Tafuta

Vatican News
Tafakari za kipindi cha Kwaresima 2019: Maboresho ya maisha ya kiroho! Tafakari za kipindi cha Kwaresima 2019: Maboresho ya maisha ya kiroho!  (Vatican Media)

Tafakari za kipindi cha Kwaresima 2019: Maisha ya kiroho!

Padre Cantalamessa amekazia zaidi kuhusu: Kuchechemea kwa tunu msingi za maisha ya kiroho; ukweli wa maisha mintarafu Mapokeo kutoka katika Maandiko Matakatifu; umuhimu wa kurejea katika undani wa maisha; na kwamba, Kristo Yesu kama mfano bora wa kuigwa katika mchakato unaomwezesha mwamini kuingia katika undani wa maisha yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 zinaongozwa na kauli mbiu "In te ipsum redi" yaani “Ingia ndani mwako” mwaliko kwa waamini kuingia katika undani wa maisha yao, kwa kuondokana na mahangaiko na changamoto za maisha, ili hatimaye, kupata amani na utulivu wa ndani; kwa kugundua na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika undani wa maisha yao na Walatini wanasema "Coram Deo". Ukweli wa maisha umejikita katika undani wa mtu!

Sehemu ya kwanza ya mahubiri haya, tarehe 15 Machi 2019, Padre Cantalamessa aliwataka waamini kuachana na tabia ya unafiki kwa kutaka kujikweza na badala yake, wakite maisha yao katika toba na wongofu wa ndani, ili kujenga nyoyo safi, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu! Katika mahubiri yake, sehemu ya pili, tarehe 22 Machi 2019 Padre Cantalamessa amekazia zaidi kuhusu: Kuchechemea kwa tunu msingi za maisha ya kiroho;  ukweli wa maisha mintarafu Mapokeo kutoka katika Maandiko Matakatifu; umuhimu wa kurejea katika undani wa maisha; na kwamba, Kristo Yesu kama mfano bora wa kuigwa katika mchakato unaomwezesha mwamini kuingia katika undani wa maisha yake!

Itakumbukwa kwamba, Tafakari hizi za Kipindi cha Kwaresima zinahudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wanaoishi mjini Roma. Waamini wanahamasishwa kuingia katika undani wa maisha yao, kuangalia mahali walipojikwaa na kuanguka; vivuli vinavyowasonga katika maisha kiasi hata cha kushindwa kuona ile sura ya Mungu katika maisha yao! Mwanadamu anayo kiu ya kutaka kuonana na Mwenyezi Mungu katika: Maandiko Matakatifu, Sakramenti na katika Kanisa lenyewe kama Sakramenti ya wokovu. Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kuingia katika undani wa maisha, ili kugundua uwepo endelevu wa Mungu.

Zakayo tajiri na mtoza ushuru, awe ni mfano bora wa kuigwa katika jitihada za kumtafuta Kristo Yesu katika maisha, ili awapatie fursa ya toba, wongofu wa ndani, msamaha wa dhambi na hatimaye, wokovu! Waamini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuchechemea kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na matokeo yake ni kuzagaa kwa dhana ya “ukweli” unaofumbatwa katika maoni binafsi. Ukweli kwamba, mwanadamu ameumbwa katika mwili na roho hauna tena mashiko, watu wengi wanataka kujitafuta wenyewe ili kuweza kushibisha tamaa za milango ya fahamu kama anavyosema Mhubiri: 1:8. Masuala ya kijamii, yanaangaliwa pia kwa “jicho la kengeza” kiasi hata cha kutothamini utu na heshima ya binadamu. Ukweli kuhusu maisha ya kiroho ni kazi ambayo kwa sasa inafanywa na wanasaikolojia na wapembuzi wa mambo ya kisaikolojia, kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu hana tena nafasi katika undani wa maisha ya mwanadamu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wanalitaka Kanisa kutokimbia ulimwengu, bali kujikita katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, kwa kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu aliye hai katika maisha ya mwanadamu, ushuhuda endelevu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho. Ukweli wa maisha ya kiroho mintarafu Mapokeo kutoka katika Maandiko Matakatifu unaendelea kufutika taratibu katika maisha ya watu, changamoto kama walivyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni kuanza kujikita katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa: Kwanza kabisa kwa kuboresha maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ili kweli watu waweze kumwabudu Mungu kutoka katika undani wa mioyo yao, ili kujenga na kudumisha umoja na tunu msingi za maisha ya kiroho; Hekalu la Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika undani wa maisha yao kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amefanya makao katika nyoyo zao! Kuna umuhimu wa kurejea tena katika ujenzi wa maisha ya kiroho kwa kujikita katika ukimya wa ndani, ili kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu aweze kuzungumza na mja wake. Padre Cantalamessa anakaza kusema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, hata leo hii kuna Mafarao wanaoamrisha dunia kutokana na nguvu zao za kiuchumi, matangazo ya biashara, raha na starehe! Matokeo yake ni vijana na watu wengi kugeuzwa kuwa ni watumwa wa ulaji wa kupindukia!

Ni wakati wa kutoa nafasi kwa Mungu katika: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na matukio ambayo yataweza kuwakutanisha vijana, ili kuboresha maisha yao ya kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia sababu za mafanikio au kushindwa kwao katika maisha, kwa mwanga wa uwepo wa Mungu ndani mwao, “Coram Deo” katika unyenyekevu! Wongofu wa ndani, uwawezeshe waamini kutambua hali yao ya maisha ya kiroho! Kwaresima ni kipindi cha kufunga na kusali; kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuwaweka huru kutoka katika utumwa wa malimwengu. Je, Sheria ya Ukimya “Silentium” katika nyumba za watawa imefutwa? Leo hii watu wanasogoa kwa simu hadi usiku wa manane!

Kwaresima ni fursa ya kumwona Mungu kati ya maskini, katika Ekaristi Takatifu na kutenda kwa ajili ya kumtukuza Mungu, asili ya maisha na wema wote! Huu ni wakati wa kuchuchumilia mambo msingi ya maisha ya kiroho, kwa kujiweka wazi mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu. Ni muda wa kusali na kutafakari pamoja na kujisadaka kwa ajili ya ya huduma kwa Kanisa!

Padre Cantalamessa
22 March 2019, 17:29