Tafuta

Vatican News
Ijumaa Kuu: Padre Raniero Cantalemessa: Tafakari ya Ijumaa kuu: Mateso ya Kristo yanayovyoendelea kufunuliwa katika maisha ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Ijumaa Kuu: Padre Raniero Cantalemessa: Tafakari ya Ijumaa kuu: Mateso ya Kristo yanayovyoendelea kufunuliwa katika maisha ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii  (Vatican Media)

Ijumaa kuu 2019: Kristo Yesu utambulisho wa mateso ya watu!

Kristo Yesu, Mteule na Mtakatifu wa Mungu, kwa kumwaga Damu yake Azizi, amekomboa mwandamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti! Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kama ilivyoandikwa! Ni mshindi, Hakimu mwenye haki, Jiwe kuu la msingi. Kwa kufufuka kwake, amekuwa haki kwa wasiokuwa na haki, chemchemi ya utu na matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

IJUMAA KUU, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Aprili 2019, ameongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mahubiri ya Ijumaa kuu yametolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa!

Tafakari hii imeongozwa na kauli mbiu “Alidharauliwa na kukataliwa na watu”. Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko. Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu! Huu ndio ufunuo wa Uso wa Yesu wa Nazareth, anaendelea kujionesha kati ya maskini, wanaodharauliwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao wanageuziwa kisogo! Tangu mwanzo, maisha ya Kristo Yesu yamekuwa ni kama Njia ya Msalaba, kielelezo cha mshikamano na maskini! Kristo Yesu alizaliwa Pangoni, mahali pa kulishia wanyama kwa sababu, hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.

Yesu alipotolewa Hekaluni, wazazi wake walitoa huwa wawili na makinda ya njiwa wawili, alama ya ufukara wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Katika maisha yake ya hadhara, hakuwa hata na mahali pa kulaza kichwa chake. Wakati wa hukumu na hatimaye mateso yake, Yesu alivikwa taji ya miiba kichwani, akavalishwa joho la rangi nyekundu, mikono na miguu yake ikafungwa imara kwa kamba ngumu, wakamwekea mwanzi katika mkono wake wa kuume na kuanza kumdhihaki na kumtesa.

Pontio Pilato baada ya kuona kwamba, Kristo Yesu alikuwa ameteswa vya kutosha akatoka nje na kuwaambia watu “Ecce homo” yaani “Tazameni mtu huyu”. Hata leo hii kuna maelfu ya watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa! Ni watu wanaokataliwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Kristo Yesu ni kiongozi ambaye ameacha historia kubwa katika maisha ya watu kutoka katika kila taifa, lugha, jamaa na dini na kwamba, watu wengi wanaweza kujitambulisha naye! Kristo Yesu ni mfano wa watumwa waliodharauliwa na kunyanyasika, lakini, Yesu katika maisha na utume wake, akawarejeshea tena utu na heshima yao kama wana wa Mungu, ni Kristo Yesu anayejua hata leo hii mateso ya wakimbizi  na wahamiaji wanaotenganishwa na familia zao.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, mateso na kifo cha Kristo Yesu ni amana, utajiri na Fumbo la Ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ikumbukwe kwamba, Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu! Kristo Yesu, Mteule na Mtakatifu wa Mungu, kwa kumwaga Damu yake Azizi, amekomboa mwandamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti! Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, aliyeteswa, akafa, amefufuka kama ilivyoandikwa! Kristo Yesu ni mshindi; ni Hakimu mwenye haki, Jiwe kuu la msingi lililokataliwa na waashi. Kwa kufufuka kwake, Yesu amekuwa haki kwa wasiokuwa na haki, chemchemi ya utu, heshima na matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Kanisa la mwanzo, liliadhimisha: Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Kuu katika tukio moja linalodhihirisha Pasaka ya Bwana, kama ilivyokuwa kwa Wayahudi “Passover”, Pesach”, yaani “Kupita juu”. Kielelezo cha ukombozi wa Waisraeli kutoka utumwani, kuelekea kwenye uhuru kamili; Ushuhuda wa Kristo kutoka hapa ulimwenguni kurudi kwa Baba yake wa mbinguni. Kwa waamini hili ni tendo la kutoka katika utumwa wa dhambi na kuanza kutembea katika mwanga na neema ya Kristo Mfufuka. Yesu anakuwa ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega pamoja na hatima ya maisha mwanadamu.

Katika muktadha wa matukio yote haya, Pasaka kwa hakika ni Sherehe ya maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo! Msalaba ni alama ya nguvu ya ushindi; upendo na wokovu; msamaha na upatanisho; umoja na mshikamano wa dhati. Huu ni ushindi dhidi ya utamaduni wa kifo, dhambi na ukatili; ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kumkimbilia Mwenyezi Mungu ili kupata wokovu! Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza na kujipoteza mwenyewe?” Lk. 9:25.

Mama Kanisa amepewa dhamana na wajibu wa kusimama na kuambatana na maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linapaswa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti; mtetezi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linapaswa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata mahitaji yao msingi kama vile: chakula, maji na malazi bora. Haya ni mambo mazito yanayowagusa waamini wa dini mbali mbali duniani! Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa anahitimisha mahubiri yake Ijumaa kuu kwa kurejea tena kwenye Kitabu cha Nabii Isaya anayefanya rejea kwa Mtumishi wa Mungu, ili kukazia haki; msamaha na upatanisho; ustawi na maendeleo kwa waja wake. Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, akahesabiwa pamoja na hao wakosao, lakini alichukua dhambi za watu wengi, na kuwaombea wakosaji!

Ecce Homo
20 April 2019, 07:46