Tafuta

Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia 2019: Kardinali Claudio Hummes, Mwezeshaji mkuu; Askofu David M. A. Guinea & P. Michael Czerny, Makatibu Maalum. Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia 2019: Kardinali Claudio Hummes, Mwezeshaji mkuu; Askofu David M. A. Guinea & P. Michael Czerny, Makatibu Maalum. 

Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia: Uteuzi wa Mwezeshaji & Makatibu

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Claudio Hummes kuwa Mwezeshaji mkuu wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na Askofu David M. De Aguirre Guinea & P. Michael Czerny, kuwa Makatibu maalum wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Kauli mbiu : "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya maendeleo fungamani".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali: kuhusu: haki jamii, malezi ya awali na endelevu, katekesi makini, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia unaoziunganisha nchi tisa ambazo ni: Bolivia, Brazil, Colombia, Equador, Perù, Venezuela, Suriname na Guyana.

Hatua zote za maandalizi tayari zimekwisha kutekelezwa na kwamba, Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia iko tayari! Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Claudio Hummes, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Sao Paulo, Brazil, ambaye pia aliwahai kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuwa ni Mwezeshaji mkuu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Claudio Hummes, kwa sasa ni Rais wa Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, REPAM, ulioanzishwa kunako mwaka 2014 unaendelea kusimamia sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwenye Ukanda wa Amazonia. Mtandao huu ni matokeo ya Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean, uliofanyika huko Aparecida kunako mwaka 2007.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua pia Askofu David Martinez De Aguirre Guinea, O.P. wa Jimbo Katoliki la Puerto Maldonado nchini Perù, pamoja na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kuwa Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Papa: Sinodi Amazonia
06 May 2019, 10:08