Tafuta

Vatican News
Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2018: "Christus vivit" unazinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019. Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2018: "Christus vivit" unazinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019.  (AFP or licensors)

Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2018: Uzinduzi rasmi!

Papa Francisko hapo tarehe 25 Machi 2019 ameweka mkwaju kwenye Wosia wa Kitume wa “Vive Cristo, esperanza nuestros”. Na kwa lugha ya Kilatini, Wosia huu unajulikana kama “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu kusikiliza mpango wa Mungu na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Ni matunda ya safari ndefu ya utume wa Kanisa kwa vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia huu wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Christus Vivit” yaani “Kristo anaishi” unaazinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019, Mama Kanisa anapokumbuka siku ile Mtakatifu Yohane Paulo II, Muasisi wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani alipoaga dunia, mjini Vatican na kuzikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2005. Huu ni Wosia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao! Wosia huu unazinduliwa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Katika jopo hili kuna Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Wengine katika tukio hili la maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya ni pamoja na Mama Laphidil Oppong Twumas, Mratibu wa Utume wa Vijana wa Ghana Jimbo Katoliki la Vicenza, nchini Italia pamoja na Profesa Piroddi Lorrai, Mwalimu wa Shule ya Sekondari, Jimbo kuu la Roma.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa Mama wa Mungu, “Theotokos”, hapo tarehe 25 Machi 2019 ameweka mkwaju kwenye Wosia wa Kitume wa “Vive Cristo, esperanza nuestros”. Na kwa lugha ya Kilatini, Wosia huu utajulikana kama “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu kusikiliza mpango wa Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Sehemu ya pili ni kung’amua, ili kushiriki katika mpango wa Mungu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza. Sehemu ya tatu ni kuamua, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, aliyekubali kuwa ni Mama wa Mungu.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018 yaliongozwa na kauli mbiu “Vijana, Manga’amuzi na Miito”. Sinodi ya vijana ilikuwa ni mwendelezo wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, ndiyo maana, Baba Mtakatifu anakazia kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya utume wa familia na utume wa vijana. Kumbe, ni dhamana na jukumu la familia kuwarithisha vijana tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili waweze kuwa kweli ni watakatifu na raia wema, tayari kukuza na kudumisha: umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Christus Vivit

 

01 April 2019, 14:41