Tafuta

Kardinali Parolin: Kanisa litaendelea kukuza na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kidugu! Kardinali Parolin: Kanisa litaendelea kukuza na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kidugu! 

Kardinali Parolin: Kanisa linataka kudumisha amani & umoja wa kidugu

Mama Kanisa daima ameendelea kujizatiti katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani, kwa kukazia ukweli na uwazi katika majadiliano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Lengo ni kukuza na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ndio mchango wa Papa Benedikto XV hadi Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mchakato wa ujenzi wa matumaini kati ya Mashariki na Magharibi kuanzia mwaka 1919 hadi mwaka 2019 ndiyo tema iliyoongoza kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Milano, Kaskazini mwa Italia, Jumanne, tarehe 14 Mei 2019. Kongamano hili limehudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Askofu Joseph Li Shan wa Jimbo kuu la Peking pamoja na Askofu Joseph Huang Bingzhang wa Jimbo Katoliki la Shantou lililoko nchini China.

Maaskofu hawa kwa mara ya kwanza wanahudhuria matukio kama haya, baada ya Vatican na China kutiliana mkataba wa mpito kuhusu uteuzi wa Maaskofu, hatua kubwa katika kukuza majadiliano kati ya pande hizi mbili! Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine anapenda kukazia zaidi: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu; Umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, mintarafu mpango wa Mungu wa kutaka kumkomboa mwanadamu. Umoja katika utofauti ni jambo linalowezekana. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa ni alama na Sakramenti ya Wokovu; ni chombo cha umoja na mshikamano kati ya Mungu na binadamu.

Kardinali Pietro Parolin katika hotuba yake elekezi amesema, Mama Kanisa daima ameendelea kujizatiti katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani, kwa kukazia ukweli na uwazi katika majadiliano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Lengo ni kukuza na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ndio mchango uliotolewa na Papa Benedikto XV; Papa Pio XI na Papa Pio XII. Wengine ni Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mama Kanisa anawakumbuka pia Mtakatifu Paulo VI, Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko kwa wakati huu!

Papa Benedikto XV aliliongoza Kanisa wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na kutangaza kwamba, hii ni vita isiyofaa na ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao pasi na sababu msingi. Tangu wakati huo, Kanisa likaanza kuwa na mwelekeo mpya kuhusu masuala ya vita. Papa Benedikto XV katika Wosia wake wake wa Kitume “Pacem Dei Munus Pulcherrimum” yaani “Amani ni Zawadi Kubwa ya Mungu”, akawataka watu wa Mataifa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza mchakato wa upatanisho.

Ni katika muktadha huu, Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” yapata miaka 100 iliyopita. Ndiyo maana Mama Kanisa anasema kwamba, huu ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwaliwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Huu ndio utume ambao Mama Kanisa anataka kuutekeleza pia katika Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuangalia Mashariki, lakini China, ikipewa msukumo wa pekee. Huu ni mwaliko wa kujikita katika unyenyekevu.

Papa Benedikto XV alikazia utamadunisho wa imani pamoja na kuhakikisha kwamba, Kanisa mahalia linapata pia mihimili ya Uinjilishaji, kwani Kanisa linataka kuwa kweli ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wa Mataifa kwa kuendeleza pia majadiliano ya kidini; kwa kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia pamoja na mafungamano kati ya watu. Papa Pio XI na Papa Pio XII waliendelea kukazia umoja na mshikamano wa familia ya binadamu iliyokuwa inatishwa kutokana na nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wayahudi. Kanisa likaitaka familia ya binadamu kudumisha usawa na umoja; upendo na mshikamano wa dhati; kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Kanisa linasema, hakuna kitu chochote kinachoweza kupotea kwa njia ya amani, lakini vita inaweza kupoteza yote! Uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na China haukuwa mzuri sana tangu nyakati za akina Matteo Ricci na wenzake anasema Kardinali Pietro Parolin, kwani walionekana kuwa kama wapinzani wakuu dhidi ya tamaduni na mapokeo ya Kichina. Baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, Kanisa likaendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa binadamu. Kanisa likawa mstari wa mbele kuyasaidia mataifa machanga katika mchakato wa maendeleo fungamani. Hii ndiyo dhana iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Matunda ya tafakari hii ni Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”. Kimsingi amani ya kweli inafumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Huu ukawa ni ujumbe mahususi wakati ambapo walimwengu walikuwa wanaendelea kupigana vita baridi! Haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, vinapaswa kuzingatiwa na wote! Mtakatifu Paulo VI mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki akachapisha Waraka wa Kitume, "Ecclesiam suam" yaani "Kanisa la Bwana", Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaani: Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na utamadunisho.

Mtakatifu Paulo VI akajitahidi kumwilisha mafundisho haya kwa hija mbali mbali, lakini zaidi kwa kutembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na kuwahutubia wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume “Populorum progressio” yaani “Kuhusu Maendeleo ya watu” akakazia zaidi kuhusu umoja na mshikamano wa watu wa Mungu ili kujenga na kudumisha udugu na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu!

Ulinzi na usalama ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani duniani. Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa Mstaafu Benedikto XVI pamoja na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wao, wamekumbana na changamoto ya mashindano ya silaha za kinyuklia, kuporomoka kwa misngi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kanisa likasema, vita ni matokeo ya binadamu kushindwa kujadiliana katika ukweli na uwazi. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, watu wanapaswa kujikita katika kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi, uchoyo na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto!

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ni dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo kwa kukazia ari na mwamko wa kimisionari; kwa kuzishughulikia changamoto mamboleo kwa mwanga wa Injili; umuhimu wa uinjilishaji na mwelekeo wake wa kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maendeleo fungamani ya binadamu yanafumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu, heshima, umoja na udugu wa kibinadamu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Pietro Parolin anasema, Kanisa linapenda kujielekeza zaidi nchini China. Tarehe 22 Septemba, 2018, Vatican na China viliwekeana sahihi Mkataba wa Mpito kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia nchini China. Lengo ni huduma kwa Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China pamoja na kuendeleza majadiliano, katika kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Papa Francisko anasema, amani ya kweli inasimikwa katika majadiliano yanayowawezesha watu wa mataifa kushirikiana na kushikamana, ili kuwaletea watu wa Mungu ustawi na maendeleo ya kweli.

Mkataba wa Mpito ni nyenzo ya majadiliano kati ya Vatican na Serikali ya China, Kati ya Vatican na Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini China, ili kudumisha wongofu wa ndani na upatanisho unaolenga kuimarisha umoja wa Kanisa. Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin kwamba, Kanisa kwa msaada na neema ya Mungu sanjari na ushirikiano na wadau mbali mbali litaweza kujenga ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya: haki, amani, umoja, udugu wa kibinadamu, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika ujumla wake!

Kard. Parolin: Milano
15 May 2019, 16:07