Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz, Profesa na Mtaalam wa Kemia atangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz, Profesa na Mtaalam wa Kemia atangazwa kuwa ni Mwenyeheri. 

Mwenyeheri Prof. Maria Guadalupe: Mtaalam wa Kemia aliyebobea!

Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri alikuwa ni Jaalimu aliyebobea katika tafiti za sayansi ya kemia. Alibahatika kuweka uwiano mzuri kati ya Habari Njema ya Wokovu na shughuli zake za kisayansi. Upendo kwa Mungu na jirani; Ibada na maisha ya sala; pamoja na kujiaminisha mbele ya Mungu vilikuwa ni kati ya vipaumbele vilivyotawala maisha ya Mwenyeheri huyu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi, tarehe 18 Mei 2019, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemtangaza mtumishi wa Mungu Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri wa Fernàndes de Heredia kuwa ni Mwenyeheri. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa huko Jimbo kuu la Madrid, nchini Hispania. Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri alikuwa ni Jaalimu aliyebobea katika tafiti za sayansi ya kemia. Alibahatika kuweka uwiano mzuri kati ya Habari Njema ya Wokovu na shughuli zake za kisayansi.

Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz Alizaliwa mwaka 1916 na kubahatika katika maisha yake ya ndoa kupata watoto 4. Baba yake mzazi aliuwawa kikatili wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania. Akabahatikakujiendeleza sana katika elimu na kunako mwaka 1944 akabahatika kukutana na Mtakatifu Josemarìa Escrivà aliyebadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake na kujisikia ari na moyo wa kutaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kwa kujiunga na Shirika la Opus Dei, yaani “Kazi ya Mungu”.

Ndani ya Shirika hili, nyota yake ikaendelea kung’ara na kupewa majukumu mbali mbali aliyoyatekeleza kwa nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji wa kina! Aliendelea kujisadaka kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya. Kwa hakika alikuwa ni mwanamke wa shoka na alihakikisha kwamba, anajiendeleza zaidi katika masomo na hatimaye, akajipatia shahada ya uzamivu katika kemia. Akatumia karama na vipaji vyake kuanzisha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kwa ajili ya watoto wa wakulima, ili hata wao waweze kushiriki katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kulinda, utu, heshima na haki zao msingi.

Kwa ushuhuda wa maisha na wito wake kama mwamini mlei, akasaidia sana kuhamasisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Alipokuwa anatoa katekesi kwa vijana, anaongoza mafungo ya kiroho na huduma kwa maskini, watu wengi “walimvulia kofia” kutokana na uwezo wake mkubwa kiasi hata cha watu kumpachika jina la “Profesa wa Mungu”. Upendo kwa Mungu na jirani; Ibada na maisha ya Sala pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ni mambo ambayo aliyapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yake.

Ni mwanamke aliyebahatika kushuhudia imani iliyokuwa inamwilishwa katika matendo. Akawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani, akawa kweli ni shuhuda na chombo cha furaha ya Injili na huduma ya upendo kwa maskini! Kunako mwaka 1957 akapata ugonjwa wa moyo, aliojitahidi  kuupokea kwa moyo wa unyenyekevu, imani na matumaini kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Katika hali ngumu na changamoto za maisha, kunako mwaka 1965 akatetea kazi yake ya utafiti na hivyo kutunikiwa shahada ya uzamivu katika kemia. Alibahatika kupata tuzo nyingi kutokana na tafiti mbali mbali za kisayansi alizozifanya enzi ya uhai wake, akabahatika kuwafunda vijana kuwa wanasayansi waliobobea na mashuhuda wa Kristo Mfufuka. Akafariki dunia tarehe 16 Julai 1975 wakati wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu katika mahubiri yake amekaza kusema, Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri alikuwa ni mwanga wa Kristo, zawadi ambayo aliitoa kwa njia ya huduma kwa jirani zake, akawa mwaminiifu wa tunu msingi za Kiinjili na shuhuda wa upendo wa Mungu kwa jirani zake. Ni mwamini aliyerutubisha maisha yake kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Ibada kwa Bikira Maria. Katika shida na mahangaiko yake ya ndani, Kristo Yesu alikuwa ni kimbilio lake la daima. Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri ni mfano bora wa kuigwa na waamini wengine katika kumwilisha: Sala na Kazi; Taamuli na Taaluma; kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kutekeleza mapenzi yake.

Alikuwa ni Jaalimu mwenye kipaji cha kusikiliza; kuvumilia na kutafuta ukweli wa mambo kisayansi; na hatimaye, amekuwa kweli ni zawadi kwa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, yampasa kila mmoja, kadiri ya vipawa vyake na majukumu yake, kuendelea mbele bila kusitasita katika njia ya imani iliyo hai, iamshayo matumaini na kutenda kwa mapendo! Maneno haya yanapata utimilifu wake katika maisha na utume wa Mwenyeheri Maria Guadalupe Ortiz de Landàzuri.

Mwenyeheri M. Guadalupe
18 May 2019, 16:08