Tafuta

Vatican News
Vatican inashiriki Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa Mazingira "Expo Bejing 2019" kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kitamaduni! Vatican inashiriki Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa Mazingira "Expo Bejing 2019" kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kitamaduni!  (AFP or licensors)

Expo- Bejing 2019: Vatican inashiriki Onesho la Kilimo cha Maua!

Zaidi ya nchi 110 zinashiriki katika Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa Mazingira, nchini China. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano yanayoendelea kati ya Vatican na Serikali ya China. Tarehe 14 Septemba 2019 itakuwa ni Siku ya Vatican Kitaifa. Vatican imeandaa kongamano kuhusu wongofu wa kiekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, Vatican imekubali mwaliko wa Serikali ya China wa kushiriki katika “Expo Bejing 2019” yaani “Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa mazingira”. Onesho hili linafunguliwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019 kwa ushiriki wa Kardinali Ravasi na Askofu mkuu Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na litahitimishwa hapo tarehe 7 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ishi kijani, Ishi vizuri zaidi”.

Taarifa zinaonesha kwamba, zaidi ya nchi 110 zinashiriki katika Onesho hili huko Bejing, nchini China. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano yanayoendelea kati ya Vatican na Serikali ya China. Tarehe 14 Septemba 2019 itakuwa ni Siku ya Vatican Kitaifa. Hapa Vatican imeandaa kongamano kuhusu wongofu wa kiekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu yanayozingatia kwa namna ya pekee kabisa: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hii ni nafasi pia kwa Vatican kuendeleza Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu muhimu sana ya kazi ya uumbaji kama yanavyofafanuliwa katika Waraka wake wa kitume wa “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.  Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini. Anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Baba Mtakatifu anasema, utunzaji bora wa mazingira unakita mizizi yake katika wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli, mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Dhamana hii ya kijamii, inapania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Itakumbukwa kwamba, Septemba 2018, Vatican na China vilikubaliana kuhusu uteuzi wa Maaskofu, dhamana inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Vatican imewekeza kiasi cha Euro milioni moja sawa na Dola za Kimarekani milioni 1.13.

Kardinali Gianfranco Ravasi anakaza kusema, huu ni uwekezaji utakao zaa matunda kwa wakati wake, kwani kwa sasa mchakato wa majadiliano kati ya Vatican na China unajikita zaidi katika utamaduni na kwa siku za mbeleni, China inapenda kuendeleza majadiliano haya katika masuala ya sanaa, utamaduni pamoja na tafiti za kisayansi. Kardinali Gianfranco Ravasi pamoja na Monsinyo Tomasz Trafny, Afisa mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Utamaduni ndio waliopewa dhamana na Sekretarieti kuu ya Vatican kushughulikia maandalizi yote ya ushiriki wa Vatican kwenye Onesho la Expo Bejing 2019. Banda la Vatican katika Onesho hili limewekewa: Kisima cha maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Kuna nyumba ya kijani kwa ajili ya kukuzia mimea, kuna bustani ya matunda yanayovutia, zawadi kutoka Uholanzi.

Kuna nyaraka za kale kutoka Maktaba kuu ya Kitume ya Vatican, “Vatican Library” kuhusu matumizi ya miti shamba katika tiba pamoja na virutubisho vyake kama yanavyofafanuliwa kwenye Kitabu cha “Herbarium” nyenzo muhimu sana katika tiba na elimu ya dawa. Vitabu vingine ni “Dioscorides: Materia medica” kilichotungwa karne ya kwanza baada ya Kristo! Kuna mchoro wa Adamu na Hawa, uliochorwa na Peter Wenzel kunako karne ya 19, kutoka Jumba la Makumbusho ya Vatican. Umuhimu wa mwanga katika maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili, umezingatiwa katika Onesho la Expo Bejing 2019. Umuhimu wake, unapata chimbuko kutoka katika Maandiko Matakatifu, kwenye kazi ya Uumbaji.

Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, Banda la Vatican katika Onesho la Expo Bejing 2019 kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 7 Oktoba 2019 ni matunda ya ushirikiano na mshikamano kutoka Maktaba Kuu ya Kitume ya Vatican, Jumba la makumbusho la Vatican, Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Ubalozi wa China nchini Italia, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO pamoja na Uholanzi. Kuna watu wengi wamejisadaka ili kukamilisha Onesho hili kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kitamaduni kati ya Vatican na China.

Bejing Expo 2019
27 April 2019, 09:01