Tafuta

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yameanza mkutano wake mkuu: Kufahamiana; Malezi na Majiundo Makini, Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 & Taalimungu katika shughuli za kichungaji. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yameanza mkutano wake mkuu: Kufahamiana; Malezi na Majiundo Makini, Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 & Taalimungu katika shughuli za kichungaji. 

Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa: Ufunguzi

Hotuba ya ufunguzi: Maandalizi ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”, Maandalizi ya Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini, CAM5; Umuhimu wa kutandaza msingi wa kitaalimungu katika sera na mikakati ya shughuli za kimisionari na kwamba, kwa mwaka huu, tema inayoongoza mkutano huu ni shughuli za kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, Jumatatu, tarehe 27 Mei 2019 amefungua mkutano wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, unaoendelea hapa mjini Roma hadi tarehe 1 Juni 2019. Ametumia fursa hii kuelezea yale yaliyojiri tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kushika wadhifa huu, maandalizi ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”, Maandalizi ya Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini, CAM5; Umuhimu wa kutandaza msingi wa kitaalimungu katika sera na mikakati ya shughuli za kimisionari na kwamba, kwa mwaka huu, tema inayoongoza mkutano huu ni shughuli za kichungaji.

Mwaka 2018-2019 umekuwa ni mwaka wa kufahamiana na Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, shughuli mbali mbali zinazofanywa na Mashirika haya katika mchakato wa malezi na majiundo ya mihimili ya uinjilishaji, kwa hakika inapendeza sana. Malezi na majiundo makini ya wakurugenzi wa Mashirika haya ni kati ya vipaumbele vilivyobainishwa na Mkutano mkuu uliopita! Amewafanikiwa kukutana na kuzungumza na Maaskofu walipokuwa wanafanya hija za kitume mjini Vatican. Kwa sasa Baraza linaandaa mwongozo kwa ajili ya Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa.

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hiki Kiwe ni kipindi cha: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia! Askofu mkuu Giampietro Dal Toso amesema, Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini litakaloadhimishwa kunako mwaka 2022 huko Puerto Ricco, itakuwa ni kumbu kumbu ya miaka 400 tangu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu lilipoanzishwa, Miaka 200 tangu Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yalipoanzishwa na miaka 100 yalipotambuliwa rasmi na Mama Kanisa kama chombo cha uinjilishaji kwa watu wa Mataifa.

Askofu mkuu Dal Toso amekazia umuhimu wa Mama Kanisa kutoa msingi wa kitaalimu kwa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja ya kuibua mbinu mkakati mpya wa kuhamasisha waamini kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua changamoto kubwa ya uinjilishaji mpya iliyoko mbele ya Kanisa. Mashirika haya hayana budi kusonga mbele kwa kusoma alama za nyakati! Taalimungu ya utume wa Kanisa ni muhimu kufafanuliwa, ili iweze kueleweka na wengi, kama sehemu ya mkakati wa kuhamasisha ari na mwamko wa shughuli za kimisionari ndani ya Kanisa.

Dal Toso: PMS
28 May 2019, 15:45