Tafuta

Vatican News
Papa Mstaafu Benedikto XVI anafanya kumbu kumbu ya Miaka 92 tangu alipozaliwa. Papa Mstaafu Benedikto XVI anafanya kumbu kumbu ya Miaka 92 tangu alipozaliwa.  (Vatican Media)

TAHARIRI: Hija ya toba na wongofu katika utume wa Kanisa!

Kashfa hii, ilishughulikiwa sana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI enzi ya uongozi wake. Anasema, jibu makini dhidi ya kashfa hii ni toba, wongofu wa ndani tayari kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kanisa lina asili mbili yaani ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na lina asili ya kibinadamu, kwa kuongozwa na binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, katika Tahariri yake kuhusu kumbukizi la Miaka 92 tangu alipozaliwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, anasema, limekuja wakati ambapo kuna mjadala kuhusu ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kashfa hii, ilishughulikiwa sana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI enzi ya uongozi wake. Anasema, jibu makini dhidi ya kashfa hii ni toba, wongofu wa ndani tayari kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kanisa lina asili mbili yaani ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu, Nafsi ya pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na lina asili ya kibinadamu kwa sababu Kristo Yesu amelikabidhi na kuliacha liendelee kujengwa na kuimarishwa kwa njia ya mikono ya binadamu.

Ukilitazama Kanisa kwa macho ya kibinadamu, kuna hatari kwamba, Kanisa likaonekana kuwa kama ni taasisi ya kisiasa kama zilivyo taasisi nyingine. Mbaya zaidi, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, imechafua kwa kiasi kikubwa maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha baadhi ya watu kukosa imani na matumaini kwa Kanisa la Kristo! Hii ni hatari kubwa anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Papa Francisko ameendeleza mchakato wa kukabiliana na changamoto ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Viongozi hawa wawili wanaunganishwa kwa pamoja na “hija ya toba na wongofu wa ndani”.

Andrea Tornieli katika tahariri yake anakaza kusema, jibu makini dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, haliwezi kupatikana kwa kujiaminisha katika miundo mbinu ya Kanisa hata kama ni muhimu kiasi gani! Kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizobainishwa na Mama Kanisa katika siku za hivi karibuni, au kwa kujikita katika protokali inayopaswa kutekelezwa hatua kwa hatua pamoja na kujenga mazingira salama kwa malezi na makuzi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Nyenzo mbali mbali zilizobainishwa na Mama Kanisa kwa nyakati mbali mbali ni muhimu sana, lakini kwa zenyewe haziwezi kujitosheleza hata kidogo!

Viongozi hawa wakuu wa Kanisa kwa nyakati mbali mbali wamewaandikia watu wa Mungu barua za kichungaji kuelelezea masikitiko ya Kanisa akama alivyofanya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 huko Ireland. Alisema, kulikuwa na haja ya kuwa na mwono na mwelekeo mpya, kwa kutambua kwamba, watoto ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Mwaka 2011 ukatangazwa kuwa ni mwaka wa toba na wongofu wa ndani; waamini wakasali, wakafunga na kujipatanisha na Mungu, huku wakiongozwa na Neno la Mungu.

Watu wakajisadaka na kumwilisha sala na tafakari zao katika matendo ya huruma, kuomba huruma na neema ya Mungu ili kupyaisha tena maisha na utume wa Kanisa nchini Ireland. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akakazia sana umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja tena huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo! Toba na wongofu wa ndani, ni matendo ambayo yalipaswa kuboreshwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Maisha ya Sala. Adui mkubwa wa Kanisa ni dhambi zinazotendwa na watoto wake, wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Toba na wongofu wa ndani, viwasaidie waamini kupata neema na rehema kutoka kwa Mungu, chemchemi ya imani na matumaini mapya!

Andrea Tornielli anasema, Mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko akawaandikiaujumbe watu wa Mungu nchini Chile, waliozama na kutopea katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Aliwataka waamini kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu aweze kulipyaisha tena Kanisa lake kutoka katika undani wake. Huu ni mwaliko wa kutubu kwa kuangalia udhaifu na mapungufu yaliyojitokeza, tayari kumkimbilia Kristo Yesu ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutokana na kashfa hii. Tarehe 20 Agosti 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaandika barua kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia akielezea madhara ya kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu akawataka waamini kufunga, kusali, kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuamsha tena dhamiri zinazosinzia, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kusimama kidete, ili kuimarisha sera, mikakati na utamaduni wa ulinzi kwa watoto wadogo, ili kuwajengea mazingira salama kwa malezi na makuzi yao. Ni changamoto ya kuondokana na mifumo yote inayosababisha kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Toba na wongofu wa ndani ni silaha madhubuti zinazowawezesha waamini kuonja shida na mahangaiko ya jirani zao. Waamini wawe na ujasiri wa kujinyima na kutoa kuliko kupokea!

Matumizi mabaya ya madaraka, umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko ni kati ya mambo yanayolitesa sana Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, licha ya umaarufu wa Kanisa katika maisha na utume wake, lakini bado linapaswa kushughulikia kwa ukamilifu zaidi udhaifu na dhambi za watoto wake!

Papa Mstaafu Benedikto XVI

 

16 April 2019, 10:52