Tafuta

Sr. Eugenia Bonet, wa Shirika la Waconsolata ameteuliwa na Papa Francisko kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu 2019 kuzunguka Magofu ya Colosseo. Sr. Eugenia Bonet, wa Shirika la Waconsolata ameteuliwa na Papa Francisko kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu 2019 kuzunguka Magofu ya Colosseo. 

Tafakari Njia ya Msalaba 2019: Ijumaa Kuu: Utumwa mamboleo!

Chama cha Kiraia cha “Slaves No More” kilianzishwa tarehe 29 Desemba 2012 na watawa pamoja na waamini walei wanaopambana dhidi ya biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sr. Bonet anasema, lengo ni kusaidia mchakato wa kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu, tarehe 19 Aprili 2019 imeandaliwa na Sr. Eugenia Bonet wa Shirika la Consolata ambaye pia ni Rais wa Chama cha Kiraia “Slaves No More”. Kiini cha tafakari hii ni mateso, nyanyaso na dhuluma zinazojitokeza katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo! Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa mpito mjini Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko amemkabidhi Sr. Bonet dhamana ya kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba.

Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 ambao wametumbukizwa katika biashara hii inayozalisha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 32 kwa mwaka na hivyo kuchuana kwa karibu sana na biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya duniani. Wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio walengwa wakuu katika biashara hii na wengi wao ni wale wanaotoka katika nchi za Amerika ya Kusini, Afrika na nchi za Ulaya Mashariki ambazo kwa miaka mingi zilikuwa chini ya utawala wa Kikomunisti.

Chama cha Kiraia cha “Slaves No More” kilianzishwa tarehe 29 Desemba 2012 na watawa pamoja na waamini walei wanaopambana dhidi ya biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sr. Bonet katika mahojiano na Vatican News anakaza kusema, lengo ni kusaidia mchakato wa kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo, kwa kuunda mtandao utakaowashirikisha wadau mbali mbali, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana ambao wengi wao wanatumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Biashara hii inapaswa kupigwa vita tangu kule wanakotoka waathirika hawa, nchi wanakopitia na hatimaye, nchi wanakopelekwa kutumikishwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anasikitika kusema, utumwa mamboleo upo na wala si jambo lililopitwa na wakati” na wala hakuna mtu anayeweza kujitoa kabisa kwamba, hausiki na janga hili, kwani kwa namna moja au nyingine, anashiriki katika biashara ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Waathirika wa biashara na utumwa mamboleo ni watu wanaoonekana kila kukicha, wakiwa wameandikwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Ni watu ambao wamepachikwa majina kama vile: wahamiaji wa kiuchumi, wakimbizi, wahamiaji haramu, watu wasiokuwa na makazi maalum; watoto wasiosindikizana na wazazi au walezi wao. Ni watu wanaosafiri katika misafara mikubwa ya watu pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali!

Kinachosikitisha ni kuona kwamba, wengi wanasahau kwamba, hawa ni binadamu, wenye utu, heshima na historia yao! Kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo! Hawa ni watu wanaozikimbia familia na nchi zao kutokana na vita, baa la njaa na utapiamlo; madhulumu na nyanyaso za kisiasa na kidini, umaskini wa kutisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna makundi makubwa ya uhalifu wa kitaifa na kimataifa yanayofaidika, kwa kuwatumbukiza watu katika utumwa mamboleo. Hawa ndio wale watoto wanaofanyishwa kazi za suluba; biashara ya ngono; biashara ya binadamu na viungo vyake na hata wakati mwingine wanajikuta wakilazimishwa kushiriki na kuridhia vitendo vya kihalifu.

Askofu Mkuu Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, kuna haja ya kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kutokomeza: kazi za suluba, biashara ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana; mambo ambayo yanazidi kuongezeka kila kukicha! Waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, wanapaswa kuwezeshwa, ili kuanza kuandika tena ukurasa mpya wa maisha yao! Vatican itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ili kupambana na biashara ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo.

Kanisa tayari limekwisha kutoa Mwongozo kwa ajili ya kupambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Mkazo katika Mwongozo huu kwanza kabisa ni kusaidia kulipa deni la wahusika, kuwapatia nafasi ya kujifunza kazi pamoja na kuwapatia kazi itakayowawezesha kuwa na kipato chenye uhakika pamoja na kuwa na makazi bora zaidi. Huduma kwa waathirika wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni mchakato unaowashirikisha wadau wengi, kumbe, washirikiane, ili kulinda utu na heshima ya wanawake!

Tafakari ya Njia ya Msalaba 2019
06 April 2019, 16:43