Tafuta

Caritas Internationalis: Ujumbe wa Pasaka 2019: Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaoteseka! Caritas Internationalis: Ujumbe wa Pasaka 2019: Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaoteseka! 

PASAKA YA BWANA 2019: Ujumbe wa Caritas: Upendo na Ukarimu

Kardinali Tagle anasema, Caritas Internatinalis inalotoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kila mwamini anaweza kuchangia hata kwa kile kidogo alicho nacho kwa ajili ya kuenzi huduma inayotolewa na Caritas. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika huduma ya upendo.

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, katika ujumbe wake wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2019 anakazia: fadhila ya upendo, ukarimu na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Leo hii kuna watu wanakabiliwa na maafa pamoja na majanga makubwa katika maisha yao; vita na vitendo vya kigaidi vinaendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Katika hali na mazingira kama haya, watu wengi wanaanza kujiuliza, Je, kweli Mungu yupo? Mbona vitendo vyote hivi ni kinyume kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake? Kardinali Luis Tagle anawakumbusha wale wote waliokata tamaa na kusongwa na mawazo, ile sala ya Kristo Yesu pale Msalabani “Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?” Upendo ulijificha wapi wakati Yesu alipokuwa anahukumiwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani?

Mwanadamu katika safari ya maisha yake anaweza kukumbana na ukakasi wa imani, hasa pale ambapo ukosefu wa haki msingi za binadamu unatawala na kushamiri! Matukio yanayoendelea kushamiri yanaonesha kana kwamba, ulimwengu umekumbwa na giza nene! Imekuwaje, watoto huko Sri Lanka, baada tu ya kupokea Komunio ya Kwanza, wakauwawa kwa bomu la kujitosa mhanga? Kardinali Luis Tagle katika ujumbe wake wa Pasaka anawaalika waamini kuwa na jicho la imani na kuangalia jinsi ambavyo upendo unamwilishwa hatua kwa hatua katika maisha ya watu, hata kama ni “kiduchu”

Kristo Yesu alipokuwa kwenye Njia ya Msalaba pamoja na chuki, uhasama na mateso yaliyomsibu, lakini bado aliweza kuonja uwepo mwanana wa Mama yake, Bikira Maria aliyemfuata kimya kimya! Yule mwanafunzi aliyempenda, akadiriki hata kusimama chini ya Msalaba bila kuwasahau wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumsikitikia Yesu kwa mateso makali aliyokuwa anakabiliana nayo! Zote hizi zilikuwa ni cheche za upendo, zilizomfikia hata Yusufu wa Arimathaya akapiga moyo konde na kwenda moja kwa moja kwa Pilato kuomba mwili wa Yesu ili akauzike. Nikodemo akaleta mchanganyiko wa manemane kuuandaa mwili wa Yesu kwa maziko!

Wanawake wakashuhudia mahali alipozikwa na asubuhi na mapema siku ya kwanza ya Juma, wakawa wakwanza kufika na hatimaye, kutangaza na kushuhudia kwamba, Yesu amefufuka kweli kweli! Hata katika ugumu wa moyo, Pilato hakuona hatia kwa Yesu, akataka kumfungulia, lakini aliogopa maneno na macho ya watu! Hizi ni cheche za upendo na ukarimu zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu ambamo umegubikwa na giza na uvunjifu wa haki msingi za binadamu! Mateso na kifo cha Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na sadaka yake Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!

Hii ndiyo dhamana na utume unaotekelezwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, yaani Caritas Internationalis. Ni Shirika linalotoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kila mwamini anaweza kuchangia hata kwa kile kidogo alicho nacho kwa ajili ya kuenzi huduma inayotolewa na Caritas. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika huduma ya upendo.

Caritas inawapongeza wale wote walioshiriki kampeni ya Caritas Internationalis “Share the journey” yaani “Shiriki safari” kama kielelezo cha dhati kabisa cha kutaka kutembea kwa pamoja, ili kufahamiana na hatimaye, kuondoa chuki na uhasama dhidi ya wakimbizi na wahamiaji. Nguvu ya upendo wa Kristo Mfufuka iwafikie wananchi sehemu mbali mbali za dunia wanaoteseka kutokana na vita, majanga asilia, vitendo vya kigaidi. Bila kuwasahau wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Caritas ni upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ni sadaka na majitoleo, kwa ajili ya kuwasha cheche za upendo kwa watu wanaoteseka!

Caritas: Upendo
23 April 2019, 09:56