Vatican News
Juma Kuu 2019: Mchango wa Ijumaa Kuu: Kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa na Nchi Takatifu anasema Kardinali Leonardo Sandri Juma Kuu 2019: Mchango wa Ijumaa Kuu: Kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa na Nchi Takatifu anasema Kardinali Leonardo Sandri 

Ijumaa kuu 2019: Mchango wa Umoja na Mshikamano na Nchi Takatifu

Kardinali Leonardo Sandri, anawaalika waamini kuonesha umoja, mshikamano na upendo unaomwilishwa katika Injili ya huduma kwa Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, Cyprus, Misri, Eritrea na Uturuki. Huu ndio ushuhuda wa imani unaowasaidia kumsindikiza Kristo Yesu kwa njia ya imani anapoingia katika mateso, kifo na hatimaye ufufufuko wake kadiri ya Maandiko Matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu unalenga kukuza na kudumisha amani katika maeneo matakatifu, kwa kuwawezesha Wakristo kuendelea kuwa ni vyombo vinavyotumiwa na Kristo mwenyewe kwa ajili ya mafao ya eneo la Mashariki ya Kati. Ni mchango unaosaidia utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu na fungamani. Huu ni ushuhuda wa umoja na Injili ya upendo, inayowaunganisha na kuwawajibisha Wakristo wote pamoja na kuwasaidia Wakristo kuendelea kubaki huko Mashariki ya Kati licha ya matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa Kanisa katika kukuza na kudumisha: umoja, upendo na haki msingi za binadamu.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika ujumbe wake kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa mwaka 2019 anawaalika, kuonesha umoja, mshikamano na upendo unaomwilishwa katika Injili ya huduma kwa Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, Cyprus, Misri, Eritrea na Uturuki. Huu ndio ushuhuda wa imani unaowasaidia kumsindikiza Kristo Yesu kwa njia ya imani anapoingia Yerusalemu kwa shangwe, tayari kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anawahamasisha waamini kumfuasa Kristo katika Njia yake ya mateso, kwa kuondokana na ubinafsi, uchoyo na hali ya kutaka kujitafuta wenyewe na hivyo kuwa tayari kutoka ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kuteseka, kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza alitembelea Nchi Takatifu Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo. Katika Wosia wake wa kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu”  uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, ukawa ni chanzo cha Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu.  Mtakatifu Paulo VI alikazia sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi.

Huu ndio ukawa mwanzo wa kukusanya Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, kama alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano. Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Itakumbukwa kwamba, kuna watu wanalazimika kuyakimbia makazi na nchi zao kutokana na  dhuluma za kidini.

Kanisa linapenda kuwahimiza Wakristo kuendelea kubaki huko Mashariki ya Kati, kwa kuonja na kudumisha mshikamano wa umoja na upendo kutoka kwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni ushuhuda unaosimikwa katika mshikamano wa sala, hali na mali pamoja na hija zinazofanywa na Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mwaka 2019, taarifa zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la Wakristo wanaotoka China, Indonesia, Sri Lanka, Ufilippini na hata katika baadhi ya Nchi za Kiafrika, Tanzania ikiwemo, ingawa haivumi sana! Huu ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Ijumaa Kuu 2019: Kard. Sandri
17 April 2019, 08:00