Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwaangukia na kuwabusu miguu viongozi wakuu wa Serikali ya Sudan ni angalisho kwamba, uongozi ni huduma hasa kwa maskini! Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwaangukia na kuwabusu miguu viongozi wakuu wa Serikali ya Sudan ni angalisho kwamba, uongozi ni huduma hasa kwa maskini!  Tahariri

TAHARIRI: Uongozi ni huduma ya upendo kwa watu wa Mungu!

Hiki ni kitendo kinachodhihirisha kwamba, uongozi ni huduma kwa watu wa Mungu. Tukio hili linapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa Injili ya huduma ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu Francisko amewapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini, tukio ambalo limewaliza wengi, walipomwona, Baba Mtakatifu katika umri na hali yake, akililia amani Sudan ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baada ya kipindi cha sala, tafakari na upatanisho kwa ajili ya kuombea amani kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, Alhamisi jioni, tarehe 11 Aprili 2019, Baba Mtakatifu Francisko alipiga magoti kwa unyenyekevu na heshima kubwa na kuanza kubusu miguu ya viongozi wa Sudan ya Kusini, wanaotarajia kuanza utekelezaji wa muundo wa Serikali ya mpito, hapo tarehe 12 Mei 2019. Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni kielelezo cha kilio cha ndani kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Mtumishi wa watumishi wa Mungu, anayeguswa na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kutokana na vita, njaa na magonjwa.

Hiki ni kitendo kinachodhihirisha kwamba, uongozi ni huduma kwa watu wa Mungu na wala si vinginevyo na kwamba, tukio hili linapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko amewapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini, tukio ambalo limewaliza wengi, walipomwona, Baba Mtakatifu katika umri na hali yake, akililia amani Sudan ya Kusini! Andrea Tornieli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, katika Tahariri yake kuhusiana na tukio hili anakaza kusema, linakita mizizi yake katika mwanga wa Injili. Ni tukio linalowakumbusha  waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, Kristo Yesu, aliwaosha mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika Injili ya huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawasihi viongozi wa Sudan ya Kusini kama ndugu wamoja, kudumu katika amani. Matatizo na changamoto daima zitakuwepo, lakini amani nchini Sudan ya Kusini ni jambo linalowezekana kabisa! Baada ya kipindi cha sala, tafakari na upatanisho, sasa ni wakati wa kuheshimu na kutekeleza mkataba wa amani, tayari kuanza mchakato wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa! Amewakumbusha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowawajibisha kuitafuta, kuilinda na kuidumisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini.

Familia ya Mungu Sudan ya Kusini ina kiu ya kutaka kuona amani inatawala tena katika akili na nyoyo za watu, baada ya viongozi wa Serikali na Kidini kutoka Sudan ya Kusini kukubali na kuitikia wito na mwaliko kutoka kwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Mtumishi wa watumishi wa Mungu! Andrea Tornieli anakumbusha kwamba, tukio kama hili lilikwisha wahi kutokea kunako tarehe 14 Desemba 1975, Mtakatifu Paulo VI, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Kubatilisha maamuzi ya utengano wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, baada ya Misa Takatifu, akiwa amevaa mavazi ya Ibada, aliwapigia magoti wajumbe wa Kanisa la Kiorthodox chini ya upongozi wa Patriaki Dimitrios wa kwanza.

Haya ni matukio yanayowakumbusha waamini umuhimu wa kumwilisha Injili ya upendo katika huduma kwa watu wa Mungu. Hii ni changamoto ya kuendelea kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwafunda waamini, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Mababa watakatifu ambao kimsingi ni watumishi wa watumishi wa Mungu, hawaogopi wala kusita kupiga magoti, kama ushuhuda wa kumwiga Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao wa daima!

Tahariri: Tornielli

 

15 April 2019, 08:37