Majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo yajenge misingi ya haki, amani na maridhiano sanjari na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji duniani! Majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo yajenge misingi ya haki, amani na maridhiano sanjari na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji duniani! 

Majadiliano ya kidini: Wayahudi & Wakristo: Huduma kwa wakimbizi

Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi liwe ni kutoa huduma ya pamoja kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kupambana na watu wenye misimamo mikali dhidi ya Wayahudi; dhuluna na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu uendeleze majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi nchini Italia na Israeli, ili hatimaye. kupanua wigo zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi liwe ni kutoa huduma ya pamoja kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kupambana na watu wenye misimamo mikali dhidi ya Wayahudi; dhuluna na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu uendeleze majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi nchini Italia na Israeli, ili hatimaye, kuvuka mipaka ya nchi hizi mbili, ili kuendelea kupanua wigo wa majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huduma!

Mkutano wa Kamati ya Washauri wa Kimataifa wa Majadiliano ya Kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi, IJCIC, pamoja na wajumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kuanzia tarehe 13-16 Mei 2019 wamekuwa na mkutano wao wa 24, mwendelezo wa utekelezaji wa Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, “Nostra aetate” yaani “Nyakati zetu” linalohusu majadiliano ya kidini. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, ndilo lilolokuwa mwenyeji wa mkutano huu ulioratibiwa na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Rabi Daniel Polish. Wajumbe walibahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Italia, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia pamoja na Jumuiya ya Wayahudi wa Roma.

Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Watu, Mawazo, Mipaka na Safari”. Wajumbe wameguswa kwa namna ya pekee na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani pamoja na kuhoji sera na mikakati ya chuki na uhasama zinazotaka kuwatumbukiza watu katika maafa makubwa. Viongozi wa kidini wanapaswa kuwasaidia watunga sera, wahudumu katika miundo mbinu ya huduma za kijamii ili kufanya maamuzi sahihi katika maisha ya watu. Ushirikiano kati ya wadau mbali mbali katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, unapaswa kuwa ni endelevu, wa kudumu na unaowawajibisha wahusika kujikita katika utu!

Wajumbe wametoa ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Jumuiya za waamini wa dini hizi mbili zilivyoweza kujibu changamoto za huduma ya kibinadamu, kwa kutoa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji. Jumuiya hizi zimeonesha umakini mkubwa wa matumizi sahihi ya rasilimali watu na fedha kwa weledi na ubunifu, uzoefu na manga’muzi yanayopaswa kuendelezwa hata kwa siku za usoni! Wajumbe wamekazia pia umuhimu wa  kukuza na kudumisha malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kusaidia huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kama walivyojifunza kutoka katika Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake makuu mjini Roma.

Jumuiya hii imekuwa ni msaada mkubwa wa huduma kwa makini, wakimbizi na wahamiaji ambao wanatoka katika mataifa mbali mbali, wakiwa na lugha, tamaduni, dini, imani na mapokeo tofauti, yanayopaswa kuzingatiwa pia! Tofauti zote hizi ni utajiri na amana inayopaswa kusaidia ujenzi wa mchakato wa umoja katika utofauti! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 15 Mei 2019 alikutana na kuzungumza na Wajumbe wa Kamati ya Washauri wa Kimataifa wa Majadiliano ya Kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi, IJCIC, pamoja na wajumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa ishirini na nne kimataifa!

Tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua mchakato wa majadiliano ya kidini na katika Tamko lao la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu”, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa binadamu! Baba Mtakatifu alisema, mkutano huu unapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mambo wanayowaunganisha ili kukuza na kudumisha: umoja, mshikamano na ushirikiano wa dhati. Lengo ni kutoa huduma ya pamoja kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kupambana na watu wenye misimamo mikali dhidi ya Wayahudi; dhuluna na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.

Mkutano huu uendeleze majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi nchini Italia na Israeli, ili hatimaye, kuvuka mipaka ya nchi hizi mbili. Baba Mtakatifu alipenda kuwatia shime kuendeleza majadiliano ya kidini, ili kuweza kufahamiana vyema zaidi na hivyo kujenga mazingira ya maridhiano pamoja na waamini wa dini hizi mbili kuthaminiana. Wajenge utamaduni wa waamini wa dini hizi mbili kukutana, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini. Maandiko Matakatifu yanasema: “Hila imo moyoni mwa wafikirio uovu, bali wafanyao mashauri, amani, kwao kuna furaha” (Mit 12: 20). Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amesema, mkutano huu uwe ni wa amani kwa ajili ya amani ulimwenguni!

Papa: Majadiliano
20 May 2019, 09:12