Kardinali Parolin: Hija ya Papa Francisko: Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini: Mjumbe wa amani na umoja wa watu wa Mungu Kardinali Parolin: Hija ya Papa Francisko: Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini: Mjumbe wa amani na umoja wa watu wa Mungu 

Hija ya kitume: Macedonia ya Kaskazini & Bulgaria: Umoja & Amani

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, hija hii imejikita kwa namna ya pekee, kama kikolezo cha umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na ukarimu kwa watu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia yale mambo msingi yanayowaunganisha watu, ili kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 29 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Bulgaria na Macedonia ya Kaskazini, kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris” yaani “Amani duniani” pamoja na “Msiogope enyi kundi dogo”. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, hija hii imejikita kwa namna ya pekee, kama kikolezo cha umoja na mshikamano wa kitaifa; amani na ukarimu kwa watu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia yale mambo msingi yanayowaunganisha watu, ili kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa pili kutembelea Bulgaria, baada ya hija ile ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002. Amani ni zawadi ya kwanza ya Kristo Mfufuka kwa wafuasi wake waliokuwa wanaelemewa na hofu kuu ya Wayahudi, baada ya kushuhudia kashfa ya Fumbo la Msalaba. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru kamili;  kwa kudumisha usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kardinali Parolin anakaza kusema, amani ni msingi wa wema, heshima na ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Amani ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Baba Mtakatifu katika hija hii ni hujaji wa amani na shuhuda wa Kristo Mfufuka. Hii ni amani ambayo inapaswa kuangaliwa kwanza kabisa mintarafu Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XXIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anayesema kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika msingi wa: ukweli, haki, upendo na uhuru. Ni kwa njia ya msamaha na upatanisho, amani inaweza kukuzwa na kudumishwa.

Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha yake, aliwahi kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Bulgaria. Kwa muda wa miaka kumi, aliishi na kutekeleza dhamana na utume wake nchini Bulgaria. Baba Mtakatifu Francisko anataka kukazia kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika misingi iliyobainishwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume. Hii ni changamoto ya kutafuta na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu; kwa kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu, katika upendo.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua,  huu ni mwaliko wa kuchuchumilia yale mambo msingi yanayowaunganisha zaidi, kuliko kuhangaikia yale yanayowagawa na kuwasambaratisha. Huu ndio mchango ambao Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuuendeleza wakati wa hija yake ya kitume nchini Bulgaria. Baba Mtakatifu katika hija hii anapenda pia kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, yanayosimikwa kwa namna ya pekee katika uekumene wa damu unaobubujika kutoka katika ushuhuda wa waamini kwa Kristo na Kanisa lake; uekumene wa sala, kwa kushirikiana na kusaidiana katika maisha ya kiroho, lakini zaidi ni uekumene wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa njia hii, kweli Wakristo watakuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu atakuwa na nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria. Atatoa heshima zake kwa watakatifu Cyril na Metodi, waliokita maisha na utume wao katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano; wakazama zaidi katika uinjilishaji na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Bado kuna ukakasi na migawanyiko miongoni mwa Wakristo anasema, Kardinali Parolin, kumbe ni wajibu wa waamini kuhamkikisha kwamba wanavuka vikwazo vyote hivi ili waweze kuwa wamoja, tayarai kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Parolin anakaza kusema, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji zinaongozwa na mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu ataonesha uwepo wake wa karibu kwa kutembelea kambi za wakimbizi na wahamiaji. Kanisa linataka kusimama kidete ili: kulinda na kudumisha: usalama, utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Habari Njema, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa na waamini.

Macedonia ya Kaskazini ni nchi ambayo ina ibada kubwa kwa Watakatifu Cyril, Metodi na Mama Theresa wa Calcutta. Lakini ibada na upendo kwa Mama Theresa wa Calcutta ni kubwa, kutokana na majitoleo yake kama shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, upendo hauna budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia watu kuondokana na mifumo inayosababisha umaskini duniani, ili hata wao waweze kukua na kukomaa.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha mahojiano haya kwa kusema, hija hii ya kitume ina umuhimu wake kijiografia, ikizingatiwa kwamba, Bulgaria ni makutano ya watu kutoka katika tamaduni na imani mbali mbali. Baba Mtakatifu anataka kukazia tena umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja hata katika tofauti msingi, kama sehemu ya kutajirishana na kukamilishana katika hija ya maisha ya hapa duniani! Macedonia ya Kaskazini ni nchi ambayo ina makabila, dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, utajiri mkubwa kwa familia ya Mungu nchini humo!

Kardinali Parolin
03 May 2019, 17:40