Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin: Uhuru wa kidini ni sehemu ya vinasaba vya utu, heshima na haki msingi za kibinadamu! Kardinali Pietro Parolin: Uhuru wa kidini ni sehemu ya vinasaba vya utu, heshima na haki msingi za kibinadamu!  (AFP or licensors)

Uhuru wa kidini ni sehemu ya vinasaba vya utu na haki msingi!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na Jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayojikita katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi duniani!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano, tarehe 3 Aprili 2019 ameshiriki katika hitimisho la kongamano la kimataifa kuhusu uhuru wa kidini, lililoandaliwa na Ubalozi wa Marekani mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tusimame kidete Kulinda Uhuru wa Kidini”. Kardinali Parolina anasema, takwimu za Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, kuna watu wengi wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao, wakiwemo Wakristo, hali inayowanyima haki zao msingi. Kimsingi hali ya uhuru wa kidini kimataifa inaendelea kuporomoka kila kukicha!

Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kuungama na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Parolin anakaza kusema, haitoshi kusimama kidete kulinda uhuru wa kidini, bali kuna haja ya kujenga na kudumisha ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza na kudumisha uhuru wa kidini. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ushirikiano na mafungamano ya kijamii ni njia muafaka kabisa ya kupambana na ukosefu wa uhuru wa kidini sehemu mbali mbali za dunia! Huu ni wakati wa kuachana na maneno matupu na kuanza kutenda.

Kardinali Parolin anasema, uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu; hii ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inakita mizizi yake katika asili ya binadamu. Viongozi wa Serikali wanalo jukumu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanalinda uhuru wa kidini, kwa sababu hii ni dhamana yao kwani wao si asili ya uhuru wa kidini. Kulinda uhuru wa kidini na ukomo wake ni tema mbili zinazohusiana na binadamu! Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwani binadamu ni dira na mwongozo wa Sheria za Kimataifa na haki msingi za binadamu!

Uhuru wa kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu inayofumbatwa katika utu na heshima yak. Ni mchakato unaomwezesha binadamu kutafuta na kuumbata ukweli katika maisha yake sanjari na kuendeleza nguvu na karama alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Uhuru wa kidini unamwezesha mtu kuishi katika uhuru kamili pamoja na kupata fursa ya kushuhudia imani yake katika matendo katika hali ya faragha au katika maisha ya hadhara.

Hii ndiyo changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo unaokumbwa na  nyanyaso na dhuluma kutokana na kukosekana kwa maridhiano kati ya watu! Ukosefu wa uhuru wa kidini unapaswa kuangaliwa katika mapana yake, kwani kuna baadhi ya nchi ambamo uhuru wa kidini unatumiwa kuwagawa watu kwa misingi ya imani yao! Hapa kuna raia wa daraja la kwanza na raia wa daraja la pili. Hali hii inawakumba Wakristo zaidi. Kuna wakati mwingine, mashambulizi ya kidini yanafumbatwa katika itikadi za kisiasa, kiasi cha kusahau haki msingi za binadamu!

Kardinali Parolin anasikitika kusema, katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka haki mpya za binadamu, ambazo zinasababisha kinzani kuhusu uhuru wa kuabudu na haki ya mtu kuishi. Uhuru wa kidini ni sehemu ya maisha ya binadamu, bila ya kuwa na mwelekeo huu, Jumuiya ya Kimataifa daima itajikuta ikiogelea katika migogoro mbali mbali. Waamini wana haki ya kumheshimu na kumwabudu Mwenyezi Mungu aliye asili ya uhai, uhuru na furaha ya kweli. Ni kutokana na muktadha huu kwamba, Vatican itaendelea kusimama kidete kukuza na kudumisha uhuru wa kidini unaofumbatwa katika uhuru wa dhamiri, utu na heshima ya binadamu.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu ilitiwa sahihi kati ya Baba Mtakatifu Francisko Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa Majadiliano ya Kidini Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, hapo tarehe 4 Februari 2019. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Hati hii ni matunda ya uvumilivu, busara na hekima inayopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kudumisha amani duniani! Kardinali Parolin, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujisomea Hati hii, ili kupyaisha tena umuhimu wa maisha ya kiroho miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; kwa kujikita katika maadili na utu wema mintarafu mafundisho ya dini mbali mbali duniani. Ni kwa njia hii, tabia za uchoyo na ubinafsi, kinzani na vita; misimamo mikali ya kidini na kiimani vitaweza kudhibitiwa!

Kardinali Parolin: Uhuru wa kidini
04 April 2019, 16:09