Tafuta

Vatican News
Mwenyeheri Maria Concepciòn Cabrera Arias de Armida, Conchita".  Alikuwa na Ibada kwa Bikira Maria na alikazia utakatifu wa mapadre. Mwenyeheri Maria Concepciòn Cabrera Arias de Armida, Conchita". Alikuwa na Ibada kwa Bikira Maria na alikazia utakatifu wa mapadre. 

Mwenyeheri "Conchita": Ibada kwa Maria & Utakatifu wa Mapadre!

Mwenyeheri Maria "Conchita" Katika maisha yake, alikubali kupokea mateso na changamoto za maisha na kuzitoa kuwa ni sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa ni mwanamke mwenye upendo kwa Mungu na jirani. Alijaribiwa sana katika maisha, kwani alishuhudia watoto wake wanne, wakipoteza maisha mbele yake, akayapokea yote haya na kuyatolea kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi, tarehe 4 Mei 2019, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemtangaza mtumishi wa Mungu Maria Concepciòn Cabrera Arias de Armida, maarufu kama “Conchita” kuwa Mwenyeheri. Ibada hii ya Misa takatifu imeadhimishwa Jimbo kuu la Mexico, huko nchini Mexico. Mwenyeheri Maria Concepcion Cabrera alikuwa ni mwamini mlei na mama wa familia aliyebahatika katika maisha yake kupata watoto tisa, kati ya mwaka 1862 hadi mwaka 1937.

Ni mama aliyekuwa na Ibada pamoja na upendo mkubwa kwa Bikira Maria, akajizamisha katika Fumbo la Msalaba na akawa ni faraja ya watu waliokuwa wanateseka: kiroho na kimwili. Katika maisha yake, alikubali kupokea mateso na changamoto za maisha na kuzitoa kuwa ni sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa ni mwanamke mwenye upendo kwa Mungu na jirani. Alijaribiwa sana katika maisha, kwani alishuhudia watoto wake wanne, wakipoteza maisha mbele yake, akayapokea yote haya na kuyatolea kwa Mwenyezi Mungu. Ni mama aliyesali na kuombea wongofu na utakatifu wa mapadre ndani ya Kanisa. Aliwaona Mapadre kuwa ni “Kristo mwingine” katika maisha yake na kwamba, ndani yake, alihisi kuwa ni Mama wa Mapadre na aliwaona kuwa kama watoto wake wapendwa!

Licha ya shughuli zote hizi, lakini ni mwanamke wa shoka aliyeandika sana kuhusu amana na utajiri wa maisha ya kiroho. Kazi hii kwa sasa imekusanywa katika vitabu 158. Vitabu hivi vimekuwa ni chemchemi ya kuanzishwa kwa Shirika la Mitume wa Msalaba nchini Mexico pamoja na Mashirika mengine matano. Kanisa linaendelea kumkumbuka kama mwamini aliyesimama kidete kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, amana na utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Alikuwa ni mwanamke mwenye kipaji cha ubunifu kilichosaidia kulijenga na kuliimarisha Kanisa. Kwa hakika alikuwa ni mama mwenye matumaini makubwa kwa Kristo Yesu na daima alimwomba kuendelea kulipyaisha Kanisa lake kwa njia ya utakatifu wa maisha!

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kukaa mioyoni mwao kwa imani, wakiwa na shina na msingi katika upendo, ili wapate kufahamu pamoja na watakatifu wote upendo wa Kristo unaovuka ufahamu, ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wote wa Mwenyezi Mungu! Upendo kwa Mungu na jirani ulimwezesha kutumia muda mwingi zaidi katika tafakari mbele ya Ekaristi Takatifu, chemchemi ya upendo wake wa kimama na faraja kwa wale wote wanaoteseka! Upendo kwa jirani, ulimwezesha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii!

Fumbo la Msalaba lilikuwa ni alama ya huruma, upendo na wokovu wa binadamu. Alikazia umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho na utakatifu wa Mapadre, changamoto mamboleo ili kuweza kuganga na kuponya madonda ya kashfa ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Waamini watambue karama na nguvu zao katika ujenzi wa Kanisa. Waamini wawe na ujasiri wa kukiri udhaifu wao, tayari kukimbilia katika huruma na upendo wa Mungu. Mwenyeheri Maria Concepcion Cabrera katika maisha yake, alifanikiwa kuunganisha sala na kazi; “Ora et Labora” kama ilivyokuwa kwa Maria na Martha ndugu zake Lazaro. Ni mfano bora wa kuigwa na wanawake sehemu mbali mbali za dunia katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni matumaini ya Kardinali Giovanni Angelo Becciu kwamba, familia ya Mungu nchini Mexico itaweza kumwilisha changamoto zilizotolewa na Mwenyeheri huyu kama amana na utajiri wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu. Aendelee kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanao ogelea katika umaskini wa hali na kipato, ili waweze kupata msaada unaobubujika kutoka katika Injili ya upendo unaotangazwa na kushuhudiwa na wafuasi wa Kristo Yesu.

Mwenyeheri: Conchita
06 May 2019, 11:14