelet, SJ. Imegota miaka 10 ya mabadiliko makubwa na miaka 5 ya upyaisho wa utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya kijamii, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, unaoendelea kusoma alama za nyakati, ili ujumbe na nia za Baba Mtakatifu kila mwezi ziweze kuwafikia watu wengi zaidi mahali walipo! Utume wa Sala Kimataifa kwa sasa unaendelea kuchanja mbuga kwa kutumia mitandao ya kijamii, ili kuweza kuwashirikisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema katika sala, huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanaliwezesha hata Kanisa kuweza kuvuka mipaka ya kijiografia na kuwa karibu zaidi na watu kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Watu wanavutwa zaidi na ushuhuda ndiyo maana hatua ya kwanza imekuwa ni kuweka ujumbe wa Baba Mtakatifu katika video, ili watu waone na kushiriki pamoja naye katika sala, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa duniani. Lengo ni kukuza mahusiano kati ya mwamini na Baba Mtakatifu katika sala inayomwilishwa kwenye matendo! Kuanzia  Ijumaa, tarehe 28 Juni 2019, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, hadi Jumamosi tarehe 29 Juni 2019 Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, miamba ya imani, Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa unaadhimisha Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwake. Itakumbukwa kwamba, Utume wa Sala Duniani unakijumuisha pia Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi Takatifu, EYM. Utume wa Sala Kimataifa ulianzishwa kunako tarehe 3 Desemba 1844 huko Paris, Ufaransa na Padre Francesco Saverio Gaufrelet, SJ.

Imegota miaka 10 tangu Utume wa Sala Kimataifa ulipoanza kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wake na miaka 5 tangu dira na mwelekeo mpya wa utume wa Sala Kimataifa ulipopitishwa na kuidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko.  Kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato huu wa upyaisho wa maisha ya Utume wa Sala Duniani, hapo tarehe 27 Machi 2018, Baba Mtakatifu akaidhinisha Katiba Mpya ya Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, kama sehemu ya utume wa Kipapa na makao yake makuu yakahamishiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu akamteuwa Mheshimiwa Padre Frederic Fornos, SJ., kuwa Mkurugenzi wake mkuu. Kumbe, hiki ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake; muda wa kuomba toba na wongofu wa ndani kwa mapungufu yaliyojitokeza, tayari kuomba neema na baraka ya kuyakumbatia ya mbeleni kwa imani na matumaini makubwa!

Maadhimisho haya yanawashirikisha wajumbe zaidi ya 6000 kutoka katika nchi 52. Padre Frederic Fornos, katika hotuba yake kwa ajili ya kumkaribisha Baba Mtakatifu ili aweze kuzungumza na wajumbe hawa amesema, kimsingi waamini wanaounda Mtandao wa Sala Kimataifa ni watu wa kawaida kabisa na wala hawana nafasi kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa njia ya ukarimu, ushuhuda wa imani, sadaka na maisha ya sala, wanalisaidia Kanisa kusonga mbele na maisha pamoja na utume wake. Hawa ni wale wanaokimbilia huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu; neema ya kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kudumu katika imani, matumaini na mapendo, licha ya vikwazo na changamoto mbali mbali anazopambana nazo katika maisha na utume wake!

Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa pamoja na mambo mengine unajihusisha kikamilifu katika kuandaa picha za video zinazosindikiza nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi (www.ilvideodelpapa.org) pamoja na Jukwaa la Sala kwa ajili ya utume wa Kanisa (www.clicktopray.org).

Utume wa Sala: Historia
28 June 2019, 18:21