Tafuta

Vatican News
Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 inaongozwa na kauli mbiu "Si wahamiaji peke yao"! Itaadhimishwa 29 Septemba 2019 Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 inaongozwa na kauli mbiu "Si wahamiaji peke yao"! Itaadhimishwa 29 Septemba 2019 

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2019: Kauli mbiu!

Huduma, upendo na mshikamano wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Anaguswa kwa namna na shida pamoja na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Si Wahamiaji peke yao”. Hii ni tema ambayo imefafanuliwa hivi karibuni na Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi wa Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu na fungamani. Baba Mtakatifu  Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashiriksha.

Waamini wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kumtambua Kristo Yesu kati ya wakimbizi na wahamiaji wa nyati zote, ili kuweza kumfungulia malango ya maisha na nyoyo, ili kumkaribisha na kumkarimu. Huduma, upendo na mshikamano wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Anaguswa kwa namna na shida pamoja na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitaabisha kumtambua na kumhudumia Kristo Yesu anajifunua kati ya wakimbizi na wahamiaji; maskini na wagonjwa, hata kama macho yao, yanapata taabu sana kumtambua!  Hii pengine, inatokana na mavazi chakavu anayovaa; miguu yake iliyochafuka kwa tope kutokana na kutembea kwa muda mrefu ili kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi; au kutokana na uso wake kuvimba kwa sababu ya kutembea kwenye jua kali na hivyo kupigwa na upepo mkali; au kwa kuangukiwa na theluji kali!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, pengine watu wanashindwa kumtambua Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji kutokana na madonda makubwa wanayobeba mwilini wao kutokana na vipigo, dhuluma na nyanyaso wanazokumbana nazo njiani; au kwa vile tu, wanashindwa kuzungumza lugha ya mahali wanapopata hifadhi. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, chimbuko lake ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu.

Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mikakati ya Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na sababu za kichungaji akaamua Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji iadhimishwe Jumapili ya Pili ya Mwezi Septemba na sasa ameridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwamba, Siku hii iadhimishwe Jumapili ya mwisho ya Mwezi Septemba.

Kumbe, kwa mwaka 2019, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji inaadhimishwa tarehe 29 Septemba. Mabaraza ya Maaskofu yanapewa angalisho, ili kuzingatia marekebisho haya yaliyoridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kusaidia kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa mintarafu huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji duniani.  Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu na fungamani itaendelea kuragibisha huduma ya upendo kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, ili kuwasaidia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kupata uelewa mpana zaidi wa tema zinazochaguliwa na Baba Mtakatifu.

Siku ya Wakimbizi Duniani 2019
11 March 2019, 10:44