Tafuta

Vatican News
Majandokasisi kutoka nyumba mbali mbali za Malezi, wataanza kupewa Daraja ya Ushemasi na wengine watapewa Daraja ya Upadre, Mwezi Mei 2019 hapa mjini Roma. Majandokasisi kutoka nyumba mbali mbali za Malezi, wataanza kupewa Daraja ya Ushemasi na wengine watapewa Daraja ya Upadre, Mwezi Mei 2019 hapa mjini Roma.  (ANSA)

Mashemasi ni wahudumu wa: Liturujia, Neno la Mungu na Upendo

Mei Mosi 2019 katika Kanisa kuu la Mt. Apolinari wafuatao wapewa Daraja ya ushemasi; Frt. Deogratias Method Nyamwihula wa jimbo kuu Katoliki la Mwanza na Frt. Frank John Gilagiza wa Jimbo Katoliki Kigoma. Pamoja na Frt. Atta Okyere wa Jimbo Katoliki Kumasi nchini Ghana. Atakayewadarakisha ni Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Na Karoli Joseph Amani - Vatican.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.

Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu! Mjini Roma, taifa la Mungu litakuwa na furaha hivi karibuni kwa tunu faradhi kutoka kwa Mungu, kupata idadi kubwa ya mashemasi kutoka katika vyuo mbalimbali vya kipapa mjini Roma. Mfululizo wa kutolewa Daraja takatifu la ushemasi utaanza kwa mafrateli wa Seminari Kuu ya Mama yetu wa Kikao cha Hekima (Sedes Sapientiae) iliyo chini ya Mapadre wa Kazi ya Mungu (Opus Dei) Katika siku ya Mei Mosi 2019 katika Kanisa kuu la Mt. Apolinari ambapo watapatiwa Daraja Takatifu ya la ushemasi; Frt. Deogratias Method Nyamwihula wa jimbo kuu Katoliki la Mwanza na Frt. Frank John Gilagiza wa Jimbo Katoliki Kigoma. Pamoja nao yupo Frt. Atta Okyere wa Jimbo Katoliki Kumasi nchini Ghana. Atakayewadarakisha si mwingine ni Mhashamu Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Mnamo tarehe 04 mwezi Mei 2019 ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican zitarindima nyimbo vigelegele na shangwe kutoka makabila, nchi na mabara mbalimbali ulimwenguni, kwani kwa kuwekewa mikono na sala ya kuwekwa wakfu na Kardinali Fernando Filoni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa Uinjilishaji wa Watu, watapewa Daraja takatifu ya Ushemasi mafrateli 26 wa Seminari Kuu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu (Pontificio Collegio Urbano della Propaganda Fide). Kutoka Tanzania ni Frt. Amani Karoli Joseph wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Frt. Nyebosa Alphonce Marwa wa Jimbo Katoliki Musoma na Frt. Tibanyendera Victor Lucas wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Kutoka Kenya ni Frt. Kimanjara Samuel Maina wa Jimbo Katoliki Nyahururu.

Kundi zima la watarajiwa linao waafrika 17, kutoka Bara la Amerika ya Kusini ni mmoja na Bara la Asia wapo 10 ambapo wawili kati yao ni wa Kanisa Katoliki la Mashariki (Oriental rite) la Siro Malabar (India) na watapatiwa Daraja ya Ushemaji katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Mhashamu Askofu Stephen Chirappanath (Mkaguzi wa Kitume kanda ya Ulaya) mnamo tarehe 11 mwezi Mei 2019 katika adhimisho la Ekaristi Takatifu kwa Liturujia ya Mapokeo ya Siro Malabar. Mnamo tarehe 18 Mwezi Mei 2019, shangwela na vifijo vitarindima katika Seminari Kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa (Pontificio Collegio Mater Ecclesia) ambapo Kardinali Beniamino Stella Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri atatoa Daraja ya Ushemasi kwa mafrateli 14, wakiwemo Frt. Wangwe Peter Olaka na Frt. Ladislaus Milagiro wote wawili kutoka Jimbo Katoliki Kigoma. Katika kundi lao waafrika ni watano na watano ni kutoka Bara la Amerika ya kusini na wawili ni kutoka Bara Asia.

Sanjari na matukio hayo, Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora nchini Tanzania katika Kanisa kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, atatoa Daraja Takatifu ya Ushemasi Frt. Eradius Rwegoshora na Frt. Cornelio Chaula mnamo tarehe 04 Mwezi Mei 2019. Baraka na fanaka za Mwenyezi Mungu ziwasindikize na kuwaongoza katika huduma ya Neno, Sakramenti za Kanisa na Huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu.

Daraja la Ushemaqsi 2019
30 April 2019, 11:02