Tafuta

Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO 2019: Uinjilishaji mpya, Maendeleo fungamani na Familia ya Mungu Afrika Magharibi. Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO 2019: Uinjilishaji mpya, Maendeleo fungamani na Familia ya Mungu Afrika Magharibi. 

Askofu mkuu Rugambwa: Kanisa Barani Afrika: Familia & Maendeleo!

Askofu mkuu Rugambwa amekazia umuhimu wa Kanisa kudumisha maendeleo fungamani ya binadamu. Kanisa linapaswa kukabiliana na changamoto changamani kwa ari na moyo mkuu wa Kiinjili; kuendeleza mchakato wa uinjilishaji na utume wa Kanisa, ili hatimaye, kujenga na kudumisha Kanisa kama familia ya Mungu inayosimikwa katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi (RECOWA-CERAO) linaadhimisha mkutano wake mkuu wa tatu, kuanzia tarehe 13-20 Mei 2019 huko Ouagadougou, nchini Burkina Faso, kwa uwepo na ushiriki wa Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye amewasilisha ujumbe kutoka kwa Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji mpya na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, Familia ya Mungu Afrika Magharibi”.

Ufunguzi wa mkutano huu umehudhuriwa pia na viongozi wakuu kutoka Serikali ya Burkina Faso pamoja na viongozi wa kidini. Askofu mkuu Rugambwa katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa Kanisa kuendeleza na kudumisha maendeleo fungamani ya binadamu. Kanisa linapaswa kukabiliana na changamoto changamani kwa ari na moyo mkuu wa Kiinjili; kuendeleza mchakato wa uinjilishaji na utume wa Kanisa, ili hatimaye, kujenga na kudumisha Kanisa kama familia ya Mungu inayosimikwa katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati!

Askofu mkuu Rugambwa anasema, lengo liwe ni kufyekelea mbali ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Afrika Magharibi na badala yake, kukuza na kudumisha umoja na upatanisho wa kitaifa! “Uinjilishaji mpya na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, Familia ya Mungu Afrika Magharibi” ni tema inayoleta matumaini, lakini pia inaibua changamoto changamani kwa viongozi wa Kanisa ambao wamepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Askofu mkuu Rugambwa anasema, kumekuwepo na ongezeko kubwa la miito ya kipadre na kitawa sanjari na ongezeko la vyama pamoja na mashirika ya kitume, miongoni mwa waamini walei. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, ari na moyo wa kimisionari, umekuwa na kuongezeka ndani na nje ya Afrika Magharibi. Hizi ni dalili kwamba, Kanisa la Mungu ni hai na linaendelea kutoa ushuhuda, kwa kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu, kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pasi na ubaguzi.

Ukosefu wa: haki, amani; ulinzi na usalama; demokrasia na maendeleo fungamani ni kati ya changamoto kubwa zinazogumisha maisha na utume wa Kanisa huko Afrika Magharibi. Umaskini, mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukabila, misimamo mikali ya kidini na kiimani, vitendo vya kigaidi pamoja na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu ni changamoto pevu. Licha ya Ukristo kuenea kwa miaka mingi, lakini inasikitisha kuona kwamba, bado kuna baadhi ya waamini ambao waanendeleza dini zao za asili kwa kujikita katika imani potofu za ushirikina na ukanimungu; mambo yanayochangia kukwama kwa ukuaji wa imani.

Askofu mkuu Protase Rugambwa amekumbusha kwamba, mkutano mkuu wa Pili wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Afrika Magharibi, uliofanyika kunako mwaka 2016 ulikazia zaidi: Upatanisho, maendeleo na familia kama changamoto za uinjilishaji Afrika Magharibi. Leo hii, kuna haja ya kuongeza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kama sehemu ya uinjilishaji, ili kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu sanjari na uporaji wa rasilimali na utajiri wa Afrika ya Magharibi unaofanywa na makampuni makubwa ya kigeni, wakati kuna maelfu ya watu wanaendelea kuogelea katika umaskini na vita!

Mama Kanisa anatumwa kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, yu hai kati ya waja wake; chanzo na kilele cha mchakato mzima wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kumkomboa mwanadamu na kwamba, uinjilishaji ni utambulisho wa maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, uinjilishaji wa kina hauna budi kwenda sanjari na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.Kanisa Afrika Magharibi, liendelee kujenga na kuimarisha dhana ya Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika kwa kujenga na kudumisha: upendo, umoja na maridhiano, ili kuondokana na ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Afrika ya Magharibi.

Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo yanayotekelezwa na Kanisa zima. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya Kanisa kuwafunda viongozi wa Kikristo watakaojisadaka bila ya kujibakiza katika utekelezaji wa shughuli za kitume na kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa. Kwa maneno mengine, ni kuwashirikisha kikamilifu waamini walei katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Itakumbukwa kwamba, CERAO, ni Baraza la Maaskofu wa Afrika Magharibi lililokuwa linaundwa na Maaskofu waliokuwa wanazungumza lugha ya Kifaransa na lilianzishwa kunako mwaka 1963.

Na Baraza la RECOWA lilianzishwa kunako mwaka 1977 na lilikuwa linawajumuisha Maaskofu waliokuwa wanazungumza lugha ya Kiingereza. Kwa kuunganisha Mabaraza haya, kumeonesha mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa nchi za Afrika Magharibi. Tendo hili anasema, Kardinali Filoni ni muhimu sana, ili kuwawezesha Maaskofu kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kichungaji kwa umoja na mshikamano wa dhati.

Askofu mkuu Rugambwa

 

16 May 2019, 17:11