Tafuta

Vatican News
Huruma na upendo wa Mungu hauna mipaka! Huruma na upendo wa Mungu hauna mipaka!  (Vatican Media)

Askofu mkuu Fisichella: Huruma ya Mungu haina mipaka!

Waamini wamegundua tena umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho; uwepo wa Wamisionari wa huruma ya Mungu na Ijumaa ya huruma ya Mungu kama mbinu mkakati wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wahitaji zaidi. Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia zaidi juu ya “huruma ya Mungu” katika maisha na utume wa Kanisa, mwaliko na changamoto kwa Mama Kanisa kulitafakari tena “Fumbo la Huruma ya Mungu kama chemchemi ya furaha, utulivu wa ndani na amani na kwamba, huruma ni sharti muhimu sana la wokovu na ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu”. Hili ndilo chimbuko la maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya kufunga maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Ibada ya huruma ya Mungu imepata msukumo wa pekee kutoka kwa Mtakatifu Faustina Kowalska na kuvaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyethubutu hata kuanzisha Jumapili ya Huruma ya Mungu kunako mwaka 2000. Baba Mtakatifu Francisko akatangaza Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa waamini kuweza kuadhimisha tukio hili wakiwa kwenye majimbo yao, bila kulazimika sana kwenda kufanya hija mjini Roma.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu anasema kwamba, kati ya kumbu kumbu endelevu za maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu ni: Waamini kugundua tena umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho; uwepo wa Wamisionari wa huruma ya Mungu na Ijumaa ya huruma ya Mungu kama mbinu mkakati wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kumrudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni Sakramenti inayomfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma ya Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa ni fursa kwa waamini wengi kuweza kutubu na kumwongokea tena Mwenyezi Mungu katika maisha yao kwa kukimbilia katika Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho. Wamisionari wa huruma ya Mungu wamekuwa ni alama ya hamasa ya umama wa Kanisa kuingia katika utajiri wa Fumbo la imani yaani, huruma ya Mungu ambayo haina mipaka kwa waja wake. Kwa njia ya Wamisionari wa huruma ya Mungu, waamini wengi wamepata nafasi ya msamaha na maondoleo ya dhambi zao. Wamisionari wa huruma ya Mungu kwa kweli wanatambua kwamba, wao ni wadhambi na wamekuwa watu wa kwanza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa.

Huruma ya Mungu inajionesha katika maisha ya watu kwa kuwasaidia kutubu na kuongoka, ili hatimaye, kushirikiana na Mungu kama vyombo na mashuhuda wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Mwenyezi Mungu anachukua hatua ya kwanza ili kuonesha upendo kwa mdhambi, kama ilivyo kwa Mama Kanisa kuanza kwa ushupavu kuwaendea na kuwatafuta walioanguka, waliotengwa na kuwakaribisha ili kuwaonjesha tena  mang’amuzi ya huruma ambayo ni matunda ya nguvu ya Baba isiyokuwa na kikomo.

Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu  wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, alijiwekea utaratibu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yake, dhamana ambayo anajitahidi kuiendeleza kila wakati anapopata fursa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Fisichella: Huruma ya Mungu

 

01 May 2019, 14:04