Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa asema, atawajibika mbele ya sheria kwa kutetea maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa asema, atawajibika mbele ya sheria kwa kutetea maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! 

Kardinali Krajewski asema atawajibika kwa kutetea maskini!

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza sadaka ya Kipapa baada ya kurejea mjini Vatican, asikia kilio cha mahangaiko ya watu zaidi ya 400 waliokatiwa umeme mjini Roma kutokana na kushindwa kulipa bili ya umme. Matokeo, watu wakakosa umeme na maji ya moto, hali ambayo ilikuwa inahatarisha sana usalama na maisha ya watoto na wazee waliokuwa wanaishi kwenye jengo moja mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa, hivi karibuni amefanya hija ya kichungaji kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Visiwa vya Lesvos, huko nchini Ugiriki. Baada ya kurejea mjini Vatican, alisikia kilio cha mahangaiko ya watu zaidi ya 400 waliokatiwa umeme mjini Roma kutokana na kushindwa kulipa bili ya umme. Matokeo, watu wakakosa umeme na maji ya moto, hali ambayo ilikuwa inahatarisha sana usalama na maisha ya watoto na wazee waliokuwa wanaishi kwenye jengo moja mjini Roma.

Kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na kilio cha watu hawa maskini ambao wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji pamoja na wananchi wa Italia wanaoteseka kutoka na umaskini mkubwa, akamua kwenda kwenye jengo hilo na kuwasha tena umeme kwa ajili ya matumizi ya watu hawa maskini, waliokuwa wanaoteseka kutokana na umaskini. Kitendo hili kimeonekana kuwa ni uvunjwaji wa sheria, kanuni na taratibu za huduma ya umeme nchini Italia! Kardinali Konrad Krajewski anasema, amefanya hivyo kwa kuguswa na utu, heshima na mahangaiko ya maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anasema, anafahamu fika matokeo yake na kwamba, yuko tayari kukabiliana na mkondo wa sheria na hata kama ni kulipa faini, lakini maskini wa Roma wapate umeme na maji ya moto!

Watu 400 wengi wao wakiwa ni watoto na wazee, kukosa umeme ni hatari sana. Kardinali anafahamu mateso na mahangaiko ya wananchi wanaoishi katika jumba lile! Haiwezekani watu wote hawa kutelekezwa bila kupatiwa huduma muhimu. Jambo la msingi ni kujiuliza ni kwa nini watu hawa wamekimbilia kupata hifadhi kwenye jengo ambalo lilikuwa limetelekezwa? Inakuaje, watu wenye utu na heshima yao, wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi kiasi hiki? Kardinali Konrad Krajewski anasema yuko tayari kuwajibishwa kisheria, lakini ataendelea kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Kardinali Konrad
13 May 2019, 15:00