Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linawahamasisha waamini walei kusimama kidete ili kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linawahamasisha waamini walei kusimama kidete ili kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko!  (ANSA)

Waamini walei, simameni kidete kuyatakatifuza malimwengu!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kwa kushirikiana kwa dhati kabisa na vyama pamoja na mashirika ya kitume. Mkutano huu umeongozwa na tema juu ya nyanyaso za kijinsia, ambazo kimsingi ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka, uchu wa mali, kiasi cha kudumaza maisha ya watu, hali ambayo imepelekea baadhi ya watu kutumbukia katika utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, vipigo vya wanawake majumbani, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wasichana na wanawake ni kati ya mambo ambayo yamejadiliwa hivi karibuni, kwa kina na mapana na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kwa kushirikiana kwa dhati kabisa na vyama pamoja na mashirika ya kitume. Mkutano huu umeongozwa na tema juu ya nyanyaso za kijinsia, ambazo kimsingi ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka, uchu wa mali, kiasi cha kudumaza maisha ya watu, hali ambayo imepelekea baadhi yao kutumbukia katika utamaduni wa kifo! Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Baraza lake limekabidhiwa dhamana ya kulinda na kutetea Injili ya uhai pamoja na kuwasindikiza waamini walei, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na utume wao katika Kanisa.

Kardinali Farrell amekazia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wote wa Mungu kusimama kidete ili kupambana dhidi ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusimamia ukweli na kuendelea kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuibua mbinu mkakati utakaonda mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi ya watoto ndani ya Kanisa pasi na woga wala wasi wasi wa kuibuka tena kwa nyanyaso za kijinsia ambazo kimsingi zimechafua sana maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei, vyama na mashirika ya kitume yanakumbushwa kwamba, yanayo dhamana na wajibu wa kuzuia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wa dogo, changamoto pevu na endelevu.

Watambue kwamba, hili ni kosa la jinai na hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza mwelekeo mpya wa maisha unaofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kushughulikia kikamilifu shutuma zote za nyanyaso za kijinsia. Kashfa hii imewagusa hata waamini walei katika ujumla wao, kumbe, huu si wakati wa kunyoosheana kidole, bali kupambana kufa na kupona na kashfa hii. Jambo la msingi ni kuboresha mahusiano kati ya waamini walei katika vyama vyao vya kitume, ili visigeuzwe na wajanja wachache kuwa ni kichaka cha “kuzalishia” kashfa kwa Kanisa na kwamba, wanapaswa kuwaheshimu walengwa wa huduma yao ya uinjilishaji pasi ya kuwageuza kuanza kuwatumia kwa mafao binafsi, kama ambavyo historia ya Kanisa inavyobainisha!

Vyama na mashirika ya kitume yajenge na kuboresha mazingira yatakayowawezesha kufikiri na kutenda kadiri ya Katiba zao, kwa kuondokana na saratani ya uchu wa mali na madaraka; utegemezi na upendeleo; pamoja na kuendelea kufunda dhamiri safi na nyofu. Pamoja na mambo yote haya, vyama na mashirika ya kitume hayana budi kuendelea kujikita katika malezi, makuzi na majiundo ya wanachama wao kwa kukazia: maisha ya kiutu, kanuni maadili na utu wema; maisha ya kiakili na kiroho. Baraza la Kipapa linawataka waamini walei kusoma kwa makini Barua binafsi yaani “Motu proprio” ya Baba Mtakatifu Francisko ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni madonda katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Madonda haya yanapaswa kugangwa na kuponyeshwa kwa toba, wongofu wa ndani na mwelekeo mpya unaokazia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Linda Ghisoni, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake amesema, nyanyaso hizi ni kati ya mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; kwa kuonesha unyonge na udhaifu wa mtu kushindwa kujitetea mwenyewe kutokana na nguvu kubwa inayoshinda uwezo wake! Hapa ndipo mtu anapojiona anadhalilishwa kwa macho makavu na wala hana uwezo wa kukimbia au kupambana na nyanyaso hizi na matokeo yake, anakuwa mpole tu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kashfa hii ni nyeti sana kwa sababu inagusa maisha na utume wa Kanisa.

Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, sanjari na kuendelea kumwilisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi, ili kupambanua sera na mikakati itakayoliwezesha Kanisa kufyekelea mbali kashfa za nyanyaso za kijinsia. Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Ulinzi wa Watoto, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian anasema, kashfa hii ni changamoto pevu katika masuala ya elimu, inayohitaji sera na mbinu mkakati wa kuzuia na kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyajnyaso za kijinsia. Kanisa linataka kujenga imani na matumaini; kwa kuamsha dhamiri za watu kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto wadogo, dhamana na wajibu kwa watu wote. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu mkakati wa “Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”.

Ikumbukwe kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni uhalifu wa hali ya juu kabisa unaoharibu maisha, utu na heshima ya watoto wadogo, kiasi cha kusababisha athari kubwa sana kwa watu! Waamini walei wajifunze mbinu mkakati wa kuwalinda watoto, ili kuhabarisha, kuwafunda waamini pamoja na kujenga mtandao utakaowalinda watoto hasa katika mazingira ya: kifamilia, maeneo ya michezo, malezi na majiundo ya watoto, ili kukuza na kujenga mahusiano yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili pamoja na nia njema.

Vyama vya Kitume
25 June 2019, 15:56