Tafuta

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linasema, vitendo vya kigaidi vinatishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linasema, vitendo vya kigaidi vinatishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii! 

Kanisa Afrika Magharibi: Ugaidi unatishia amani na maendeleo!

Kardinali Philippe Ouédraogo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger anasema, ni kwa njia ya umoja na mshikamano wa dhati, familia ya Mungu Afrika Magharibi inaweza kushinda changamoto ya vita, kinzani na mauaji ya kigaidi. Kwa siku za hivi karibuni, yameendelea kupukutisha maisha ya Wakristo, kama ilivyojitokeza huko Burkina Faso! Uhuru wa kuabudu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi (RECOWA-CERAO) kuanzia tarehe 13-20 Mei 2019 linaadhimisha mkutano wake mkuu wa tatu, huko Ouagadougou, nchini Burkina Faso. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji mpya na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, Familia ya Mungu Afrika Magharibi”. Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hotuba yake elekezi amesema, mkutano mkuu wa Pili wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Afrika Magharibi, uliofanyika kunako mwaka 2016 ulikazia zaidi: Upatanisho, maendeleo na familia kama changamoto za uinjilishaji Afrika Magharibi.

Leo hii, anasema kuna haja ya kuongeza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kama sehemu ya uinjilishaji, ili kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu sanjari na uporaji wa rasilimali na utajiri wa Afrika ya Magharibi unaofanywa na makampuni makubwa ya kigeni, wakati kuna maelfu ya watu wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, machafuko na vita! Kwa upande wake Kardinali Philippe Ouédraogo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na Niger anasema, ni kwa njia ya umoja na mshikamano wa dhati, familia ya Mungu Afrika Magharibi inaweza kushinda changamoto ya vita, kinzani na mauaji ya kigaidi.

Kwa siku za hivi karibuni, yameendelea kupukutisha maisha ya Wakristo, kama ilivyojitokeza huko kwenye Parokia ya Dablo ambapo magaidi walisababisha vifo vya waamini watano, akiwemo Padre Simèon Yampa. Hivi karibuni tena, magaidi wameshambulia maandamano ya kidini huko Singa na kusababisha mauaji ya waamini watano pamoja na uharibifu mkubwa wa Sanamu ya Bikira Maria. Kardinali Philippe Ouédraogo anasema, licha ya hali tete ya ulinzi na usalama nchini Burkina Faso, lakini Maaskofu kutoka nchi za Afrika Magharibi wamehudhuria mkutano huu kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Vitendo vya kigaidi vinahatarisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini kiasi hata cha kumong’onyoa mshikamano na mafungamano ya kijamii ndani na nje ya Afrika. Katika salam zake Bwana Jean Claude Kassi Brou, Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amelipongeza Kanisa kwa kuonesha nia ya kutaka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa haki, amani na maridhiano huko Afrika Magharibi. Lengo ni kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Rais Roch Marc Christian Kaborè wa Burkina Faso katika hotuba yake, amesikitika kusema kwamba, vitendo vya kigaidi ambavyo vimejitokeza nchini humo kwa siku za hivi karibuni, vinahatarisha sana uhuru wa kidini, umoja na mafungamano ya kijamii. Walengwa wakuu wa matukio ya kigaidi nchini Burkina Faso wamekuwa ni Wakristo. Amesema, hao waliosababisha mauaji hayo ni watu ambao kwa hakika wanakabiliwa na ukosefu wa kanuni maadili na utu wema. Nchi nyingi za Afrika Magharibi kwa sasa zinaendelea kupambana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Mkutano wa CERAO 2019
17 May 2019, 15:57