Tafuta

Daktari  Denis Mukwege mtuzwa Nobel ya Amani 2018 akisalimiana na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake tarehe 22 Mei 201 Daktari Denis Mukwege mtuzwa Nobel ya Amani 2018 akisalimiana na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake tarehe 22 Mei 201 

Baba Mtakatifu Francisko asalimiana na Dk.Denis Mukwege

Mara baada ya kumaliza katekesi,Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kusalimiana na Dk.Denis Mukwege,Mtuzwa Nobel ya amani 2018.Baadaye amezungumza na waandishi wa Radio Vatican kwa lugha ya kifaransa na kiswahili na kusisitizia juu ya umuhimu wa jamii kufuata sheria maana kwa kuidharau,matokeo yake ni kama tunavyoona nchini DRC.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Tarehe 22 Mei 2019 mara baada ya katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko amepata kusalimiana na Daktari Denis Mukwege, Mtuzwa Nobel ya amani 2018. Taarifa hizo ni kutoka kwa msemaji wa mpito wa vyombo vya habari Dk. Alessandtro Ghisotti. Daktari Denis Mukweke alizaliwa huko Bukavu kunako tarehe 1 Machi 1955.  Amekuwa Daktari mashuhuri hasa katika nyanja ya utetezi wa wanawake waathirika wa ubakakwaji katika nchi ya DRC. Na mara baada ya kutoka katika uwanja wa Mtakatifu Petro kuudhuria katekesi na kumsalimia Baba Mtakatifu,Dk Mukwege amefika  katika Jengo la Radio Vatican na kuhojiwa ndani ya studio na mwandishi wa habari kwa lugha ya kifaransa, lakini pia hata kutoa ufupisho kwa lugha ya kiswahili kwa  kile kilichozungumzwa katika mahojiano.

Amani kuhusu nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Dr. Mukwege katika kufafanua kwa ufupi kile ambacho kimeweza kuzungumzwa katika mahojiano kwa  lugha ya kiswahili amesema: “Wasikilizaji wapenzi wa kiswahili ningepena kuwambia sababu ya uwepo wangu hapa Radio Vatican. Jambo ambalo nimeweza kuzungumza zaidi ni kuhusu amani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na  amani  hii wanasema haiwezi kupatikana bila kuwa na sheria. Ikiwa sheria haiheshimiki, ikiwa watu hawafuati sheria, wale ambao wametenda vitendo vya ujeuri, wanaoua watu wataendelea kufanya hivyo tu, kwa sababu hakuna kile kinacho wazuia kufanya na ndiyo maana tunaomba na tunaita Umoja wa Mataifa ili wasaidie kuleta Ripoti yenye majina ya hawa, ambao wametenda ujeuri, ambao wameua watu kiholela. Watu hawa wapelekwe mahakamani ili wajue la kujitetea kwa kile ambacho wametenda”.

Haki tunayo itafuta siyo ya watu kwenda jela bali ni kurejesha iliyo haribika

Dk. Mukwege akiendelea na maelezo kuhusu haki amesema: “Na hii ambayo tunaita “justice” “haki”  siyo tu ya kusema kwamba  watu wapelekwe jela, lakini zaidi kuitengeneza ile ambayo imeharibika ili kuhepusha watu wasirudie kutenda mabaya, kwa maana inaleta hali ya uelewa ndani ya jamii ya kile ambacho jamii inapaswa kufanya na kile ambacho haipaswi kufanya na mwisho, nafikiri kwamba, sheria ni ile ambayo inaweza kusaidia watu kujua kila mmoja yupo ngazi ipi na anapaswa kufanya nini, ili jamii nzima iweze kuendelea. "Lakini- amesisitiza-  tunapo dharau sheria ni kwamba mambo yote yanaharibika na ndiyo mfano huo leo hii unaonekana nchini Congo, kwa maana kila mmoja anafanya anachopenda na anaharibu na hii inaharibu jamii na taifa lote. Asante”, amehitimisha Dk. Mukwege.

Sauti ya Dk. Mukwege…

Dk Mukwege

Dk. Denis Mukwege ni mtaalamu wa masuala ya uzazi wa wanawake DRC

Dk. Denis Mukwege ni mtaalamu wa masuala ya uzazi ya wanawake ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC  na  tangu mwaka 1988 alianzisha Hospitali ya Panzi, hospitali ambayo kwa sasa imekuwa maalum duniani kote  katika kuuguza madhara ya ndani ya miili ya wanawake wengi   yaliyo sababishwa na kubakwa. Dr. Mukwege alitunukiwa tuzo ya Nobel ya amani 2018 pamoja na Nadia Murad ambapo Kamati ya Nobel ilimtaja kijana huyo kwamba: yeye ni mmoja wa wasichana na wanawake takriban 3,000 wa jamii ya Yazidi ambao ni waathiriwa wa ubakaji na udhalilishwaji wa kingono uliotekelezwa na wapiganaji wa Serikali ya kiislam. Hata hivyo Dk Mukwege pamoja na wenzake wameweza kuwatibu na kuwafanyia upasuaji wa kurekebisha viungo maelfu ya waathirika wa udhalilishaji wa kingono, wengi ambao walidhalilishwa vitani.  Kunako mwaka 2014 Bunge la Ulaya lilimpatia  Zawadi  ya Sakharov kwa ajili ya uhuru wa mawazo na baada ya miaka minne ndipo  akatunukiwa tuzo ya Nobel ya Amani.

Waathiriwa 30,000 wa ubakaji kufikia mwaka 2013 na Hospitali yake inafadhiliwa

Halikadhalika Dk. Denis Mukwege ambaye amekuwa akishughulikia afya ya wanawake nchini DRC inasadikika kuwa na wenzake wameweza kuwahudumia waathirika 30,000 wa ubakaji kufikia mwaka 2013.  Hata hivyo katika hospitali yake ni kuwa kuna wakati waliobakwa waliweza kujaza  hata vitanda vyote 350 vya hospitali ya Denis Mukwege. Mradi huu wa daktari Mukwege unafadhiliwa na shirika la kuwahudumia watoto la Unicef na wahisani wengine. Waathiriwa pia hutibiwa katika zahanati inayo hamishwa hamishawa na ambayo pia inafadhaliwa na wahisani hao hao.  Dk.  Mukwege anasifiwa kwa kujitolea maisha yake yote ya utu uzima kuwatibu maelfu ya wahanga wa ubakaji na unyanyasaji mwingine wa kijinsia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hususan eneo la mashariki mwa nchi hiyo, na kuwa sauti ya kuwatetea. Oktoba mwaka 2012, Dk. Mukwege alinusurika jaribio la kuuwawa, ambapo dereva wake alipoteza maisha. Kamati ya Tuzo ya Nobel ilisema Mukwege na Nadia wamekuwa alama ya umoja wa kitaifa na kimataifa, katika kupambana na unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya mizozo. Washindi waliotangazwa mwaka 2018 walichaguliwa kutoka orodha ya watu 216 na mashirika 115, ambayo yalikuwa yamewasilishwa mbele ya kamati. Orodha hiyo ni ya pili kwa ukubwa kuwahi kupokewa na kamati hiyo!

22 May 2019, 14:46