Tafuta

Askofu mkuu Bernardito Auza, amebainisha mambo makuu saba yanayoweza kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana dhidi ya vitendo vya kigaidi duniani! Askofu mkuu Bernardito Auza, amebainisha mambo makuu saba yanayoweza kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana dhidi ya vitendo vya kigaidi duniani! 

Vatican yabainisha mambo 7 ya kupambana na vitendo vya kigaidi!

Vitendo vya kigaidi vinahatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu. Hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini sanjari na umuhimu wa kutunza dhamiri nyofu! Vitendo vya kigaidi vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu ya umma. Hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini sanjari na umuhimu wa kutunza dhamiri nyofu! Vitendo vya kigaidi vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho”. Serikali zinalo jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, sanjari na kujenga utamaduni wa haki, amani, maridhiano pamoja na mafungamano ya kijamii. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati wa mjadala kuhusu udhibiti wa vitendo vya kigaidi unaojielekeza katika misingi ya imani: kukuza na kudumisha maridhiano na mafungamano ya kijamii.

Ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, Askofu mkuu Auza anasema, kuna haja kwanza kabisa: kujenga na kudumisha utamaduni wa maridhiano na mafungamano ya kijamii; kwa kuheshimu uhai kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; kwa kuthamini haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Pili ni kuhakikisha kwamba, watu wote wanakuwa na haki sawa mbele ya sheria za nchi bila upendeleo wa mahali anakotoka mtu, dini, kabila au nafasi yake katika jamii. Pale haki msingi za baadhi ya raia zinapovunjwa, sheria ichukue mkondo wake. Tatu, ni kutenganisha utendaji wa Serikali na dini; kwa kukazia ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Kuna hatari kwa viongozi wa kiserikali kutumia dini kwa ajili ya mafao binafsi pamoja na kujijenga kisiasa, kiuchumi na kijamii, hatari kubwa inayoweza kusababisha machafuko katika nchi.

Nne, ni kuhakikisha kwamba, viongozi wa kiserikali, kijamii na kidini, kwa pamoja wanaungana kukemea na kulaani watu wanaotumia dini kuchochea chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii inayopelekea hata kushamiri kwa vitendo vya kigaidi. Kamwe jina la Mwenyezi Mungu haliwezi kutumiwa kwa ajili ya kusababisha vita! Askofu mkuu Auza anasema, tano ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inawashughulikia na kuwahudumia waathirika wote wa vitendo vya kigaidi na wasiwepo wale wanaobaki nyuma! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupambana na hofu dhidi ya waamini wa dini wa Kiislam, Wayahudi na Wakristo. Hapa inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi Wakristo wanaposhambuliwa na vikundi vya kigaidi, viongozi na hata wakati mwingine, vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinashindwa kutaja moja kwa moja matukio haya kwa kutafuta lugha laini kama ilivyokuwa hivi karibuni nchini Sri Lanka.

Jambo la sita ni kuhakikisha kwamba, waamini wa dini na madhehebu mbali mbali wanaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Huu ni mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti hizi msingi ambazo ni amana na utajiri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Serikali mbali mbali zinapaswa kuunga mkono jitihada za majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi wao! Askofu mkuu Bernardito Auza anakaza kusema, jambo la saba ni elimu makini inayokita mizizi yake kwenye majadiliano, kanuni maadili na utu wema; haki, amani na upatanisho pamoja na kuheshimu utawala wa sheria. Kamwe mitandao ya kijamii isitumike kuwavuruga vijana kwa kuwapandikizia misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Ikumbukwe kwamba, mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu. Kumbe, kuna haja ya kudumisha uvumilivu na udumifu; hekima, busara na ujasiri pamoja na uongozi bora!

Vitendo vya Kigaidi
25 June 2019, 16:25