Tafuta

Vatican News
Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030: nguvu ya kimaadili inahitajika kwa kuwahusisha viongozi wa dini mbali mbali duniani! Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030: nguvu ya kimaadili inahitajika kwa kuwahusisha viongozi wa dini mbali mbali duniani!  (ANSA)

Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu: nguvu ya kimaadili

Vatican inakazia: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza na dini mbali mbali duniani. Wanasayansi wanakiri kwamba, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira. Kumbe kuna haja ya kubadili: mtindo wa maisha, mfumo wa uzalishaji na ulaji, vinginevyo watu wataendelea kukumbwa na maafa kila kukicha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika hotuba yake elekezi kwa wajumbe wa mkutano kuhusu “Dini na Malengo Endelevu ya Binadamu”,  uliokuwa unafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 7-9 Machi 2019, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya maendeleo endelevu na jumuishi sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu. Anasema, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, malengo yanafikiwa kwa kujikita katika majadiliano na utekelezaji wake kwa kutambua kwamba, mambo haya yote yanategemeana na kukamilishana.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, uzingatie pia upendo kwa jirani na kwa namna ya pekee kwa watu mahalia ambao wanayonywa na kudhalilishwa kutokana na nguvu ya kiuchumi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu unapaswa kuwa ni mchakato wa kusikiliza kwa makini kilio cha dunia pamoja na maskini. Hawa ndio wakimbizi na wahamiaji, vijana na watu mahalia, ili kwa pamoja waweze kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa maendeleo endelevu na fungamani kwa kuwa na ushiriki mpana zaidi kwa ajili ya hatima yao.

Kwa upande wake, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu amekazia: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza na dini mbali mbali duniani. Anasema, wanasayansi na wataalam wa mazingira wanakiri kwamba, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira na ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kufanya mageuzi makubwa katika mtindo wa maisha, mfumo wa uzalishaji na ulaji, athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kiwango cha joto duniani kinaendelea kupanda na hivyo kutishia usalama wa maisha, ustawi na maendeleo ya watu! Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 unazingatia kilio cha maskini duniani pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu Kumi na Saba, yaliyobainishwa na nchi 190 wanachama wa Umoja wa Mataifa yanapania kwa namna ya pekee kabisa: kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na ekolojia duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ni njia inayoielekeza Jumuiya ya Kimataifa, kusimama kidete: kulinda na kudumisha, utu na heshima ya binadamu kama inavyofafanuliwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Utekelezaji huu, unahitaji pia kuungwa mkono na kanuni maadili na utu wema; mambo msingi yanayosimamiwa na dini mbali mbali duniani. Dini zinaweza kusaidia utekelezaji huu kwa kuzingatia kwamba walau asilimia 80% ya watu wote duniani ni wachamungu na wanazo dini wanazoamini. Kumbe, maamuzi katika maisha yao yanaweza kuwa na athari kubwa katika mahusiano na mafungamano na jirani zao pamoja na mazingira katika ujumla wake.

Kardinali Peter Turkson anaendelea kufafanua kwamba, waamini wanaweza kusaidia katika mchakato wa maboresho ya maisha pamoja na kuenzi jumuiya zao, ili ziweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Wanaweza pia kusaidia utunzaji bora wa mazingira, kwani hii ni sehemu ya kazi ya uumbaji. Kanuni maadili na utu wema ni muhimu sana kwa ajili ya utunzaji wa mazingira, ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu asema kwamba, wajumbe wa mkutano kuhusu “Dini na Malengo Endelevu ya Binadamu” wanakiri kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzishirikisha dini mbali mbali kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu!

Kardinali Turkson: Malengo

 

12 March 2019, 10:06