Kardinali Parolin: Likizo ni muda muafaka wa kuimarisha diplomasia ya maisha ya kiroho kwa kufanya tafakari ya kina, tayari kupyaisha maisha na utume wao kwa siku za usoni! Kardinali Parolin: Likizo ni muda muafaka wa kuimarisha diplomasia ya maisha ya kiroho kwa kufanya tafakari ya kina, tayari kupyaisha maisha na utume wao kwa siku za usoni! 

Kardinali Parolin: Likizo: Imarisheni Diplomasia ya kiroho!

Kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, huu ni wakati wa kuimarisha diplomasia ya maisha ya kiroho, kwa kuchunguza dhamiri katika ukweli, uwazi na utulivu wa ndani, ili kuweza kufanya tathmini ya kina kuhusu maisha, maamuzi na matendo waliyotekeleza katika kipindi cha mwaka 2018-2019, tayari kujipyaisha, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni aliandaa dhifa kwa ajili ya Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, kama alama ya kumshukuru Mungu kwa kufunga mwaka wa kazi, tayari kuanza mapumziko ya kiangazi, fursa maalum ya kujipatia nguvu ya kuweza kusonga mbele na utume wao mjiini Vatican. Kardinali Parolin, amefafanua kwamba, likizo ni muda wa mapumziko, unaomwezesha mtu kubadili mfumo wa kazi na mtindo wa maisha. Kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, huu ni wakati wa kuimarisha diplomasia ya maisha ya kiroho, kwa kuchunguza dhamiri katika ukweli, uwazi na utulivu wa ndani, ili kuweza kufanya tathmini ya kina kuhusu maisha, maamuzi na matendo waliyotekeleza katika kipindi cha mwaka 2018-2019, tayari kujipyaisha, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Ni fursa ya kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu ile diplomasia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Dhifa hii imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Vatican. Kardinali Parolin, amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi kutoka balozi mbali mbali kwa ushirikiano wao mwema; wakati wa raha, shida na machungu ya maisha na hata wakati mwingine, kwa kushirikishana Injili ya matumaini. Kwa hakika, baada ya pilika pilika za mwaka mzima, sasa wanayo haki ya kujipatia mapumziko, ili kuweza kujichotea nguvu ya maisha ya kiroho na kidiplomasia. Kardinali Parolin, ametumia fursa hii, kuwakaribisha Mabalozi wote waliowasilisha hati zao za utambulisho katika kipindi cha Mwaka 2018-2019 na kuwasihi wajisikie kuwa ni sehemu ya familia ambamo tofauti za mawazo, ustawi na mafao zinashikamananishwa pamoja kwa ajili ya utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Parolin ametumia fursa hii pia kutoa salam zake za rambi rambi kwa wale ambao katika kipindi cha mwaka mzima, wameondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao, ili wote hawa waweze kuonja: huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka na kuwaombea wananchi ambao wameathirika kutokana na majanga asilia. Katika maisha na utume wao kama wanadiplomasia ndani mwao wanaonja na kukuza ule udugu wa kibinadamu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, unaowahamasisha kushikamana kwa dhati, ili kutekeleza majukumu yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Ujenzi wa udugu wa kibinadamu unahitaji sadaka na majitoleo yao, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mwanga angavu wa diplomasia uendelee kuimarisha udugu wa kibinadamu sehemu mbali mbali za dunia. Mwishoni mwa hotuba yake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewashukuru na kuwapongeza wanadiplomasia na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano mzuri na Vatican. Amewaomba kufikisha salam na matashi mema ya Vatican kwa viongozi wa Serikali na Mashirika yao ya Kimataifa!

Ujumbe kwa Mabalozi

 

25 June 2019, 15:12