Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin amemtembelea Askofu mkuu mteule Ante Jozic aliyepata ajali hivi karibuni huko nchini Croatia. Kardinali Pietro Parolin amemtembelea Askofu mkuu mteule Ante Jozic aliyepata ajali hivi karibuni huko nchini Croatia.  (ANSA)

Askofu mkuu mteule Jozic apata ajali mbaya, Croatia!

Monsinyo Ante Jozic, Mei Mosi, 2019 alikuwa awekwe wakfu kuwa Askofu mkuu, Lakini kutokana na ajali mbaya ya gari aliyoipata tarehe 7 Aprili 2019 akalazimika kulazwa hospitalini nchini Croatia. Kardinali Pietro Parolin, Mei Mosi, 2019 amemtembelea Askofu mkuu mteule Ante Jozic, ili kumjulia hali, pamoja na kumfikishia salam za pole kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni amemteua Monsinyo Ante Jozic, kuwa Balozi mpya wa Vatican huko Pwani ya Pembe na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu. Mei Mosi, 2019 alikuwa awekwe wakfu kuwa Askofu mkuu, tayari kwenda kutekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe. Lakini kutokana na ajali mbaya ya gari aliyoipata tarehe 7 Aprili 2019 akalazimika kulazwa hospitalini nchini Croatia. Kardinali Pietro Parolin, Mei Mosi, 2019 amemtembelea Askofu mkuu mteule Ante Jozic, ili kumjulia hali, pamoja na kumfikishia salam za pole kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu mteule Ante Jozic alizaliwa tarehe 16 Januari 1967 huko Trilj, nchini Croatia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Monsinyo Ante Jozic, akajiendeleza zaidi katika masomo ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na kujipatia Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe 1 Julai 1999 akaanza utume wa kidiplomasia mjini Vatican. Katika kipindi chote hiki, amewahi kufanya utume wake kwenye Ofisi za Ubalozi wa Vatican huko: India, Urussi na Ufilippini.

Askofu mkuu mteule Jozic ni mtaalam wa mahusiano kati ya China na Vatican, Kati ya Kardinali John Tong Kong, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong. Kardinali Pietro Parolin, hospitalini hapo aliambatana na viongozi mbali mbali kutoka Ubalozi wa Vatican nchini Croatia pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa nchini humo. Amekutana na kusalimiana pia na ndugu, jamaa na marafiki wa Askofu mkuu mteule Ante Jozic.

Askofu mkuu: Jozic

 

03 May 2019, 15:20