Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, limemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa hatua mbali mbali katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, limemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa hatua mbali mbali katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani: Shukrani kwa Papa Francisko

Baraza la Maaskofu linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kutoa mwongozo, sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kuchukuliwa pale kunapotokea shutuma za nyanyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Maaskofu wanasema, wanataka kuendeleza mapambano dhidi ya dhambi na uhalifu wa nyanyaso za kijinsia wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, katika mafungo ya mwezi Januari, 2019 yaliyoongozwa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa walibainisha kwamba, mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia yanahitaji nguvu za maisha ya kiroho na rasilimali fedha ili haki iweze kutendeka na watoto kupata mazingira salama kwa malezi na makuzi yao. Maaskofu wanapaswa kuwajibika kikamilifu katika misingi ya haki na imani, ili “kufyekelea mbali ndago za kashfa za nyanyaso za kijinsia” ili kuwajengea watu matumaini na Kanisa kuendelea kujitakatifuza kama njia ya kuimarisha utume na uinjilishaji wa kina!  

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia;  anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Barua hii ni kati ya mambo msingi ambayo Baraza Maaskofu Katoliki Marekani limekuwa likayajadili kwa kina na mapana katika mkutano wake wa Mwaka uliofunguliwa tarehe 11 Juni na kufungwa rasmi tarehe 14 Juni 2019. Maaskofu walipiga kura ili kupitisha Waraka wa Maaskofu unaotambua dhamana na wajibu wao wa Kikanisa kuhusu: Sheria, Taratibu na Kanuni zinazopaswa kufuatwa ili kupambana vyema na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Marekani.

Mkutano huu umefunguliwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kumwandikia Barua Baba Mtakatifu Francisko, kumwelezea kwamba, bado wanalo deni kubwa la kufanya toba, wongofu wa ndani ili kuambata utakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mafungo ya Mwezi Januari yaliwasaidia sana Maaskofu kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa nguvu ya sala; ili kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa.  Baraza la Maaskofu linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kutoa mwongozo, sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kuchukuliwa pale kunapotokea shutuma za nyanyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Maaskofu wanasema, wanataka kuendeleza mapambano dhidi ya dhambi na uhalifu wa nyanyaso za kijinsia wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mkutano wa Kanisa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo ndani ya Kanisa uliofanyika mjini Vatican mwezi Februari 2019 umekuwa na manufaa na utajiri mkubwa. Huu ni mkutano uliowashirikisha Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na viongozi wakuu wa Kanisa na hivyo kuwawezesha kusikiliza na kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, sanjari na kusikiliza shuhuda zilizotolewa na waathirika wa nyanyaso za kijinsia. “Ninyi ni nuru ya ulimwengu” ni maneno yanayowanyenyekesha na kuwawajibisha kuendelea kumtafakari Kristo Yesu, Nuru ya Ulimwengu; kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, Maaskofu wanaamini kwamba, wataweza kusonga mbele kwa nguvu ya sala.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linamshukuru Baba Mtakatifu  Francisko kwa Wosia wa Kitume: Christus vivit: Kristo anaishi! Ambamo anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Sinodi ya vijana na familia. Maaskofu Katoliki Marekani wanaendelea kupyaisha matumaini ya Baba Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo sanjari na kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kuendelea kuwekeza zaidi katika shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana.

Katika mkutano huu, Askofu mkuu William Lori wa Jimbo kuu la Baltimore, nchini Marekani amekiri kwamba, kuna baadhi ya Maaskofu wameshindwa kutekeleza vyema dhamana na utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Matokeo yake, wametumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia na kushindwa kuwajibika kimaadili dhidi ya watu walioshutumiwa kwa kesi za nyanyaso za kijinsia katika maeneo yao. Kashfa hii imechafua maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Marekani. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, linasema, litaendelea pia kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini au Eutanasia!

Askofu mkuu Christophe Pierre, Balozi wa Vatican nchini Marekani katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Monsinyo J. Brian Bransfield, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani amekazia umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu Katoliki Nchini Marekani. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni mwaliko wa kujifunga kibwebwe ili kuzuia; kwa kuzingatia ukweli na uwazi; kwa kutoa taarifa sahihi pamoja na kuendelea kuganga na kuponya madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia; jambo ambalo linahitaji uwajibikaji mkubwa wa Maaskofu mahalia. Waathirika wa nyanyaso za kijinsia wapewe kipaumbele na kushughulikiwa kadiri ya Sheria, taratibu na kanuni zilizopo.

Maaskofu Katoliki USA
26 June 2019, 16:11