Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anatembelea Jimbo kuu la Camerino-San Severino Marche: Alama ya Mshikamano wa kidugu! Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anatembelea Jimbo kuu la Camerino-San Severino Marche: Alama ya Mshikamano wa kidugu! 

Hija ya Papa Francisko Camerino: Ratiba elekezi!

Papa Francisko, tarehe 16 Juni 2019 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji kama kielelezo cha mshikamano wa upendo wa kidugu, kwa kutembelea Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino, nchini Italia. Haya ni maeneo yaliyoathirika sana kwa matetemeko ya ardhi yaliyojitokeza kati ya mwaka 2016-2017, sehemu kubwa ya Italia, ilipopigishwa magoti kutokana na athari za majanga asilia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linasadiki na kufundisha kwamba, Mungu Baba ni Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ndiye anayelitakatifuza Kanisa. Imani ya Kanisa inaungama kwamba, kuna Mungu mmoja tu, kwa asili (natura) kwa uwamo (subustantia), na kwa uwapo (essentia). Hili ndilo Fumbo la Imani, linaloadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili tarehe 16 Juni 2019. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 16 Juni 2019 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji kama kielelezo cha mshikamano wa upendo wa kidugu, kwa kutembelea Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino lililoko mkoa wa Marche, nchini Italia.

Haya ni maeneo yaliyoathirika sana kwa matetemeko ya ardhi yaliyojitokeza kati ya mwaka 2016-2017, sehemu kubwa ya Italia, ilipopigishwa magoti kutokana na athari za majanga asilia! Takwimu zinaonesha kwamba, watu 283 walifariki dunia na zaidi ya watu 2, 500 waliathirika vibaya sana kutokana na matetemeko yalijitokeza katika maeneo haya. Licha ya watu kupoteza maisha, lakini pia miundo mbinu ya majengo na barabara ziliharibiwa sana! Baba Mtakatifu atakapowasili Jimboni humo, atapokelewa na Askofu mkuu Francesco Massara wa Jimbo Kuu la Camerino-Sanseverino kwa niaba ya viongozi wa Kanisa na Dr.  Luca Cerscioli, Rais wa Mkoa wa Marche kwa niaba ya viongozi wa Serikali.

Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea majengo ya makazi ya watu kwa muda na kusalimiana na wanafamilia wanaoishi humo. Atatembelea Kanisa kuu na kukutana na Mameya wanaongoza miji inayounda Jimbo hili. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, baadaye, atapata chakula cha mchana na wakleri wa Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino na baadaye, majira ya alasiri, atarejea tena mjini Vatican kuendelea na shughuli zake za kitume! Itakumbukwa kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu.

Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika katika  usawa, ustawi na mafao ya watu wote duniani.

Papa: Camerino

 

 

14 June 2019, 15:52