Kardinali Pietro Parolin: Vatican ina matumaini makubwa katika majadiliano na ushirikiano unaoendelea kujengeka na kuimarika kati ya Vatican na China Kardinali Pietro Parolin: Vatican ina matumaini makubwa katika majadiliano na ushirikiano unaoendelea kujengeka na kuimarika kati ya Vatican na China 

Kardinali Parolin: Majadiliano & Ushirikiano: Vatican & China!

Ujumbe wa Papa Francisko kwa China: Wawe ni vyombo na wajenzi wa umoja na upatanisho; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Waendeleze utamadunisho pamoja na kuwekeza tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili kwa vijana wa kizazi kipya! China na Vatican ziendeleze mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema,  tarehe 24 Mei ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, anayeheshimiwa sana kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Sheshan, huko Shanghai, nchini China. Hii ni siku maalum ambayo, Wakristo wote wanaungana kiroho na waamini Wakatoliki wanaoishi nchini China ili kusali na kuwaombea ili waendelee kuamini, kutumaini na kupenda. Sherehe hii ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815.

Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awawezeshe kuwa na ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!  Kunako mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamtangaza Bikira Maria kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China.

Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Gazeti la “Global Times” linalochapishwa kila siku nchini China, amegusia kuhusu matunda ya makubaliano ya mpito kati ya Vatican na Serikali ya China kuhusu dhamana na wajibu wa uteuzi wa Maaskofu Katoliki nchini China; Utamadunisho; ushirikiano kati ya nchi hizi mbili; nafasi na dhamana ya viongozi wa kisiasa pamoja na ujumbe kwa familia ya Mungu nchini China! Itakumbukwa kwamba, tarehe 22 Septemba 2018 Vatican na China vilitiliana sahihi makubaliano ya mpito kuhusu dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuteuwa Maaskofu Katoliki, makubaliano haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini China.

Haya ni matunda ya majadiliano, maridhiano na uvumilivu, ili kuganga na kuponya madonda ya kinzani na kutoelewana kati ya nchini hizi mbili. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoka kipaumbele cha pekee kwa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili familia ya Mungu nchini China iweze: kuamini, kutumaini na kupenda na hatimaye, kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao! Kardinali Parolin anakiri kwamba, kuna baadhi ya waamini na viongozi wa Kanisa nchini China wamekwaza na makubaliano haya ya mpito, lakini hii ni sehemu ya ukweli wa kibinadamu unaofumbatwa pia katika tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano yanayolenga kwenye maboresho ya shughuli za kichungaji nchini China; kwa kuheshimu na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika mapokeo ya China! Matunda na makubaliano haya ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano: kwa kusikilizana, ili hatimaye, kupata suluhu ya kudumu katika changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa binadamu. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wanaomba ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Utamadunisho wa Injili ni mbereko ya uinjilishaji na ushuhuda wa imani katika matendo. Mchakato huu nchini China ulianzishwa na Padre Matteo Ricci, ili kuwawezesha Wachina kuendelea kubaki Wachina, kwa kukita maisha yao katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Hii ni sehemu pia ya majadiliano ya kitamaduni. Wakatoliki nchini China ndio walengwa wakuu wanaopaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, katika upatanisho wa kweli, ili waweze kuwa Wachina pasi na hila na Wakatoliki kweli kweli.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Vatican na China zinaweza kushirikiana zaidi katika: kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kanuni maadili na utu wema katika tafiti na masuala ya kisayansi, bila kusahau uchumi fungamani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini China. Mambo muhimu ya kuzingatia ni: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Parolin anawakumbusha viongozi wa kisiasa na kijamii kwamba, uongozi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni huduma ya upendo hasa kwa maskini. Wawe ni watu wa imani na matumaini, wanaojitahidi kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu. Siasa iwe ni chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kumbe, wanasiasa wanapaswa kuwajibika barabara katika maamuzi na shughuli zao za kila siku! Kardinali Parolin ana mshukuru Mungu kwa kumwezesha kupata uzoefu na mang’amuzi makubwa katika mchakato wa majadiliano kati ya Vatican na Serikali ya China. Utashi wa kisiasa, uvumilivu na hali ya kuheshimiana ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya Vatican na China.

Ni fursa ya kufahamiana na kukuza yale mambo msingi yanayowaunganisha, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Anatambua mateso na mahangaiko ya Wakristo wengi nchini China, lakini hawa ni watu wenye matumaini makubwa! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini China ni huu: Wawe ni vyombo na wajenzi wa umoja na upatanisho; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Waendelee kujikita katika mchakato wa utamadunisho pamoja na kuwekeza tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili kwa vijana wa kizazi kipya!

China na Vatican ziendeleze mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Lengo ni kushinda kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Watu wawe ni wajenzi wa amani, umoja na udugu wa kibinadamu!

Parolin: Ushirikiano

 

24 May 2019, 10:10