Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Siku ya Vijana Kijimbo: Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma ya Upendo: Ijumaa Kuu: Mateso & Kifo: Kesha la Pasaka! Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Siku ya Vijana Kijimbo: Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma ya Upendo: Ijumaa Kuu: Mateso & Kifo: Kesha la Pasaka! 

Maadhimisho ya Juma Kuu 2019

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu ni kijana milele; wao ni leo ya Mungu; mbiu kwa vijana ni kwamba, Mungu ni upendo; wanapaswa kukua na kukomaa; kwa kukita mizizi katika mambo msingi; vijana ni wadau wa maisha yao, wajisadake bila kujibakiza pamoja na kutambua miito yao!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio ambalo linaendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, kwa kuona tena ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwamba, Mwaka huu 2019 Siku ya Vijana inaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo na maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2022 yatafanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" anagusia nafasi ya vijana katika Maandiko Matakatifu na kuwakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu ni kijana milele yote.

Vijana ni leo ya Mungu, kumbe wanapaswa kuchakarika sana. Mbiu kuu kwa vijana ni kwamba, Mungu ni upendo, ili kuufikia upendo huu, vijana hawana budi kujikita katika malezi na makuzi makini, kwa kuzamisha mizizi ya maisha yao katika mambo msingi. Kanisa litaendelea kuwasindikiza, lakini vijana wenyewe ndio wadau wa malezi na makuzi yao, kumbe wanapaswa kujitosa bila ya kujibakiza katika kufanya kazi na kwamba, wanapaswa kutambua na kuambata miito yao. Padre Alcuin Nyirenda OSB katika tafakari hii, anachambua kwa kina na mapana maadhimisho ya Juma kuu kwa Mwaka 2019, akiwabeba vijana wa kizazi kipya wanaoadhimisha Siku yao kwa ngazi ya Kijimbo, huku anawakumbusha kwamba, ujana mali, fainali uzeeeni! Eti ujana unaishia .....!!

Baada ya mazoezi magumu ya gym unategemea kuona mabadiliko. Mathalani kama uliwania kupunguza unene au uzito utaenda kujipima kwenye mizani. Kama ni udhaifu wa moyo na mapafu utaenda kwenye vipimo husika ili kujiridhisha. Iwe iweje, baada ya gym unashauriwa kuendelea na mazoezi ili kudumisha hali hiyo au kuanza tena awamu nyingine ya gym.  Ndugu zangu zimepita wiki tano kamili kutoka pale ulipoanza zoezi kuu la safari hii, ya mateso ya Yesu niliyoiita gym kwa takribani siku arobaini. Katika kipindi hiki tumefanya gym pamoja na Yesu mwenyewe. Aidha, Yesu ametufundisha kimatendo namna ya kusali na ya kushinda vishawishi vya ulimwengu.

Kuanzia Jumapili ya Matawi, tunaingia wiki pekee isiyofanana kamwe na wiki nyingine katika mwaka. Wiki hii tutamshuhudia Yesu akiingia kwenye mateso (mazoezi) makali zaidi. Aidha katika wiki hii tutabahatika kuadhimisha mafumbo makuu aliyotuachia siku ya Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Mkesha wa Pasaka. Kwa hiyo wiki hii tunaalikwa kukaa mkao wa kutulia kusali na kutathmini mateso ya Yesu ili kunufaika nayo kibinafsi na kuiga mfano wa kuufuata baadaye. Kwa siku mbili tu katika mwaka, Dominika ya Matawi na Ijumaa kuu tunabahatika kusimuliwa mateso ya Yesu kwa njia ya tamthlia yaani kwa maigizo. Wengine wanayaangalia maigizo hayo katika filamu ya kutisha ya Mel Gibson. Ama kweli mateso ya Yesu ni kama mchezo wa kuigiza lakini kuna mtu ameteseka hadi kufa.

Ndugu zangu ukiyafuatilia kwa dhati mateso hayo ya Yesu hata kabla ya kushikwa kwake bustanini utaona yanazidiana kwa uzito kutoka hatua moja hadi nyingine hadi anakufa Msalabani. Aidha ukiyafuatilia hatua kwa hatua utagundua jinsi yanavyoongea nawe moja kwa moja na yanavyogusa maisha yako ya kila siku. Hebu tuziangalie hatua chache za mateso aliyoyapitia Yesu: Mosi, Yesu Bustanini Getsemani. Yesu alipokuwa katika bustani ya mizeituni kule Getsemani aliteseka sana kabla hata ya mateso yaliyokuwa yanamsubiri. Kule bustanini Yesu alijawa na msongo mkali sana wa mawazo hadi likamtoka jasho la damu. “Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki (uchungu mkali) akazidi kuomba; hari (jasho) lake likawa kama matone ya damu yakidondoka katika nchi.” (Lk. 22:23). Hapa huwezi kuamini jinsi gani Yesu aliteseka akifikiria kifo kilichokuwa kinamsubiri siku ya pili yake tu, tena kifo cha fedheha na mateso makali.

Ndugu yangu, hii ndiyo hali halisi inayoweza kumtokea binadamu yeyote yule anapokabiliwa na matatizo mazito ya maisha hususani misiba. Hapo binadamu anawaza na kuwazua bila majibu hadi jasho linamtoka. Hebu fikiria kidogo matatizo yako yaliyoweza kukutoa jasho au yanayokutoa jasho. Licha ya kutokwa jasho la damu, Yesu anaonesha zaidi ukali wa mateso makali anayoyasikia kwa maneno anaposema: “Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa” (Mt. 26:38; Mk. 14:33). Yawezekana hata wewe umewahi kupata msongo wa mawazo katika matatizo yaliyokupata kiasi hata cha kusema “Afadhali kufa kuliko mateso ninayoyapata.” Usongo wa mawazo kwa Yesu ulikuwa mzito kiasi cha kuwaalika wafuasi wake wakeshe naye akawaambia: “kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.” Mara ngapi nawe umepita kutafuta vitulizo kwa wengine wakati wa matatizo yako. Yesu hakuishia hapo tu.

Uchungu ulipomzidi akafikia hatua hata ya kumwomba Baba yake akiondolee mbali kikombe kile cha mateso makali. Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke.” (Mt. 26:39; 14:34). Hivi ndivyo watu wanavyoweza kupatwa na mateso makali wanalalamika hadi wakafikia kumlaumu Mungu. Lakini Yesu hakulalamika bali alisali na kuita “Baba”. Jambo la kushangaza akiwa katika kuomba na kusali hivyo, akashusha pumzi na akaona anapata nguvu ghafla na kusema: “Walakini Baba, si kama nitakavyo mimi bali utakavyo wewe.” (Mt 26:39; Mk 14:36; Lk 22:42).  Hapa unaona jinsi Yesu aliyejisikia uchungu na kupondeka sana kiasi cha kusema niondolee mbali kikombe hiki. Sasa mara anaibuka kutoka hali hiyo hadi kufikia kusema sivyo nitakavyo mimi bali mapenzi yako yatimizwe. Ni sawa na kusema: “Nimepokea niko tayari.” Hapa unashuhudia mwenyewe maajabu ya sala ukiwa katika mateso na kukata tamaa. Sala inakuimarisha na kukupatia nguvu katika mateso na kukufanya usimame tena na kuendelea mbele kuyakabili mateso yako. Jinsi sala ilivyomsaidia Yesu kukabili mateso yake ndivyo inavyoweza kutusaidia hata sis. Kwa hiyo hapa umeshuhudia faidia ya gym kwa Yesu inavyoweza kuwa mfano kwetu sisi. Ndugu yangu ukiwa na tatizo lolote kimbilia sala.

Pili, tukiwa bado bustani ya Getsemani tukishuhudia patashika ya kumkamata Yesu.  Tunawaona wafuasi wote wanatimua mbinu na kusambaratika. Ama kweli “aungurumapo simba mcheza nani?” Katika patashika ile kulikuwa pia na kijana mmoja aliyekuwa anakifuatilia kwa karibu kituko kile kuanzia pale Yesu na mitume walipokuwa kwenye karamu ya mwisho. Nadhani kijana huyu alisikia jinsi Yesu alivyokuwa anaongea na mitume wake, na yawezekana alisikia pia minong’ono ya watu wakizungumza kwamba hawana uhakika na kitakachomtokea Yesu Pasaka hii. Basi baada ya mlo wa jioni, mitume walipoondoka karamuni na kuelekea kwenye bustani ya Getsemani akawafuata ili ashuhudie hatima yake. Kwa vile ilikuwa jioni, kijana alikuwa amejifunga (kikwinda) shuka kiunoni bila nguo nyingine zaidi. Alipoona vurugu la kumshika Yesu limepamba moto na wafuasi wake wanatimua mbio, naye akaona “changu nini”, akaamua kutoroka.

Kumbe, kwa bahati mbaya mtu mmoja kwenye kundi la waliofika kumshika Yesu akamng’aza kijana huyu akakishika “kikwinda” kile kwa nguvu. Kijana alipoona anazidiwa, akaamua kukiachia kikwinda kile “potelea mbali.”  akatoroka uchi wa nyama kama tunavyosoma: “Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.” (Mark 14:51-52). Hatuambiwi kijana yule alikuwa nani, lakini maoni ya wengi wanasema kwamba huyo alikuwa Marko, kwa sababu kituko hiki kinasimuliwa katika Injili hii tu. Inaelezwa pia kwamba, huu ulikuwa mtindo wa uandishi wa vitabu wakati huo jinsi mtunzi alivyotilia sahihi utunzi wake. Yaani, kuchomekea kituko cha pekee katika mazingira tatanishi.

Hapa mtunzi Marko amechomekea kituko cha kutoroka uchi katika mazingira ya kutisha na kuwafanya watu wacheke kidogo. Lakini tunachokiona hapa ni kwamba kijana huyu hakumtoroka Yesu moja kwa moja kwani baadaye alirudi na kuiandika Injili hii. Yaani, maisha yake ya awali (ya ujana) alimkimbia Yesu, lakini baadaye akamrudia na kumkimbilia Yesu tena kwa karibu na undani zaidi hata kufikia hatua ya kumwandikia Habari njema. Aidha, kwa sababu Injili ya Marko iliandikwa Roma, inawezekana pia kwamba kati ya Wainjili wale wanne walioandika maisha ya Yesu mmojawapo ndiye aliyechanganyikiwa na akaona bora kutoroka. Lakini baadaye alijirudi na kwenda Roma alikokutana na kumhoji Petro habari za Yesu na kuiandika Injili hiyo akiwa hukohuko Roma.

Kituko hiki cha Marko, kinatufundisha sisi sote kutokukata tamaa ya maisha bali daima tutumaini kwamba wale wote ambao zamani waliolikimbia kanisa au hata wale wanaomkimbia leo kwa hoja mbalimbali ikiwa ni pamoja na makwazo, lakini wanaweza wakarudia tena kanisani. Aidha endapo katika Injili halitajwi jina la mtu bali kinatajwa kijina au sifa, kama vile mama, au baba, kijana au rika basi inamhusu kila mmoja wa rika hiyo. Katika kipengele cha leo, kwa vile jina la kijana halijatajwa, basi kituko hiki kinawahusu vijana wote wa kizazi kipya. Vijana wa leo wanayo sifa ya kudadisi na ya kuthubutu kufuatilia na kushabikia mambo mapya na ya kijasiri ya ulimwenguni. Wanatumia muda mrefu kutafuta mambo ya pekee katika internet na kujasiri kuyafanya. Hapa wanaacha kufuata maadili mema ya dini na mila zao na kuyafuata. Wanaishia kumwacha Kristo na kuingia mitaani na kufuata mikumbo na mitindo ya ulimwengu mamboleo. Hususani, michezo ya mipira, unywaji wa pombe kali, ubugiaji wa unga, uendeshaji wa biashara haramu, kuzamia vikundi haramu, nk.

Vijana wanaweza hata kudiriki kuacha dini yako katoliki na kuingia dhehebu lolote la kimamboleo linalovutia kwa nyimbo na mitindo ya kisasa au la mbwembwe na mazingaombwe. Mambo yanapowachachia sehemu moja wanatoroka bila mpangilio na kuingia sehemu nyingine. Vijana kama hao ndiyo akina Marko. Wakumbuke kwamba Kristo hajawakatia tamaa, kwani anatambua kwamba watakapopigwa baridi kwa sababu walikimbia uchi watarudi wenyewe kama mwana mpotevu naye Yesu kama baba mwema yuko tayari kuwapokea wakati wowote ule na kuwavika tena nguo. Kadhalika sisi sote tufikirishwe na kijana huko Marko kwamba kila tunapomkimbia Yesu, Yeye anatusubiri tumrudie katika sakramenti ya upatanisho (kitubio).

Tatu, hatua ya kupigwa na kujeruhiwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunashtuka sana tunapoona jinsi Yesu alivyoumizwa na kujaa majeraha mwili mzima. Tunashtuka sana kusikia alivyochambwa matusi ya kila aina. Hata kesi yake iliendeshwa kinamna namna tu tena kwa muda mfupi sana bila kukaa mahabusu na haikusubiriwa kukamilisha upelelezi. Aidha kesi ya Kristo Yesu haikuwa na wakili au mtetezi kwa sababu mashahidi wote walitoroka. Yesu alianza kuhojiwa katika mahakama ya kidini na viongozi wenye chuki binafsi. Maoni yao ya jumla bila mjadala ni kwamba Yesu anastahili kunyongwa hadi kufa.

Lakini kwa vile waliogopa kuchukua mamlaka mkononi ya kuua wakayapeleka mapendekezo yao kwa mahakama ya dola ya Kirumi chini ya Pilato aliyekuwa mkuu wa mkoa wakati ule. Huko Yesu alifanyiwa dhihaka na fedheha za kila aina, akaveshwa kichwani taji la miba na hatimaye akahukumiwa kufa. Akabebeshwa msalaba. Alipofika pahala pa kusulibiwa akavuliwa nguo zote kisha wakamsulibisha kwa kumpigilia misumari msalabani. Hata alipokuwa msalabani aliendelea kuchambwa matusi. Hayo yote alifanyiwa kwa ajili yetu sisi, ikiwa na lengo la kukifunga kabisa kinywa cha dhambi kisiwe tena na kauli ya mwisho. Yaani kila mara pale Mungu Baba anapoziona dhambi, basi amwangalie Mwanaye aliyezifia Msalabani na hapohapo atusamehe.

Ndivyo tunavyotulizwa na utangulizi ya sala ya Ekaristi ya leo isemayo: “Yeye, ingawa hakuwa na kosa, alikubali kuteswa na kuhukumiwa pasipo haki kwa ajili ya wakosefu. Amefuta dhambi zetu kwa kifo chake na kutufanya wenye haki kwa ufufuko wake.” Hii ndiyo faida ya gym ya Yesu, kwa sababu inabeba dhambi zetu. Kilichobaki kwetu sisi ni kujishikilia kwa dhati katika mateso yake kama tunavyoshauriwa kwamba: “Ukibebwa jishikilie.” Yaani tushikize mateso yetu kwenye mateso ya Yesu naye atabeba yote. Hii ndiyo faida ya kufanya gym au kuteseka pamoja na Yesu.

Nne, kifo cha Yesu. Yesu alipokufa pazia la hekalu lilichanika kutoka juu hadi chini: “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili kutoka juu hata chini.” (Mt 27:51; Mk 15:38; Lk  23:45). Pazia lile lilikuwa kama kiambaza kilichotenga sehemu ya kukaa na kusali waumini wa kawaida na sehemu ya Patakatifu-takatifu palipokuwa makao ya Mungu hekaluni. Pahala hapo hakuruhusiwa kuingia mtu yeyote zaidi ya kuhani mkuu, naye aliingia mara moja tu kwa mwaka.  Yesu anapokufa pazia hilo linachanika vipande viwili. Hali inayoonesha kwamba kifo cha Yesu kimetufungua njia ya kuingia moja kwa moja pahala anapokaa Mungu.

Aidha pazia lile lilichanika kutoka juu hadi chini na siyo kutoka chini hadi juu ili kutuonesha kwamba Mungu aliye juu ndiye aliyesababisha kuchanika kwa pazia hilo kutoka juu. Lakini kwa vyovyote kwetu sisi haimaanishi tu kuingia kanisani, bali kama isemavyo barua kwa Waebrania kwamba sasa sisi tunaweza kuingia patakatifu pa patakatifu pa Mungu kwa njia ya Mwili na Damu azizi ya Kristo yaani kwa njia ya Ekaristi Takatifu: “Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tuna ujasiri wa njia ya kuingia katika mahali patakatifu kwa damu ya Yesu, aliyotuzindulia kuwa njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani, mwili wake, na kwa kuwa tuna kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu.” (Heb 10:19-20). Sasa sisi tunaingia patakatifu pa Mungu tunapopokea mwili na damu ya Yesu katika Ekaristi takatifu. Tunaingia patakatifu-takatifu wakati wa Misa tunapoadhimisha jinsi Yesu alivyotoa mwili na damu yake kwa ajili yetu Kalvari. Hiyo ndiyo faida ya Kwaresima na ya kufanya mazoezi pamoja na Yesu. Tumsifu Yesu Kristo!

 

13 April 2019, 11:37