Viongozi wa Kiserikali na Kidini Sudan ya Kusini: Siku mbili za: Sala, Tafakari na Upatanisho mjini Vatican. Viongozi wa Kiserikali na Kidini Sudan ya Kusini: Siku mbili za: Sala, Tafakari na Upatanisho mjini Vatican. 

Sudan ya Kusini: Sala, Tafakari na Upatanisho mjini Vatican

Ni wimbo wa amani, haki, uhuru, ustawi na maendeleo ya wengi! Mambo msingi yaliyowasindikiza viongozi wakuu wa Serikali na kidini kutoka Sudan ya Kusini katika mafungo ya kiroho kuanzia tarehe 10-11 Aprili 2019 mjini Vatican. Tukio hili linakita mizizi yake katika: majadiliano ya kiekumene, maisha ya kiroho na kidiplomasia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 11Aprili 2019 kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni kielelezo cha kilio cha ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu anayeguswa na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kutokana na vita, njaa na magonjwa pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu: mambo yanayoendelea kusababisha maafa na majanga makubwa nchini humo! Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana kwa kufanikisha mchakato wa kuwakutanisha viongozi wa Serikali na Kidini kutoka Sudan ya Kusini mjini Vatican kwa ajili ya kusali, kutafakari na kujipatanisha kabla ya kuanza utekelezaji wa mchakato wa Serikali ya Umoja wa Kimataifa inayotarajiwa kuanza kufanya kazi hapo tarehe 12 Mei 2019.

Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini katika wimbo wa taifa lake, inamwomba, inamshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake! Ni wimbo wa amani, haki, uhuru, ustawi na maendeleo ya wengi! Haya ni mambo msingi ambayo yamewasindikiza viongozi wakuu wa Serikali na kidini kutoka Sudan ya Kusini katika mafungo ya kiroho kuanzia tarehe 10-11 Aprili 2019 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, hili ni tukio linalokita mizizi yake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, maisha ya kiroho na kidiplomasia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, Sudan ya Kusini.

Hiki kimekuwa ni kipindi muafaka cha tafakari, toba, wongofu wa ndani, tayari kuanza mchakato wa upatanisho, msamaha na ujenzi wa umoja wa kitaifa. Viongozi wa Serikali na Kidini nchini Sudan ya Kusini, wamejiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu wakiomba: haki, amani, msamaha, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa! Sudan ya Kusini, kuanzia mwaka 2013 ilijikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha maafa na majanga makubwa kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ndiye aliyewakaribisha viongozi wa Serikali na Kidini kutoka Sudan ya Kusini, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Anasema, Kwaresima ni kipindi muafaka cha toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli si tu kwa ajili ya wakleri na watawa hata kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Kwaresima ni kipindi cha neema na baraka; ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha madaraja na utamaduni wa watu kukutana na Mwenyezi Mungu katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji!

Viongozi wa Serikali na Kidini nchini Sudan ya Kusini, wanao wajibu na dhamana maalum wanayopaswa kuitekeleza hapo tarehe 12 Mei 2019, mwanzo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Dhamana hii, inawataka viongozi wote hawa kuweka pembeni kasoro, kinzani na misigano yao, tayari kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ujenzi na maendeleo ya Sudan ya Kusini, yanayosimikwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Askofu mkuu John Baptist Odama wa Jimbo kuu la Gulu, Uganda pamoja na Padre Agbonkhianmeghe Orobator, Myesuit na ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ndio walioongoza mafungo haya!

Padre Agbonkhianmeghe Orobator katika mafungo yake, amewasihi sana viongozi wa Serikali na Kidini nchini Sudan ya Kusini kuambata mchakato wa kukutana na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. Huu ni mchakato unaopania kuganga, kuponya na kutasaka, tayari kuanza utume wao kama wajenzi na mashuhuda wa misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa. Wahusika wote walialikwa kufanya majadiliano yao katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi milioni kumi na tatu wanaotaka kuona mabadiliko makubwa baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe isiyokuwa na mashiko wala mguso!

Wimbo wa taifa la Sudan ya Kusini ndio umekuwa mwongozo na rejea katika mafungo ya siku mbili kwa viongozi wa Sudan ya Kusini. Familia ya Mungu inatamani kuona Sudan ikiwa huru na wakati huo, ikiwa imesimikwa katika umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kutambua kwamba, hata tofauti zao msingi si sababu ya kuwasambaratisha na kuwatumbukiza katika maafa ya vita, njaa na umaskini wa hali na kipato! Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si vinginevyo!

Hawa ni watu ambao tangu mwaka 2011 walitamani kuona cheche za matumaini, ustawi na maendeleo, lakini kwa bahati mbaya, wakajikuta wakitumbukia na kuzama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kunako mwaka 2013. Wananchi milioni saba wanateseka kwa njaa na utapiamlo wa kutisha; watoto wengi hawana tena fursa ya kupata elimu kutokana na vita na mashambulizi ya mara ya kwa mara na kwamba, kuna wananchi milioni nne wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuishi kama wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum hata ndani ya nchi yao wenyewe!

Viongozi wa Serikali na Kidini nchini Sudan ya Kusini, baada ya kuhitimisha sala, tafakari na mafungo yao ya siku mbili, wamezawadiwa Biblia iliyotiwa sahihi na Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu Justin Welby pamoja na Mchungaji John Calmers, ambaye amewahi kuwa Mratibu wa Kanisa la Scotland. Ujumbe: Tafuteni kile kinachowaunganisha. Shindeni kile kinachowatenganisha!

Mateso: Sudan ya Kusini
12 April 2019, 11:15