Tafuta

Vatican News
Caritas Internationalis ni chombo cha huduma ya Injili na ujenzi wa udugu wa binadamu! Caritas Internationalis ni chombo cha huduma ya Injili na ujenzi wa udugu wa binadamu!  (Vatican Media)

Caritas Internationalis ni chombo cha Injili ya upendo na udugu!

Wajumbe wanatumia muda mrefu katika majadiliano ya vikundi. Lengo ni kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Katika kipindi cha Miaka minne ijayo kuanzia sasa, Caritas Internationalis imejiwekea Malengo Makuu 17, ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya kudumisha utu, heshima, haki, ustawi kwa kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 23 Mei, limefungua mkutano wake wa ishirini na moja kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 28 Mei 2019 na unawashiriklisha wajumbe 450 kutoka katika mataifa 164 na unaongozwa na kauli mbiu “Familia moja ya binadamu, nyumba moja kwa ajili ya wote”. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake alikumbusha kwamba, kutangaza na kushuhudia Injili ni mpango mkakati wa maisha na utume wa Kikristo.

Ili kutekeleza mpango mkakati huu, waamini hawana budi kujenga na kudumisha utamaduni wa unyenyekevu katika kusikiliza; umoja na mshikamano wa kidugu pamoja na moyo wa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kuwa mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kwa upande wake, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, Caritas Internatinalis inatoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kila mwamini anaweza kuchangia hata kwa kile kidogo alicho nacho kwa ajili ya kuenzi huduma inayotolewa na Caritas.

Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika huduma ya upendo. Mkutano huu ni fursa ya kusali, kutafakari na kushirikishana mang’amuzi ya maisha, ili kujenga ari na moyo wa utamaduni wa watu kushirikiana katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu katika huduma. Wajumbe wanatumia muda mrefu katika majadiliano ya vikundi ili kuweza kufikia azma hii. Lengo ni kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Katika kipindi cha Miaka minne ijayo kuanzia sasa, Caritas Internationalis imejiwekea Malengo Makuu 17, ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya kudumisha utu, heshima, haki, ustawi kwa kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu!

Caritas Internationalis inafanya mkutano wake wakati Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka minne, tangu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ulipozinduliwa rasmi mwaka 2015 unakazia utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko.

Caritas Internationalis
25 May 2019, 14:40