Tafuta

Baraza ka Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo cha CHARIS kutaribu huduma za Wakarismatiki Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia Baraza ka Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo cha CHARIS kutaribu huduma za Wakarismatiki Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia 

Kitengo cha CHARIS: Huduma ya Wakarismatiki: Mwanzo Mpya!

CHARIS ni kitengo kinachosimamia na kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki. CHARIS inazinduliwa rasmi wakati wa Sherehe ya Pentekoste, 9 Juni 2019. Katika mukatadha huu, Chama cha Udugu wa Kikatoliki na Huduma ya Uhamsho wa Kikatoliki Kimataifa, (ICCRS) vitakoma kutoa huduma. Mwanzo mpya wa Wakarismatiki Wakatoliki. Kazi na zawadi ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” kinachosimamia na kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki. Kitengo hiki kinaanza utekelezaji wa huduma yake wakati wa Sherehe ya Pentekoste, 9 Juni 2019. Katika mukatadha huu, Chama cha Udugu wa Kikatoliki, (The Catholic Frarenity) na Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki Kimataifa, (ICCRS) vitakoma kutoa huduma na Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu unakuwa ni mwanzo mpya wa Chama Cha Wakarismatiki Wakatoliki, kielelezo cha neema na zawadi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Katika asili yake, neno “CHARIS” maana yake ni “neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu”. Kitengo cha CHARIS kilizinduliwa rasmi tarehe tarehe 8 Desemba 2018, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii pia ilikuwa ni siku ya kuzindua rasmi Katiba inayoratibu shughuli za kitengo hiki kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu!

Kitengo hiki kimeanzishwa kwa maamuzi ya Baba Mtakatifu Francisko ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika huduma inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya waamini milioni 120 wa Kanisa Katoliki ambao ni wanachama wa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki wanaoendelea kupyaisha dhamana na utume wao unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na kwa kuimarishwa na Roho Mtakatifu, zawadi ya Baba wa milele. Utume huu unamwilishwa katika vikundi vya sala; Jumuiya za Wakarismatiki pamoja na shule za uinjilishaji na hivyo kuunda mtandao wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi kitengo hiki, hakitakuwa na mamlaka juu ya Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, bali wataendelea kutekeleza dhamana na shughuli zao kama kawaida, chini ya usimamizi wa Maaskofu mahalia. Kila tawi linaweza kupata huduma na msaada wa kiufundi utakaokuwa unatolewa na CHARIS sehemu mbali mbali za dunia. Chama hiki kimeenea katika ngazi mbali mbali, kuanzia Parokiani, Kijimbo, Kitaifa na Kimataifa! Kumekuwepo na “ukakasi kwa baadhi ya Maaskofu kuwakubali na kuwapokea wanachama hawa na kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa mahalia!Lakini, Kanisa linakumbusha  kwamba, zote hizi ni zawadi za Roho Mtakatifu zinazopaswa kuratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu!

Wakristo kwa kupakwa Krisma Takatifu wanaingizwa katika maisha ya Kristo Yesu ambaye amepakwa mafuta kuwa: Kuhani, Nabii na Mfalme. Chama hiki ni chachu ya majadiliano ya kiekumene na umoja miongoni mwa Wakristo. Wanachama wake wanajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia ya maisha na utume wao, wanashiriki kikamilifu katika utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ajili ya Kanisa zima! Kuanzia tarehe 6 – 7 Juni 2019 Kitengo cha CHARIS kimeandaa mkutano mkubwa unaowajumuisha viongozi 550 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaokutana ili kusali na kumsikiliza Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Tarehe 8 Juni 2019, Ukumbi wa Mikutano wa Paulo IV utageuka kuwa ni uwanja wa shuhuda za maisha na utume wa Wakarismatiki kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko atatumia fursa hii kutoa ujumbe kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia na huo utakuwa ni mwanzo wa uzinduzi wa Kitengo cha CHARIS ambacho sasa kitaanza kutekeleza dhamana na utume wake kisheria. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, washiriki wote watahudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, lilimteua Jean-Luc Moens kuwa Mratibu wa kwanza wa CHARIS. Huyu ni Baba wa familia, yenye watoto 7 ambaye kwa muda wa miaka 45 amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma na utume kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki nchini Ubelgiji. Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ndiye Mshauri mkuu wa maisha ya kiroho ya Wakarismatiki duniani. Padre Cantalamessa aliteuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko.

Katika mkutano wa CHARIS, viongozi mbali mbali watatoa mada kuhusu: Upyaisho wa Kikarismatiki, mkondo wa neema kwa ajili ya Kanisa zima; Uinjilishaji, Umoja wa Wakristo, Huduma kwa Maskini; Changamoto katika Uinjilishaji mpya; CHARIS kama huduma ya umoja wa Kitaifa na Kimataifa; Malezi na majiundo makini, Tume ya Kitaalimungu ya CHARIS pamoja na shuhuda kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Charis: Uzinduzi
05 June 2019, 08:34