Tafuta

Vatican News
Umoja wa Watangazaji Barani Afrika: Umuhimu wa kuwa na Jukwaa la tasnia ya mawasiliano ya jamii Barani Afrika kwa kukazia: maudhui na teknolojia! Umoja wa Watangazaji Barani Afrika: Umuhimu wa kuwa na Jukwaa la tasnia ya mawasiliano ya jamii Barani Afrika kwa kukazia: maudhui na teknolojia!  (ANSA)

AUB: Tasnia ya mawasiliano na changamoto zake Barani Afrika!

Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu ”Njia mpya za mawasiliano na athari zake katika sekta ya utangazaji Barani Afrika. Wajumbe wamekitaka chombo hiki kuendelea kujikita katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia kutoka katika matumizi ya teknolojia ya analogia kuelekea teknolojia ya digitali, kama sehemu ya maboresho ya mawasiliano Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano mkuu wa Kumi na mbili wa Umoja wa Watangazaji Barani Afrika, ”African Union of Broadcasting” AUB, uliokuwa unafanyika mjini Marrakesh nchini Morocco kuanzia tarehe 25-29 Machi 2019 umekamilika. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu ”Njia mpya za mawasiliano na athari zake katika sekta ya utangazaji Barani Afrika. Wajumbe wamekitaka chombo hiki kuendelea kujikita katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya teknolojia kutoka katika matumizi ya teknolojia ya analogia kuelekea teknolojia ya digitali, kama sehemu ya upyaisho wa huduma inayotolewa na vituo vya Radio na Televisheni Barani Afrika.  

Hii ni changamoto inayojikita katika masuala ya kiuchumi, kifedha na kijamii, mwaliko kwa nchi wanachama kushikamana na kushirikiana kwa karibu zaidi katika kubadilishana teknolojia na vipindi mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya tasnia ya habari Bara la Afrika kwa kuwa na Jukwaa la mawasiliano kwa nchi za Kiafrika! Itakumbukwa kwamba, AUB kwa mwaka 2018 ulilenga mchakato wa kuzima mitambo ya analogia na kuanza kujielekeza zaidi katika teknolojia ya kidigitali pamoja na changamoto zake.

Maudhui katika vyombo vya mawasiliano ya jamii Barani Afrika yalipewa msisitizo wa pekee. Mkutano mkuu wa kumi na mbili, imekuwa ni fursa nyingine tena kuangalia utekelezaji wa sera na mikakati iliyopangwa kwa mwaka 2018. Wamegusia mchango wa Mamlaka za mawasiliano katika mchakato wa kuhama kutoka katika teknolojia ya analogia kuelekea teknolojia mpya ya kidigitali; madhara yake katika mazingira, dhana ya mapato katika teknolojia mpya ya kidigitali; changamoto zake pamoja na mbinu mkakati wa kulunda na kutunza mazingira nyumba ya wote Barani Afrika bila kusahau masuala ya michezo ya mpira wa miguu Barani Afrika!

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe wake kwenye mkutano huu amekazia umuhimu wa Bara la Afrika kuwa na jukwaa la tasnia ya mawasiliano kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Ni mwaliko wa kushirikishana, ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi sanjari na kuzingatia kanuni, maadili, sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa, ili haki iweze kutendeka! Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika ukuzaji wa sekta ya mawasiliano Barani Afrika.

Dr. Paolo Ruffini, amekazia umuhimu wa kuzingatia maudhui, ili kuwaunganisha watu, badala ya sera zinazolenga kuwagawa na kuwasambaratisha. Mawasiliano yawalenge watu wengi zaidi, ili kukuza na kudumisha majadiliano yanayorutubishwa na ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waandishi wa habari wanapaswa kuwa wakereketwa wa kutafuta na kudumisha ukweli na kamwe wasijiridhishe na makandokando ya nje; majibu mepesi mepesi au kutumiwa kwa ajili ya masilahi ya watu wachache katika jamii!

Bw. Joseph Kambanga, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ufundi kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ni kati ya wajumbe waliohudhuria mkutano huu. Katika mahojiano maalum kutoka kwa Dr. Maria Dulce Araujo E’vora wa Vatican News, amegusia masuala mbali mbali yaliyojadiliwa na wajumbe kwenye mkutano huu! Amegusia umuhimu wa wadau watasnia ya mawasiliano Barani Afrika kushikamana kwa kushirishana habari na teknolojia; umuhimu wa kuzingatia maudhui katika habari kwa kuondokana na habari za kughushi ”Fake news”. Maendeleo ya teknolojia ya digitali, usimamizi, uratibu na udhibiti wa mawasiliano nchini Tanzania unaotekelezwa kwa dhati kabisa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA. Bwana Joseph Kambanga ameipongeza Radio Vatican kwa kukuza na lugha ya Kiswahili na kwamba, TBC imeanzisha pia Kipindi maalum cha Utalii ili kukuza sekta ya utalii wa ndani na nje!

Kauli mbiu ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2018 ilikuwa ni “Kweli itawaweka huru" Yoh. 8:32. Habari potofu na uandishi wa amani". Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waandishi wa habari kujikita katika uandishi unaopania kujenga na kudumisha amani duniani. "Fake news" yaani “Habari potofu" ni mada inayochangamkiwa sana na vyombo pamoja na taasisi mbalimbali kutokana na unyeti na utata wake katika maisha ya watu na taasisi husika. Baba Mtakatifu anawataka wadau katika tasnia ya mawasiliano yaa jamii kujikita katika kanuni maadili, weledi, uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza haki ya watu kupata habari za kweli na za uhakika, muhimu katika ujenzi na udumishaji wa Injili ya amani duniani! Habari za kughushi zimeleta madhara makubwa sana katika maisha ya watu binafsi, serikali na jamii katika ujumla wake!

Uandishi wa habari unaosimikwa katika ukweli unapania kuleta umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii kati ya watu! Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, leo hii mwanadamu anakumbana na mafuriko ya habari za kughushi, changamoto kwa wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete kupinga habari za kughushi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na weledi wa uandishi wa habari; kwa wanahabari wenyewe kuwajibika kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia ukweli! Habari za kughushi anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni habari tenge inayojikita katika takwimu zilizochakachuliwa au hata zile ambazo hazipo kabisa, ili kumwadaa msomaji, msikilizaji au hata mtazamaji! Habari za kughushi ni dalili za kukosekana kwa maridhiano katika jamii, hali inayopelekea kusambaa kwa jeuri, chuki na uhasama kati ya watu.

Ili kutambua habari za kughushi kuna haja ya kujenga na kukuza mfumo wa elimu utakaowawezesha watu kutafsiri na kupata habari za uhakika zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na kuwajengea uwezo wa kufichua habari za kughushi. Pili, kuna haja ya kukuza na kudumisha utawala wa sheria ili kuhakikisha kwamba, wale wote wanaohusika na habari za kughushi wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu zilizopo. Tatu, Makampuni ya mawasiliano ya jamii, yasaidie kuweka vyombo vitakavyofichua habari za kughusi, hali ambayo inahitaji mchakato wa mang’amuzi ya kina, ili ukweli uweze kung’ara katika maisha ya watu na hivyo kuondokana na dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu na jirani.

Wajumbe wameridhika na changamoto iliyotolewa na viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika katika kusaidia mchakato wa mabadiliko ya teknolojia, ili kwenda na wakati pamoja na kuhakikisha kwamba, vituo vya Radio na Televisheni Barani Afrika vinatoa huduma bora zaidi kwa ajili ya wananchi wa Bara la Afrika. Wizara zinazohusika na masuala ya habari na mawasiliano ya jamii Barani Afrika hazina budi kuhakikisha kwamba, zinaratibu mabadiliko haya, ili kusaidia ufanisi wa mawasiliano Barani Afrika pamoja na kuendelea kushirikiana na AUB kwa karibu zaidi.

Umoja wa Watangazaji Afrika
11 April 2019, 10:56